Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwansha Mwenge wa Uhuru kuzindua
mbio zake kwenye uwanja wa Magogo mjini Geita, Aprili 2, 2018 Kushoto
ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana,
Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Mwenge wa Uhuru
kiongozi wa vijana sita watakaokimbiza Mwenge huo,Charles Kabeho wakati
alipozindua mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye uwanja wa Magogo mjini
Geita, Aprili 2, 2018. Wapili kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
………………
*Ataja mikoa saba inayoongoza kwa utoro wa wanafunzi
shuleni
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa
mikoa ya Tabora, Geita, Mtwara na Shinyanga ambayo inaongoza kwa utoro wa
wanafunzi kwa shule za sekondari wahamasishe umuhimu wa elimu na mahudhurio
endelevu shuleni.
“Kwa ujumla utoro wa wanafunzi wa Sekondari ni
mkubwa zaidi kwa Mikoa husika kuliko shule za msingi. Nitumie nafasi hii
kuikumbusha Mikoa niliyoitaja kuhamasisha wananchi wakiwemo wazazi, walezi na
wanafunzi wenyewe kuhusu umuhimu wa elimu na mahudhurio shuleni.”
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Aprili
02, 2018) wakati akizindua mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 katika uwanja
wa Magogo mkoani Geita. Kaulimbiu ya mbio za mwenge kwa mwaka huu ni ‘Elimu ni
ufunguo wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu.’
Waziri Mkuu amesema dhamira ya Serikali kupitia
kaulimbiu hiyo ni kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo
kuwekeza katika elimu na kuzalisha rasilimali watu yenye ujuzi na stadi
zitakazowezesha kuchochea mapinduzi ya viwanda ili nchi iwe ya uchumi wa kati
ifikapo 2025.
Akizungumzia kuhusu utoro kwa shule za sekondari
nchini, Waziri Mkuu amesema mkoa wa Tabora ndio unaongoza kwa utoro kwa kuwa na
silimia 9.7,
Geita asilimia 8.1, Mtwara asilimia 6.4 na Shinyanga
asilimia 6.3.
Kuhusu utoro wa wanafunzi wa shule za Msingi nchini,
Waziri Mkuu amesema mkoa unaoongoza ni wa Rukwa kwa asilimia 3.2, Geita
asilimia 3.1, Tabora asilimia 2.9, Simiyu asilimia 2.0 na Singida
asilimia1.9.
Amesema mikoa yenye kiwango kikubwa cha utoro wa
wanafunzi na kuacha shule ihakikishe mahudhurio yanadhibitiwa shuleni ili
kuhakikisha wanafunzi wote wanaoandikishwa wanahudhuria, wanasoma na kuhitimu
ngazi husika.
“Ukitaka kuleta maendeleo ya uchumi ulio imara,
ukitaka kujenga jamii inayo heshimu na kufuata misingi ya uwajibikaji na
ubunifu, ukitaka kujenga Taifa lenye amani na utulivu, lazima uwekeze zaidi
katika elimu”.
“Kwa hiyo, uwekezaji katika elimu haumaanishi tu
kuhakikisha watoto wetu na Watanzania kwa jumla wanapata haki yao ya msingi
bali ni kuweka misingi imara itakayo liwezesha Taifa na mtu binafsi kufikia
hatua bora ya maisha”.
Waziri Mkuu amesema ili kuhakikisha Taifa linafikia
viwango bora vya elimu, Serikali ya awamu ya tano inyoongozwa na Rais Dkt. John
Magufuli, imedhamilia kuboresha elimu katika ngazi zote nchini, kuanzia Elimu
ya Awali hadi Elimu ya Juu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa mbio
za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zitaendelea kuhimiza mapambano dhidi ya rushwa kwa
sababu bado ipo na inaendelea kuwa ni adui wa haki na kudhoofisha jitihada za
Serikali za kuimarisha uchumi, kuimarisha huduma za jamii na Utawala bora.
Amesema athari zinazotokana na vitendo vya rushwa
huwaathiri watu wa kawaida zaidi na kuendelea kubaki wanyonge katika jamii,
hivyo Serikali itaendelea kupambana na vitendo vya rushwa bila kuchoka mpaka
jamii itakapoachana na vitendo hivyo vya kidhalimu.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bibi Jenista Mhagama alisema Mwenge
wa Uhuru utakimbizwa umbali wa takribani kilomita 103,440.7 kwa siku 195 katika
mikoa yote 31 nchini na halmashauri za wilaya 195.
Alisema kazi hiyo itafanywa na vijana sita kutoka
Tanzania Bara na Zanzibar ambao wameandaliwa kikamilifu ili kuhakikisha
wanaendelea kuwakumbusha Watanzania historia ya falsafa ya Mwenge wa Uhuru,
kufikisha kwa ufasaha ujumbe wa mwaka huu na kukagua na kuzindua miradi ya
maendeleo kwa umakini.
Bibi Jenista alisema mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka
2018 zinaongozwa na Bw. Charles Kabeho kutoka mkoa wa Dar es Salaam
akishirikiana na Bw. Issa Abasi Mohamed (Kusini Pemba), Bi. Agusta Safari
(Geita), Bw. Ipyana Mlilo (Tanga), Bw. Dominick Njunwa (Kigoma) na Bi. Riziki
Hassan Ali (Kusini Unguja).
Naye, Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo
– Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Ali Abeid Karume alisema atahakikisha
ujumbe wa Mwenge wa Uhuru unawafikia wananchi wote pamoja na kupita katika
miradi yote ya maendeleo iliyopangwa.
Balozi Karume ametumia fursa hiyo kuwapongeza Rais
Dkt. Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein kwa jitihada
zao za kudumisha amani, utulivu, kuwaletea wananchi maendeleo bila ya ubaguzi
pamoja na kupambana na maadui wanaotaka kudhoofisha maendeleo nchini.


0 Comments