Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dr. Augustine Mahiga
akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alipofika nyumbani kwake Bara bara ya Haile Selassie Jijini Dar es salaam
kubadilishana mawazo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisisitiza
jambo wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Balozi Dr. Augustine Maiga akiwa kwenye Makaazi yake Bara bara
ya Haile Selassie Jijini Dar es salaam.
.......................................................
Waziri
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. Augustine Mahiga amesema
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itasimamia ipasavyo na kuhakikisha kwamba
nia ya Mahujaji wa Tanzania waliojiandikisha kwenda kutekeleza Ibara ya Hijja
Nchini Saudi Arabia Mwaka huu inatimia.
Amesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inafuatilia
hatua za mwisho katika kuona tatizo lililojitokeza kwa baadhi ya Taasisi za Usafirishaji
Mahujaji upande wa Tanzania Bara kukabiliwa na madeni Nchini Saudi Arabia
linapata ufumbuzi wa haraka kabla ya kumalizika kwa muda wa mwisho wa
uthibitisho wa Mahujaji wa Mwaka huu.
Balozi Dr. Augustine Mahiga amesema hayo wakati alipofika katika Makazi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Bara bara ya Haile Selassie
Jijini Dar es salaam kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya Hijja yaliyoleta
usumbufu mwaka jana kwa Mahujaji wa Tanzania.
Amesema atalazimika kuzungumza na Mufti Mkuu wa Tanzania pamoja na
Uongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) ili kujua hatua
walizofikia katika kuona Taasisi zinazosimamia usafirishaji Mahujaji upande wa
Bara wamemaliza matatizo yanayowakabili.
Balozi Mahiga alimthibitishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uongozi
wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki utalazimika kutoa
baraka kwa Mahujaji wanaosimamiwa na Taasisi za Zanzibar kwanza wakati zile za
Tanzania Bara zitashugulikiwa baadaye
baada ya kumaliza changamoto zao.
Hatua ya Balozi Mahiga imekuja kufuatia baadhi ya Taasisi za Usafirishaji Mahujaji
za Tanzania Bara kushindwa kulipa Madeni na kupelekea Wizara inayosimamia
masuala ya Hijja Nchini Saudi Arabia kutishia kuzuia Mahujaji wa Tanzania
kuingia Nchini humo kwa Ibada ya Hijja Mwaka huu.
Akigusia Miradi ya Kiuchumi inayolenga kustawisha maendeleo ya Tanzania Waziri
wa Mambo ya Nje na Afrika Mashariki Balozi Mahiga alisema ipo haja ya kufuatilia
Miradi iliyopata Mikopo na ufadhili wa Kimataifa ili kujua maendeleo yake.
Balozi Mahiga aliitaja baadhi ya Miradi hiyo ni pamoja na ile ya Ujenzi wa Bandari ya Maruhubi
kwa Mpiga Duri Kisiwani Unguja na ile ya Bandari ya Wete Kisiwani Pemba ambayo imo ndani
ya Mpango Mkuu wa Miradi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alimpongeza Balozi Maiga kwa hatua alizoamua kuzichukuwa za kukabiliana na
changamoto zilizojitokeza kwenye masuala ya Hijja.
Balozi Seif alisema Ibada ya Hijja ni miongoni mwa Nguzo Tano wanazowajibika
Waumini wa Dini ya Kiislamu wenye uwezo kuzitekeleza ambayo imo ndani ya Imani
za Waumini jambo ambalo wasimamizi wa masuala hayo wanalazimika kuwa makini
katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akielezea furaha yake kutokana na uamuzi wa Tanzania kuweka nia ya kutaka kufungua
Ubalozi wake Nchini Jamuhuri ya Cuba, Balozi Seif alisema hatua hiyo
muhimu itaongeza chachu ya uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya Tanzania na
Cuba.
Balozi Seif alisema Cuba ni Taifa la kwanza lililoyatambua na kuyaunga mkono Mapinduzi
ya Zanzibar ya Mwaka 1964 na imekuwa ni mshirika mkubwa kwa Tanzania hasa
katika kusaidia Taaluma kwenye miradi iliyomo ndani ya Sekta zaKilimo, Afya na
hata masuala ya Viwanda.
Habari na picha kwa hisani ya Ofisi ya Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar na
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki-Ofisi ya Zazibar
26/06/2018



0 Comments