Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB Plc Sabasaba Moshingi akizungumza na wafanyakazi waliokuwa Twiga Bancorp pamoja na wateja wa benki hiyo jijini Dar es Salaam wakati anawakaribisha rasmi kutokana na Benki Kuu ya Tanzania(BoT),kuziunganisha benki hizo.
Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya Windhoek Tanzania Simon Salatiel ambaye ni moja ya wateja wa iliyokuwa benki ya Twiga Bancorp akitoa shukrani zake jijini Dar es Salaam baada ya benki hiyo kuunganishwa na benki ya TPB Plc.
Wafanyakazi wa Benki ya TPB Plc(kulia), wakibadilishana mawasiliano baada ya benki hiyo kuwakaribisha rasmi waliokuwa wafanyakazi wa benki ya Twiga Bancorp ambapo kwa sasa zimeunganishwa.
Moja ya wateja wakubwa wa Benki ya Twiga Bancorp (kulia) akisalimiana na baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya TPB Plc jijini Dar es Saalaam baada ya kufanyika hafla iliyoandaliwa na benki ya TPB kuwakarabisha wateja na wafanyakazi wa Twiga kutokana na uamuzi wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT)kuziunganisha benki hizo.Katikati ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB Plc Sabasaba Moshingi.
Picha zote na Prona Mumwi
Picha zote na Prona Mumwi
...................................................................
Na Mwandishi Wetu
OFISA Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB Plc
Sabasaba Moshingi amewatoa hofu wateja wote waliokuwa kwenye benki ya Twiga
Bancorp huku akiwahakikishia kuwa wapo katika mikono salama na wataendelea
kupata huduma kama hapo awali.
Moshingi ametoa kauli hiyo jijini Dar es
Salaam jana baada ya benki ya TPB kuandaa hafla fupi ya chakula cha jioni kwa
ajili ya kuwakaribisha wateja na wafanyakazi waliokuwa kwenye benki ya Twiga
Bancorp.
Kwa kukumbusha tu benki ya TPB na Twiga
Bancorp zimeunganishwa Mei 17 mwaka huu baada ya Benki Kuu ya Tanzania(BoT)
kutoa tamko rasmi.
"Hakuna kilichobadilika, huduma
zitabaki pale pale, wateja wote mtaendelea kuhudumiwa katika matawi ya
iliyokuwa benki ya Twiga Bancorp mpaka kipindi cha mpito kikimalizika.
"Kipindi cha mpito tulichopewa na
BoT ni miezi mitatu, ambayo itatupa nafasi kuweka mitandao ya benki hizi pamoja
na kurahisisha katika kutoa huduma za kibenki,"amesema Moshingi.
Kwa upande wake aliyekuwa Meneja
Msimamizi wa iliyokuwa Benki ya Twiga Bancorp, Nkanwa Magina kutoka Benki Kuu
ya Tanzania, amewataka wateja waliokuwa Benki ya Twiga Bancorp kutokuwa na
wasiwasi, kwa kuwa kuunganishwa kwa benki hizo mbili kumeongeza nguvu katika
utendaji wa kutoa huduma za kibenki.
Pia amesema wafanyakazi waliokuwa katika
benki ya Twiga Bancorp, waendelee na moyo ule ule waliotoka nao kwenye benki
yao na kuonesha ushirikiano wa dhati wa wafanyakazi pamoja na wateja wa benki
ya TPB.
Wakati huo huo waliokuwa wateja wa benki
ya Twiga Bancorp, wametoa shukrani zao kwa uamuzi uliofanywa na Benki Kuu ya
Tanzania kwa kuunganisha benki hizo mbili, kwani ni faraja kwao na kusisitiza
watapata huduma kwa ufanisi zaidi.
"Tunapenda kutoa shukrani zetu za
dhati kwa Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Serikali ya Awamu ya tano kwa uamuzi
huu waliouchukuwa wakuunganisha benki hizi mbili kwani umetuondolea wasiwasi
sisi tuliokuwa wateja wa Twiga Bancorp,"amesema mteja aliyefahamika kwa
jina la Janet Mmari.

0 Comments