NA TIGANYA VINCENT
TABORA
MKUU wa Mkoa wa Tabora
Aggrey Mwanri amewataka Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Tabora, Uyui na
maeneo mengine kuhakikisha wanasaidia kudhibiti uuzaji holela wa chakula
unaofanywa na baadhi ya wananchi bila kujiwekea akiba kwa ajili ya siku za
baadaye.
Hatua hiyo inalenga
kuhakikisha kuwa kila familia iwe na akiba ya chakula ambacho kitaweza kuwafikisha
mavuno ya msimu ujao bila kuomba msaada
Serikalini.
Mwanri alitoa kauli
hiyo jana wilayani Uyui wakatika wa Kikao Maalumu cha Baraza la Madiwani
kilichokuwa kinapitia mambo mbalimbali ikiwemo uhifadhi wa mazingira na chakula
na kupitia taarifa za miradi mbalimbali.
Alisema utaratibu
wa uuzaji wa chakula utakuwa kwa kila kaya kujaza fomu maalumu ambayo
itaoonyesha chakula alichovuna msimu huu , matumizi yake kwa mwaka na ziada
iliyobaki na ndipo ataweka sahihi ya kukiri taarifa kabla ya kuruhusiwa kuuza.
Mwanri alisema
lengo la kufanya hivyo kutaka kuwabana wale wote wenye tabia ya kuuza ovyo ovyo
chakula na kikiisha wanakimbilia kuomba msaada Serikalini wakati wenyewe ndio
hawakuchukua tahadhari.
Alisema pia mavuno
ya mwaka huu kwa mahindi yanaweza yasiwe mazuri kutokana na mazao hayo
kushambuliwa na wadudu , kwa hiyo ni vema watu wakachukua tahadhari mapema.
Mwanri alisema
hamkatalii mtu kuuza mazao yake lakini akiwa Kiongozi wa Mkoa anabeba dhamana
ya kuhakikisha usalama wa wananchi ukiwemo wa chakula ndio maana anataka
atakayeuza awe kweli ana akiba ya kutosha ili isije ikafika wakati wa njaa
anaandamana kwenda Mkoani kuomba msaada.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tabora,
Uyui, Said Ntahondi aliwataka Madiwani kuhakikisha wanasimamia
maelekezo ya Mkuu wa Mkoa ya utunzaji wa chakula na kwa kushirikiana na
Watendaji katika maeneo yao ili waweze kutoa taarifa ambazo ndio zitawapa fursa
ya kukubaliwa kuuza au kutouza.
Alisema mtu
atakayeruhusiwa kuuuza chakula ni yule kweli ambaye anacho chakula cha kutosha
familia yake kwa mwaka mzima na awe na ziada iliyothibitika.
Katika hatua nyingine
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Tabora , Uyui limekubalina kuwa
kuanzia sasa kila familia lazima iwe na msitu wake na kila kijiji kiwe na msitu
wake kama juhudi za kulinda mazingira.
Ntahondi alisema hatua hiyo itasaidia
katika kuhakikisha jamii inaanzakuwa na uwelewa mzuri kuhusu faida ya misitu na
kukabiliana na wavamizi wa mistu.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora
aliwaagiza Madiwani na Watendaji mbalimbali kuhakikisha wanasimamia Sheria
katika kulinda hifadhi za mistu na vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi mzuri wa
Mkoa huo.
Aliongeza kuwa katika maeneo ya miji na barabara ambayo viti hajapandwa ni vema
ikapanda ili kuipendezesha miji na kulinda mazingira.


0 Comments