*Aonya wakulima wasiwauzie chomachoma, ataka wasubiri minada
*Akabidhi mikopo kwa akina mamalishe na babalishe
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya wakulima wa ufuta wasikimbilie kuuza zao hilo kwa wanunuzi wasio rasmi maarufu kwa jina la chomachoma bali wasubiri minada itangazwe mwezi ujao.
“Ninawasihi
msikubali kuuza kwa akina chomachoma bali tumieni Mfumo wa Stakabadhi
za Mazao Ghalani, tumeona mfumo huu ulivyosaidia kwenye korosho,”
amesema.
Waziri
Mkuu ametoa onyo hilo leo (Ijumaa, Mei 25, 2018) wakati akizungumza na
wananchi mara baada ya kukagua uwanja mpya wa michezo unaojengwa katika
kijiji cha Dodoma, kata ya Nachingwea, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
“Kuna
wawakilishi wa Kampuni ya Hyseas International Investment (T) Limited
ya kutoka China ambao wamekuja hapa kuonana na uongozi wa Halmashauri.
Wamesema watanunua ufuta wote uliolimwa Ruangwa na Nachingwea, ndiyo
maana ninawasihi msubiri, msikimbiile kuuza ufuta kwa sasa,”
alisisitiza.
Alisema
kampuni hiyo imeahidi kuweka vituo vya ununuzi kwenye kata za Mandawa,
Nanjaru, Nangurugai, Machang’anja hadi Mbangala ili wakulima
wasihangaike kusafirisha ufuta wao. “Tunataka mwaka huu, wakulima wa
ufuta nao wapate hela nzuri,” alisema.
Wakati huohuo, Waziri
Mkuu amekabidhi mikopo kwa wajasiriamali 42 wanaofanya kazi zao
wilayani Ruangwa ambapo kati yao akinamama lishe ni 39 na akinababa
lishe ni watatu.
Mkurugenzi
wa kampuni ya Ruangwa Distributors ambayo imetoa mikopo hiyo, Bw.
Abdallah Mang’onyola alisema wajasiriamali 30 kati ya 42, wamepokea
mikopo ya sh. 200,000 na 12 waliobakia wamepokea mikopo ya sh. 250,000.
Alisema
wajasiriamali hao wanatoka kwenye kata saba za Matambalale,
Narung’ombe, Mbekenyera, Chibula, Namichiga, Mandawa na Nambilanje.
Akizungumza
na wajasiamali hao pamoja na wnanchi waliofika kwenye hafla hiyo fupi,
Waziri Mkuu alimshukuru Mkurugenzi wa Ruangwa Distributors kwa kutoa
mikopo hiyo yenye masharti nafuu na isiyo na riba.
Waziri
Mkuu alisema hii ni mara ya pili kwa wajasiriamali wa Wilaya hiyo
kupatiwa mikopo. Alitumia fursa hiyo kumshukuru Bw. Mpaluka Hashim
Mtopela wa kampuni ya Sasalema ambaye awali alitoa mikopo ya sh. milioni
25 kwa wajasiriamali 89.


0 Comments