Random Posts

TACAIDS-Tupambane na Maambukizi Mapya ya Ukimwi ili Kuondoa Ukimwi 2030

 Kaimu mkurugenzi mtendaji wa Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS ),Jumanne Issango ,akifungua mkutano ulioandaliwa na Tume hiyo kwa lengo la kupitia mipango kazi ya utekelezaji wa afua za ukimwi kwa asasi mwamvuli, mitandao ya watu wanaoishi na virusi/ Ukimwi pamoja na sekta binafsi, Mjini Kibaha Mkoani Pwani
 Baadhi ya washiriki wakisikiliza jambo kwa makini wakati wa mkutano ulioandaliwa na Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kwa lengo la kupitia mipango kazi ya utekelezaji wa afua za ukimwi kwa asasi mwamvuli, mitandao ya watu wanaoishi na virusi/ Ukimwi pamoja na sekta binafsi, Mjini Kibaha Mkoani Pwani.
Picha ya pamoja ya washiriki waliohudhuria mkutano ulioandaliwa na Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kwa lengo la kupitia mipango kazi ya utekelezaji wa afua za ukimwi kwa asasi mwamvuli, mitandao ya watu wanaoishi na virusi/ Ukimwi pamoja na sekta binafsi, Mjini Kibaha Mkoani Pwani.
Picha na Mwamvua Mwiny-Mtazamo News
………
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
TUME ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), imeitaka jamii kukataa maambukizi mapya ya Ukimwi pamoja na taasisi mwamvuli kuhakikisha zinapanga mipango mkakati ili kuondokana na maambukizi hayo ifikapo 2030.
Aidha imewaasa wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo (ARVs) kikamilifu, badala ya kukatisha dozi na kukimbilia kwa waganga wa kienyeji, kwani kwa kufanya hivyo kusababisha madhara na vifo dhidi yao.
Hayo yalisemwa na kaimu mkurugenzi mtendaji wa TACAIDS ,Jumanne Issango ,wakati akifungua mkutano ulioandaliwa na Tume hiyo kwa lengo la kupitia mipango kazi ya utekelezaji wa afua za ukimwi kwa asasi mwamvuli, mitandao ya watu wanaoishi na virusi/ Ukimwi pamoja na sekta binafsi, Mjini Kibaha Mkoani Pwani.
Issango alibainisha, malengo ya kitaifa ni kuwa na 90 tatu, ambapo  asimilia 90 ya kwanza ni ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi nchini ambao bado hawajajitambua afya zao kuhakikisha wawe wamepima ifikapo mwaka 2020.
Pia ,wanaoishi na virusi vya ukimwi ifikapo 2020 wawe wameingia katika kutumia dawa za kufubaza VVU na ifikapo mwaka huo asilimia 90 ya ambao wanatumia dawa hizo wawe na virusi vilivyokuwa tayari vimefubaa.
Kwa mujibu wa kaimu huyo, malengo hayo ni makubwa na ndio maana wameitana ili kila mmoja katika asasi yake aone namna watakavyoshirikiana kutimiza 000 na ifikapo 2030 kuondoa maambukizi mapya ya UKIMWI,Unyanyapaa na Vifo.
Alisema waliogundulika na maambukizi ya VVU ni vyema wakafuata masharti ya daktari na kutumia dawa bila kufanya mzaha wala ajizi.
Issango alieleza ,wapo baadhi ya wenye virusi hivyo, ambao hawakuona umuhimu wa kufuata masharti wanayopewa jambo limewasababishia kupoteza maisha yao.
“Sio rahisi kumaliza ukimwi kabisa ifikapo 2030 lakini kwa kufanya kazi kwa makundi yote ,kupima afya zetu bila uoga, kuacha kuambukizana kwa makusudi, kutumia dawa kikamilifu, kuacha ngono zembe ,kwa hakika tutafikia malengo hayo”alisisitiza Issango.
Alieleza , malengo ya kitaifa ni kufikia watu katika upimaji na kuwaingiza katika dawa na kuhakikisha kunakuwa na ufuasi mzuri wa matumizi mazuri ya dawa hizo.
Nae Mwenyekiti wa chama cha walimu wanaoishi na VVU/UKIMWI (TAPOTI –Taifa) Mwl.Helen Masao, alisema walimu wengi ni waoga wa kupima afya zao.Alisema wapo ambao wameshapima lakini wanapenda kuhahama kwenye CTC walizoanza na kuhamia kwenye maeneo ,ama wilaya na mikoa mingine kwa lengo la kujificha wasijulikane.
Masao alisema hali hiyo inasababisha baadhi ya walimu hao kuambukiza wengine ama wanafunzi ambao wanakubaliana kwenye mahusiano ya kimapenzi.
Aliishukuru CWT kwa ushirikiano wao na kuitaka kuendelea kutambua na kujali walimu walio na maambukizi ya virusi vya Ukimwi .
Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji mtandao wa wanawake wanaoishi na VVU Tanzania ,Joan Chamungu alieleza asasi yao ikabiliwa na changamoto ya raslimali fedha, watu kuuzoea Ukimwi kuuona ni ugonjwa wa kawaida na Unyanyapaa has Vijijini.
Mwakilishi kutoka Restless Development Youth Organization ,Chuo kikuu cha ardhi Dar es salaam ,Bi Salome Jacob alisema baadhi ya vijana wanapata maambukizi mapya ya Ukimwi kutokana na tamaa na wengine kushawishika kufanya mapenzi na walimu ili kufaulishwa katika masomo yao.
“Wanafunzi wa kike vyuoni wapo wanaoshinikizwa kufanya tendo la ndoa na walimu ambao wengine tayari wameambukizwa, hivyo kusababisha mlolongo mkubwa wa maambuki mpaya kwa wanachuo”alisema Salome.
Salome alisema asasi yao unahahakisha kuna maendeleo chanya kwa vijana hasa vyuoni na kutoa elimu dhidhi ya kuepuka ugonjwa wa Ukimwi ili kufikia malengo ya kitaifa ya kupambana na ugonjwa huo.
Taasisi mwamvuli zilizoshiriki katika mkutano huo ni Baraza la Taifa la NG’O (NACONGO), Chama cha waajiri Tanzania (ATE), Chama cha walimu wanaoishi na VVU/UKIMWI (TAPOTI),TUCTA, Tanzania private sectors foundation (TPSF),Restless na Baraza la hiari la maendeleo ya jamii (TACOSODE).

Post a Comment

0 Comments