Subscribe Us

header ads

Wanawake Wajasiriamali Anzisheni Viwanda Vidogo Vidogo-Mgonja

 Mjumbe wa baraza Kuu la umoja wa wanawake Tanzania (UWT) mkoani Pwani ,Nancy Mutalemwa akizungumza katika mafunzo ya kujengewa uwezo kwa Jukwaa hilo ,Kibaha Mjini yaliyoandaliwa na kampuni ya Ae General Business Co Ltd.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
 Baadhi ya akinamama wajasiriamali mjini Kibaha wakisikiliza jambo,wakati walipokuwa wakipatiwa  mafunzo ya kujengewa uwezo kwa Jukwaa hilo ,Kibaha Mjini yaliyoandaliwa na kampuni ya Ae General Business Co Ltd.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Mkurugenzi wa Ae General Business Co Ltd Alexander Malya,(Wa Kushoto aliyesimama) akimsikiliza Katibu Wa jukwaa la  uwezeshaji Wanawake Mkoani Pwani Elina Mgonja akielezea jambo katika mafunzo ya kujengewa uwezo kwa Jukwaa hilo ,Kibaha Mjini yaliyoandaliwa na kampuni ya Ae General Business Co Ltd.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha

KATIBU wa jukwaa la uwezeshaji wanawake mkoani Pwani ,Elina Mgonja ,amewataka wanawake kuthubutu kuanzisha viwanda vidogo vidogo ili kuunga mkono juhudi za Rais Dk John Magufuli ya kufikia uchumi wa kati.

Aidha amewaasa wanawake kuacha kukata tamaa kwani wana nafasi kubwa ya kukuza uchumi na kuleta mapinduzi ya kimaendeleo kupitia shughuli zao za ujasiriamali .

Akizungumza katika mafunzo ya kujengewa uwezo kwa Jukwaa la Uwezeshaji la Wanawake ,Kibaha Mjini yaliyoandaliwa na kampuni ya Ae General Business Co Ltd, alisema mwanamke akijiamini anaweza .

Elina alieleza kuwa changamoto kubwa inayokabili wanawake  wajasiriamali ni ukosefu wa mikopo yenye riba nafuu, elimu ya ujasiriamali kwa ajili ya kutengeneza na kuboresha bidhaa zao .

Alisema licha ya vikwazo hivyo lakini haina budi kukimbilia fursa nyingine zilizopo ikiwemo kuunda vikundi ili kuwezeshwa kirahisi kupitia halmashauri na wadau mbalimbali.

"Wanawake tukiamua tunaweza ,kuna kila sababu kuacha kukatishana tamaa ,kuwekeana majungu hali  inayosababisha kurudisha nyuma wenye nia "

"Nawaomba wenye uwezo wa  kuanzisha viwanda vidogo mthubutu kwani naamini mtaweza ili kuongeza ajira na kuinua uchumi " alisema Elina .

Pamoja na hayo Elina alisema ,suala la wazo nalo ni muhimu katika biashara yoyote , bila kuwa na wazo ni ngumu kuwa na mafanikio hata kama mwanamke atawezeshwa kifedha.

Nae mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzani (UWT) mkoa wa Pwani ,Nancy Mutalemwa ,alielezea wanawake ni sehemu kubwa ya kukuza uchumi wa nchi kutokana na kuwa ni wawajibikaji wakubwa na wamefanikiwa kubuni biashara ambazo zimewainua kiuchumi.

Alisema kuwa kikubwa kinachotakiwa ni wao kuungana na kuanzisha viwanda vidogo kupitia vikundi vyao ambavyo wameviunda.

"Mna nafasi kubwa ya kuinua uchumi wa nchi pia kupitia viwanda vilivyopo hapa Pwani mnaweza kushiriki kukuza uchumi moja kwa moja au kuuza bidhaa ambazo zitatumiwa na viwanda hivyo," alisema Nancy.

Kwa upande wake ,mkurugenzi wa Ae General Business Co Ltd Alexander Malya alieleza ili wanawake wafikie adhma hiyo ya uchumi wa kati wanapaswa kubadilika kwa kuboresha bidhaa zao ili ziwe na ubora na viwango.

Malya alisema ,moja ya mbinu za kuweza kuufikia uchumi wa kati ni wao kufanya kazi kwa bidii na kujituma na kuachana na makundi ambayo hayawezi kuwasaidia.

Post a Comment

0 Comments