Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akipeana mkono na
Balozi wa Jamhuri ya Ireland nchini Paul Sherlock muda mfupi baada ya
maongezi ya mikakati ya kukuza uzalishaji wa zao la Alizeti Mkoani
Rukwa.
Balozi wa Jamhuri ya Ireland Paul Sherlock
amepokea maombi ya ushirikiano baina ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na nchi yake
yaliyolenga kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti mkoani humo jambo
litakalopelekea kuinua kipato cha mkulima wa mkoa wa huo.
Maombi hayo yaliyowasilishwa na mkuu wa mkoa wa
Rukwa Mh. Joachim Wangabo kwa balozi huyo mapema mwezi huu yalionyesha hali
ilivyo ya uzalishaji wa zao hilo kwa sasa, ambapo kati ya hekta za shamba la Alizeti
0.5 hadi 2 huzalisha tani 1.1 badala ya tani 2.5.
“Nimefurahishwa sana na jitihada za Mh. Joachim
Wangabo kwa kuona umuhimu wa kutafuta zao mbadala la biashara katika Mkoa wa Rukwa
ikiwa ni pamoja na kuinua kulimo cha mkoa na kuinua kipato cha wakulima wadogo
na hatimae kuwatafutia namna ya kuongeza viwanda vidogo na kuongeza ajira,”
Alisema Balozi Sherlock.
Kwa upande wake Mh. Wangabo amesema kuwa zao la
mahindi linazalishwa kwa wingi sana katika mkoa wake na wakulima hulichangamkia
hilo zaidi ila bei ikitetereka wakulima hao wanakosa pa kujishika hivyo kwakuwa
zao la alizeti ni la pili la kibiashara basi ni vyema kulitafutia mikakati liwe
sawa na zao la mahindi ili wananchi wachague.
“Kwa mwaka 2016/2017 hekta 47,862 zililimwa alizeti
na tukapata tani 53,470 ambayo ni chini ya kiwango tunachotakiwa kuzalisha
kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa kwa hekta 47,862 zikilimwa vizuri tunaweza
kupata tani 119,655 ambayo ni ongezeko la asilimia 55, tunataka kufika huko, tuzalishe
mafuta ya alizeti kwa wingi, kutengeneza ajira na kuongeza viwanda,” Alisema Mh.
Wangabo.
Ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo kutalipunguzia
taifa mzigo wa kununua mafuta nje ya nchi jambo linalopelekea serikali kutumia
pesa nyingi kufanya manunuzi na hatimae pesa hiyo kubaki kwa wakulima wetu.
Mkoa wa Rukwa unatarajia kushirikiana na
Shirika lisilo la kiserikali la Faida mali ambalo limefanikiwa kwa kiwango
kikubwa kukuza zao la alizeti katika Mkoa wa Singida ili kuhamishia ujuzi huo
katika Mkoa wa Rukwa.
Kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na
uwekezaji, Tanzania hutumia Shilingi bilioni 189.6 kila mwaka kununua mafuta ya
kula nje ya nchi huku ikizalisha tani 91,000 ambayo ni sawa na asilimia 40 za
mafuta hayo tofauti na makadirio ya tani 200,000 hadi 300,000 ya uhitaji wa
bidhaa hiyo kwa mwaka.
No comments:
Post a Comment