WIZARA ya
Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema kuwa katika miaka 60 ya
Uhuru sekta hiyo imekuwa ambapo kwa sasa kuna magazeti na machapisho
yaliyosajiliwa 270, Radio zaidi ya 200, Vituo vya Televisheni 48, Blog 122,
Radio mtandao zaidi ya 20.
Hayo yameelezwa
leo,Novemba 16,2021 jijini Dodoma na Waziri wa Wizara hiyo,Dk.Ashatu Kijaji
wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Sekta ya
Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika kipindi cha miaka 60, ya
uhuru wa Tanganyika.
Waziri Kijaji
amesema miaka 60 baada ya Uhuru Taifa limeshuhudia ukuaji
wa sekta ya Habari ambapo kwa sasa kuna magazeti na machapisho
yaliyosajiliwa 270, radio zaidi ya 200, Vituo vya
televisheni 48, Blog 122, radio mtandao zaidi
ya 20.
Amesema Taifa
limeshuhudia ukuaji na mabadiliko ya teknolojia nchini ambao
umepelekea kuwa na Television Mtandao (online TV) zaidi ya 500 hadi sasa.
“Idadi hii ya vyombo
vya habari inaonesha jinsi gani Taifa letu limepiga hatua kubwa katika
kurahisisha na kuimarisha uhuru wa upatikanaji wa habari kwa wananchi wetu.
“Hivyo basi sote
tutakubaliana kwamba kuna mafanikio mengi yaliyopatikana katika kipindi cha
miaka 60 ya Uhuru yanayogusa Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari hapa nchini, yanayohusisha utoaji wa taarifa mbalimbali za
Serikali za kitaifa na kimataifa, taarifa za uchumi, siasa, michezo na burudani
kwa wananchi kupitia redio, runinga, magazeti na mitandao ya kijamii,”amesema
AVISHUKURU VYOMBO VYA
HABARI
Waziri Kijaji amesema
vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kutoa habari, kuburudisha, na kuelimisha
jamii juu ya matukio na masuala mbalimbali yanayojiri ndani na nje ya Nchi na
kuchangia katika kukuza na kuimarisha demokrasia na utawala bora.
“Wizara ya Habari;
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inatambua mchango wenu katika kuwaelimisha
na kuwafikishia wananchi taarifa zinazohusu masuala mbalimbali ikiwemo Sera,
Mipango na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Hivyo basi napenda
kuwapongeza kwa kazi hii ya kizalendo mnayofanya na ni imani yangu kuwa
mtaendelea kufanya kazi zenu kwa moyo wa uzalendo na kuzingatia weledi katika
kuiletea nchi yetu maendeleo hususani kupitia sekta hii adhimu ya
Habari,”amesema
Amesema Mwaka 1993
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuona umuhimu wa vyombo
vya habari kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, iliamua kufungua
milango na kuruhusu kuanzishwa kwa televisheni, redio na magazeti ya binafsi.
Amesema Kamisheni ya
Utangazaji ilianzishwa Novemba 1993 chini ya Mwenyekiti wake Mark
Bomani na kuanza majukumu ya kupokea maombi na kutoa leseni za redio na
televisheni, kufuatilia na kusimamia urushaji wa matangazo ya redio na
televisheni pamoja na kufuatilia na kutoa masafa kwa vyombo vya utangazaji vya
binafsi.
MKONGO WA TAIFA
Amesema kuwepo kwa
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye uwezo na ubora mkubwa unaoruhusu watoa
huduma wote kuutumia bila upendeleo, kumeleta faida nyingi nchini.
Amezitaja faida hizo
ni pamoja na kushuka kwa gharama za maunganisho ya jumla (interconnection
fee) kwa simu za mkononi kutoka shilingi 115 kwa dakika mwaka 2009 hadi
shilingi 10.4 mwaka 2020.
“Punguzo hili
limewezesha kushuka kwa gharama za watumiaji wa mwisho na hivyo kufanya huduma
za mawasiliano kutumiwa na wananchi wengi,”amesema.
Amesema ukuaji wa
Sekta ya Mawasiliano unaoonekana kwenye ongezeko la matumizi ya simu za
mkononi, intaneti, miamala ya kifedha na ongezeko la mifumo mbali mbali ya
kutolea huduma kwa njia ya mtandao.
“ Mathalani mnamo
tarehe 9 Disemba 1961 wakati wa Uhuru Tanganyika ilikuwa na simu za
mezani 16,238 zilizokuwa kwenye matumizi Tanganyika nzima, nyingi zilikuwa
za taasisi na idara za Serikali,”amesema.
Amesema Hadi Juni
2021, kulikuwa na laini za simu za mkononi 53,111,246 na za mezani
71,405. Watumiaji wa intaneti wamefikia 29,152,713 ambao kabla ya uhuru
hawakuwepo;
MINARA
Amesema hadi sasa
Tanzania kuna jumla ya minara ya mawasiliano 12,902 ambapo minara 2,630 inatoa
huduma ya 2G pekee na minara 9,579 inatoa huduma ya mawasiliano ya 2G, 3G au/na
4G.
Amesema UCSAF imejenga
minara 1,068 kati ya minara tajwa hapo juu kwa kutumia ruzuku ya Serikali kwa
kushirikiana na watoa huduma ambapo hadi sasa takribani shilingi bilioni 161
zimetumika kujenga minara hiyo.
“Hivyo, ujenzi wa
minara ya mawasiliano umefanyika kwenye kata 2,579 za Tanzania Bara kati ya
kata 3,956 ambazo ni sawa na asilimia 65 na kwa upande wa Zanzibar, minara hiyo
imejengwa kwenye kata 101 kati ya kata 110 ambazo ni sawa na asilimia
92.,”amesema.
Amesema Serikali
katika azma yake ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya mawasiliano ya
uhakika na kwa gharama nafuu, Mfuko wa Mawasiliano kwa wote, hivi karibuni
imetangaza zabuni ya shilingi bilioni 37.7 za ujenzi wa minara 224 ya
mawasiliano katika maeneo ya kimkakati na mipakani.
UKUAJI WA POSTA NA MZEE
RAJABU YUSUFU
Aidha,Waziri Kijaji
amesema kabla ya Uhuru na mara baada ya Uhuru huduma za posta
zilikuwa zinatolewa kwa kutumia watu waaminifu waliochaguliwa na jamii
walioitwa mail runners.
Amemtolea mfano Mzee
Rajab Yusufu aliyefanya kazi hiyo kwenye vituo viwili kati ya Nzega na
Itobo halafu Itobo na Bukene vilivyopo mkoa wa Tabora.
“Mzee huyo alifanya
mitihani wakati wa posta ya mkoloni, alifaulu na kuwa Afisa Msaidizi wa Posta,
Tabora Mjini wakati wa mkoloni na baadae alijiendeleza na kuteuliwa kuwa
Mkurugenzi wa Posta Tanzania baada ya nchi kupata Uhuru na baadae kuwa
Mwenyekiti wa Umoja wa Posta Afrika (Pan African Postal
unioni PAPU),”amesema.
Amesema ili
kuhakikisha Wananchi wananufaika na uwekezaji mkubwa ulitokana na mazingira
mazuri ya uwekezaji kwenye eneo la Mawasiliano na Teknolojiaya
Habari, Mwaka 2010, Serikali ilianza kutekeleza Mfumo wa Anwani za
Makazi na Postikodi.
“Mfumo huu unatambulisha
mahali halisi ambapo mtu anaishi, mahali ilipo biashara yake au ofisi
anayofanyia kazi kwa kufuata jina la barabara na mtaa, namba ya nyumba au jengo
pamoja na Postikodi.
“Postikodi au simbo za
posta kama inavyotambulika ni mfumo maalum wa tarakimu unaotambulisha eneo la
kufikisha huduma za posta ambapo kwa nchi ya Tanzania inaanzia katika ngazi ya
kata, wilaya, mkoa na kanda,”amesema.

0 Comments