Balozi wa Pamba Nchini, Aggrey Mwanri akiwapa kiapo wakulima wa zao hilo ili wazingatie kanuni na sheria za kilimo bora cha pamba. ............................................................
Dotto Mwaibale na Philemon Mazalla, Singida
KAMPUNI ya Biosustain Ltd
inayojishughulisha na kilimo cha pamba mkoani Singida imejipanga
kutoa elimu kwa wakulima ili kuliendeleza zao hilo mkoani hapa.
Hayo yamebainishwa na Wakala
wa ununuzi wa pamba wa kiwanda hicho Said Abdallah wakati akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la msimu wa kilimo 2022/2023 wilayani Iramba mkoani
Singida lililofanyika Septemba 28, 2022.
“Kwa msimu huu wa kilimo
kampuni yetu imejipanga kutoa elimu elekezi kwa wakulima ili waweze kulima na
kuvuna kwa tija” alisema Abdallah.
Alisema kampuni hiyo
ina uwezo wa kuchakata pamba tani 50,000 lakini kutokana na kuwa na msimu
mbaya wamechakata tani 20,000 tu na kusababisha kuwa chini ya kiwango.
Alisema elimu hiyo
wataitoa kwa kuzunguka kijiji hadi kijiji wakishirikiana na Balozi wa Pamba Nchini, Aggyey Mwanri ambapo watatoa miundombinu wezeshi ya pikipiki na baiskeli ili
kufanikisha jambo hilo.
Alisema kwa msimu uliopita
walitoa baiskeli 20 na msimu huu wa 2022/2023 watatoa tena
baiskeli zingine 22 kwa wakulima viongozi katika kila kijiji ambacho hakikuweza
kufikiwa msimu uliopita.
Aidha Abdallah alisema
watatoa pikipiki kwa maafisa ugani wa kampuni na pia watatoa mafuta kwa maafisa kilimo wa
Serikali kwa ajili ya vyombo vyao vya
usafiri lengo likiwa kufanikisha kazi hiyo.
“Pamba ni zao lenye tija
wakati wote inyeshe mvua, liwake jua itaota tu hivyo wito wangu kila mkulima na mwananchi mliopo hapa mlime walau kila mmoja ekari moja” alisema Abdallah.
Abdallah aliongeza kuwa
msimu uliopita walivuna tani 700 lakini msimu huu wamevuna tani 861 na kuwa
walisambaza mbegu tani 138 ambayo walitarajia kupata ekari 13,000 na kwa mavuno ya
kiwango cha chini walitarajia kupata kilo milioni 4 lakini kwa bahati mbaya wamepata tani
800.
Katika ufunguzi wa kongamano
hilo Balozi wa Pamba Nchini, Aggrey Mwanri
alitoa mafunzo ya kilimo cha zao hilo kwa wakulima ambapo alitumia nafasi hiyo
kuipongeza kampuni hiyo kwa kuwa kinara wa uzalishaji wenye tija wa zao hilo mkoani
Singida. |
No comments:
Post a Comment