MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Singida (SUWASA) itajenga mabwawa matatu ya kutibu majitaka baada ya serikali kuipatia mamlaka hiyo kiasi cha zaidi ya Sh.bilioni 1.7.
Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA, Sebastian Warioba, alisema hayo leo (13/10/2022) wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mabwawa hayo baina ya SUWASA na mkandarasi M/S Perntels Company and Nangai Engineering and Contractors Co.(T) Ltd na kushudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
Alisema kutokana na ongezeko la watu wanaofikia 193,116 katika Manispaa ya Singida imesababisha ongezeko la uhitaji wa maji linalofikia kiasi cha lita 15,063,048 kwa siku na hivyo kuwepo na ongezeko la uzalishaji wa majitaka ambao umefikia lita 12,803,519 kwa siku.
Alisema SUWASA imeamua kujenga mabwawa hayo hasa kutokana na kwamba yasipodhibitiwa kwa wakati yanaweza kusababisha athari za kiafya na kimazingira kwa wananchi.
Warioba alisema mradi huo utakapokamilika utanufaisha wananchi 259,539 na pia utaboresha usafi wa mazingira na afya kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema SUWASA iweke mpango mkakati wa kuwa na mifumo ya ukusanyaji majitaka katika Manispaa ili kuwa na mji wa kisasa ambao unakidhi mahitaji.
Serukamba aliagiza SUWASA kuongeza wigo wa mtandao wa huduma za maji hasa maeneo ya pembezoni mwa mji na pia wadau wawe wanalipa Ankara za maji kila mwezi ili kuiwezesha SUWASA kumudu gharama za uendeshaji.

0 Comments