Vikundi 13 vikiwemo vya akina mama, vijana
na Watu wenye ulemavu vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi
vimepewa mafunzo ya kuwajengea uwezo juu ya usimamizi wa miradi ikiwa ni hatua
ya kuviandaa kwaajili ya kupewa mikopo isiyo na riba inayotokana na asilimia 10
ya makusanyo ya fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
Akizungumza
wakati wa mafunzo hayo Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya jamii Wilaya ya Bariadi
Bi. Beatrice Gwamagobe amebainisha kuwa katika awamu hii vikundi vipatavyo 13
vinatarajia kupatiwa mikopo isiyo na riba ambapo jumla ya Shilingi Milioni 130
zitatolewa kama mkopo kwa vikundi hivyo.
Aidha
alitoa mchanganuo kuwa Shilingi Milioni 74 zimetokana na asilimia kumi ya
makusanyo ya mapato ya ndani kwa robo ya kwanza 2022/2023, Milioni 44
zimetokana na marejesho ya vikundi vilivyokopeshwa awamu zilizopita na
Shilingi Milioni 12 ni bakaa kutoka Mwaka wa fedha 2021/2022 hivyo jumla
kufanya kiasi cha Shilingi milioni 130.
“Leo
tulikuwa na mafunzo kwa vikundi kumi na tatu ambavyo vinakwenda kupewa mikopo,
vikundi kumi ni vya wanawake, viwili vya vijana na kimoja cha watu wenye
ulemavu, vikundi hivi vinajishughulisha na shughuli mbalimbali za ujasiriamali
kama vile Kilimo, Ufugaji, Biashara na shughuli nyinginezo zinazoingiza kipato”
alifafanua Bi. Beatrice
Naye
Bi. Sophia Charles mmoja miongoni mwa wanakikundi kiitacho “Wanawake
wapiganaji” kutoka kijiji cha Mbugani kata ya Banemhi amebainisha kuwa mafunzo
waliyopewa yamewasaidia kuwaongezea uelewa juu ya namna ya kuendesha miradi yao
ili iweze kuwapa faida ambayo pia itawasaidia kufanya marejesho ya mkopo wao
kwa wakati.
Sambamba na vikundi hivyo kupewa mafunzo Afisa Sheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Bw. Raymond Cosmas aliviongoza vikundi hivyo katika utiaji wa saini wa mikataba ya mikopo hiyo na kuhakikisha vipengele vyote vimeeleweka na vimeridhiwa.

0 Comments