Na Dotto Mwaibale, Singida
UTULIVU amani na siasa safi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan umeongeza uwekezaji hapa nchini kutoka wawekezaji 20 waliokuwa
wakisajiliwa kwa mwezi hadi kufikia 80.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Dk.
Binilith Mahenge wakati akizungumza
baada ya kutembelea kiwanda cha kusindika mafuta cha Wild Flower,Grains and Oil
Mill Project kilichopo nje kidogo ya Manispaa ya Singida wakati wa ziara yake
ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani aliyoifanya Oktoba 26,2023.
" Utulivu, amani na siasa safi inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan
imekuwa kivutio kikubwa cha wawekezaji kuja nchini kuwekeza na ni jambo la
kujivunia," alisema Dk.Mahenge.
Alisema kutokana na hali hiyo idadi ya wawekezaji wanaosajiliwa TIC inaendelea
kuongezeka kila siku baada kuanza kutekelezwa kwa sheria mpya ya uwekezaji ya
mwaka 2022 ambayo imepunguza thamani ya mtaji unaohitajika kwa mwekezaji wa
ndani kutoka Dola za Kimarekani 100,000 hadi 50,000 kwa ajili ya kuwavutia
wawekezaji wa ndani.
Alisema sheria hiyo namba 10 ya 2022 inatambua wawekezaji mahiri nakupewa
vivutio vya uwekezaji na kuwa wale wenye sifa wanapewa misamaha ya kodi
kwa kuwa ndani ya kipengele hicho cha
umahiri.
Alisema hivi sasa suala zima la uwekezaji limebadilika kwa kasi kubwa na
Rais Samia Suluhu Hassan kuonekana ni namba moja kutokana na nchi kuwa na
sheria hiyo ambayo inawavutia wawakezaji wengi.
Dk. Mahenge alitumia nafasi hiyo kuwahamasisha watanzania wenye mitaji mikubwa kwenda TIC
kujisajili ili waweze kutambulika jambo litakalo ongeza idadi ya wawekezaji
hapa nchini.
Mkurugenzi wa kiwanda cha Wild
Flower,Grains and Oil Mill Project, Khalid Omary, alisema kiwanda hicho
kitakapo kamilika ujenzi wake kitatoa ajira za kudumu na za muda mfupi kwa
wananchi kati ya 400 hadi 1,000 na kuwa uwekezaji wake ni zaidi ya Sh.bilioni
56.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiwanda cha kusindika mafuta ya Alizeti cha Mount Meru Miller's Sree Valsan Nair alisema baada ya kutambuliwa
kuwa muwekezaji mahiri mwaka 2013 alipata msamaha wa kodi kwa kuondolewa VAT
kwa mafuta anayouza lakini aliendelea kulipa kodi na sasa anaomba alipwe
Sh.Bilioni 12 ambazo alikuwa akizilipa licha ya kutambuliwa kuwa ni mwekezaji
mahiri.
Nair alisema wamefungua kiwanda cha kutengeneza sabuni kutokana na mabaki
ya malighafi zingine zinazopatikana baada ya kukamuliwa kwa mbegu za alizeti na
kuongeza ajira kwa wananchi hatua ambayo imepongezwa na Mwenyekiti wa TIC Dk.
Mahenge.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha
Kuchambulia Pamba cha Biosustain (T) Limited kilichopo mjini Singida, Sajiad
Haider alisema changamoto kubwa walionayo ni umeme ambao unakatwa kwa zaidi ya
saa nane na Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) jambo ambalo limepunguza uzalishaji.
Changamoto ya pili aliyoitoa ni kuhusu eneo lao lenye mgogoro ambapo ameomba
vyombo vinavyoshughulikia suala hilo kulimaliza ili waweze kuliendeleza na
kupata sehemu ya kuhifadhi pamba yao.
Mwenyekiti wa Bodi ya TIC Dk. Binilith Mahenge katika ziara hiyo aliongoza
na mjumbe wa bodi hiyo Mhandisi Peter Chisawillo, Meneja wa TIC Kanda ya Kati
Venance Mashiba, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Lucas Mkuki na Afisa Uwekezaji
Masungu Mdanya kutoka TIC Kanda ya Kati.
Viwanda vilivyotembelewa na Dk.Mahenge ni kiwanda cha kusindika mafuta cha Wild Flower,Grains and Oil Mill Project, Kiwanda cha Kuchambulia Pamba cha Biosustain (T) Limited na Kiwanda cha kusindika mafuta ya Alizeti cha Mount Meru Miller's ambapo kesho atahitimisha ziara yake kwa kuzungumza na Serikali ya Mkoa wa Singida, kutembelea mgodi wa Dhahabu wa Shanta uliopo Wilaya ya Ikungi na kukutana na wawekezaji waliopo mkoani hapa.
No comments:
Post a Comment