-----------------------------------------------
Imeandaliwa na mtandao wa singidaniblog
BONANZA la Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida 2024 kuelekea Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja limefanyika Uwanja wa Bombadia mjini hapa huku likihamasisha huduma bora na wateja wakitakiwa kuendelea kutumia nishati ya umeme na kuwa tayari kuilipia ili nao waendelee kuhudumiwa.
Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Shirika hilo Kanda ya Kati ambaye alikuwa mgeni rasmi Mhandisi Danstan Ndamugoba wakati akifungua Bonanza hilo ambalo lilihusisha michezo ya aina mbalimbali na kuwashirikisha wafanyakazi wa shirika hilo kutoka wilaya zote za Tanesco.
Ndamugoba alisema lengo la bonanza hilo ni kuongeza ushirikiano na umoja kwa wafanyakazi, kujuliana hali na kujenga afya zao na kuwa ili waweze kutoa huduma kwa wateja wao wanatakiwa kuwa na afya njema ambayo inapatikana kwa kufanya michezo.
“Tumekutana leo hapa kwenye bonanza hili na lengo lingine tukielekea kwenye wiki la huduma kwa wateja ambayo itaanza Oktoba 7, 2024 hadi Oktoba 14, 2024 sisi kama wafanyakazi wa Tanesco Mkoa wa Singida tukiwa sehemu ya wafanyakazi wa Kanda ya Kati tumeona tujumuike ili tutengeneze na kuimarisha afya zetu huku tukipendana na wiki ijayo tukaoneshe huduma bora tunazozizotoa kwa wateja wetu,” alisema Ndamugoba.
Alisema michezo hiyo haifanyiki kwa ajili ya wiki ya huduma kwa wateja tu bali ni endelevu na kuwa itakuwa ikiendelea kufanyika kwa dhima ya kuimarisha afya za wafanyakazi katika mikoa inayounda Tanesco Kanda ya Kati ambayo ni Morogoro, Dodoma na Singida.
Kwa upande wake Meneja wa Tanesco Mkoa wa Singida, Mhandisi Mwamvita Ally alisema katika bonanza hilo wamekutana wafanyakazi wa shirika hilo kutoka wilaya zote sita za Tanesco Mkoa wa Singida kwa ajili ya kujumuika pamoja kujuliana hali sanjari na kuimarisha afya zao kupitia michezo.
Mfanyakazi wa shirika hilo kutoka Manispaa ya Singida Ibrahim Solo alisema bonanza hilo ambalo limekuwa likifanyika kila mwaka limekuwa likiwaongezea ari na mori wa kufanya kazi na kubadilishana mawazo na wafanyakazi wenzao kutoka wilaya zingine ambapo alitumia nafasi hiyo kupongeza utaratibu huo.
Naye Grace Ngoi kutoka Manyoni alisema michezo hiyo wanayoifanya kupitia bonanza hilo imekuwa ikiwajenga kiakili na kimwili na kuwaongezea nguvu ya kufanya kazi pamoja na kuimarisha afya zao.
Katika bonaza hilo michezo ya aina mbalimbali ilifanyika kama ya kutembea na yai huku likiwa limewekwa kwenye kijiko ambapo mshindi aliyeibuka kidedea kwa upande wa wanaume alikuwa ni Bakari Athuman kutoka Wilaya ya Ikungi na kwa wanawake akiwa ni Sara Shalua kutoka Singida Mjini.
Katika shindano la kukimbiza kuku kwa upande wa wanaume mshindi alikuwa ni Issa Iddi kutoka Itigi na kwa upande wa wanawake akiwa Grace Ngoi kutoka Manyoni ambao waliondoka na kitoweo hicho.
Shindano lingine lililofanyika lilikuwa ni la kula tunda aina ya Aple ambapo kwa upande wa wanawake mshindi alikuwa ni Magreth Mtae kutoka Itigi na kwa wanaume alikuwa Salim Mbeto kutoka Manispaa ya Singida.
Mchezo wa kukimbia kwenye gunia mshindi kwa upande wa wanaume alikuwa Recardo Fifi kutoka Ikungi na kwa upande wa wanawake akiwa Anna Juma kutoka Manispaa ya Singida huku mshindi wa kula mkate kwa kinywaji aina ya Pepsi akiwa ni Hamisi Mrisho kutoka Manispaa ya Singida.
Katika mchezo wa kuvuta kamba mshindi ilikuwa ni timu ya Kombaini dhidhi ya timu ya Tanesco Ofisi ya Mkoa wa Singida huku shindano la kuvaa soksi bila ya kuinama mshindi akiwa ni Mhandisi Boniface Shitindi.
Michezo mingine iliyofanywa katika bonanza hilo ni mpira wa miguu baina ya timu ya Muungano wa Timu za Wilaya dhidi ya Singida Manispaa ambapo timu ya Muungano wa wilaya iliibuka kwa ushindi wa mabao 2-1, wakati mchezo wa Netball ushindi ukienda kwa timu ya Twiga kwa mabao 5-4 dhidi ya Timu ya Tausi.
0 Comments