Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Mtae kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Shafii Makamba (kulia) akitoa maelezo kwa Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Bohari ya Dawa (MSD) ambaye pia ni Mlezi wa MSD Kanda ya Tanga, Dkt. Rukia Mwifunyi jinsi vifaa mbalimbali vilivyopelekwa kituoni hapo na MSD kupitia Serikali jinsi vinavyofanya kazi.
.............................
Na Dottoo Mwaibale, Lushoto
Mjumbe wa
Bodi ya Wadhamini ya Bohari ya Dawa (MSD) ambaye pia ni Mlezi wa MSD Kanda ya Tanga, Dkt. Rukia Mwifunyi amewaomba wateja wa MSD kueleza changamoto zao mbalimbali wanazokumbana nazo
wakati wanapohudumiwa na MSD ili ziweze kuboresha huduma.
Dkt. Mwifunyi ameyasema hayo katika ziara yake
ya kikazi mkoani Tanga alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti na baadhi ya
viongozi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na Watumishi wa Kituo
cha Afya cha Mtae ambacho kimepanda hadhi kutoa Zahanati baada ya kufanyiwa
maboresho na kuanza kutoa huduma ya upasuaji.
“Tunawaomba muwe munatuambia changamoto
mulizonazo wakati tukiwahudumia ili tuweze kuzifanyia kazi na wananchi
waendelee kupata huduma bora kwani Serikali imekwisha jenga miundombinu pamoja
na kuwezesha kupata bidhaa za afya,” alisema Mwifunyi,
Alisema katika ziara hiyo ameweza kuona matumizi
ya mabilioni ya fedha yaliyotolewa na Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan jinsi yalivyofanya kazi kubwa kwa kujenga Kituo cha Afya cha kisasa Kata
ya Mtae na kupeleka bidhaa za afya kupitia MSD zenye ubora wa hali ya juu.
Aidha, Dkt. Mwifunyi aliipongeza Halmashauri ya
Wilaya ya Lushoto kwa kuwa kinara katika kulipa madeni ya fedha yanayotokana na
bidhaa za afya wanazohudumiwa na MSD.
“MSD haiwezi kujiendesha bila ya kuwa na fedha mnapolipia
madeni yenu kwa wakati yanaisaidia MSD iweze kufanya kazi vizuri ya kupata
bidhaa za afya ambazo zinapelekwa sehemu mbalimbali hapa nchini kutoa huduma
kwa wananchi,” alisema.
Kaimu Mganga wa Hospitali ya Wilaya ya Lushoto Mohamed
Almas, alipongeza MSD kwa kufanya mabadiliko makubwa ya usambazi wa bidhaa za
afya na dawa ambapo alisema zamani bidhaa hizo zilikuwa zikiwafikia walengwa
baada ya miezi miwili lakini hivi sasa ndani ya siku tatu au nne wanakuwa
wamezipata.
“Zamani bidhaa hizo zilikuwa zikipitia
Halmashauri za Wilaya na wao ndio walikuwa wakizipeleka kwenye vituo vya afya
kupitia madaktari wa vituo vya afya, zahanati na hospitali hali ilikuwa sio
nzuri hasa pale usafiri wa kuzipeleka ulipokosekana,” alisema.
Almas aliongeza kuwa utaratibu wa kutumia
kompyuta na kuachana na matumizi ya karatasi umeleta maboresho makubwa ya
upatikanaji wa bidhaa hizo za afya.
Kwa upande wake Mfamasia wa Halmashauri ya
Wilaya ya Lushoto, Rashida Ismail alisema maboresho ya usambazaji wa bidhaa za
afya na dawa yanayoendelea kufanywa na MSD yamekuwa na tija kubwa kwani wakiaIuza
vifaa hivyo wamekuwa wakivipata kwa wakati.
Alisema mbali ya kuvipata kwa wakati mawasiliano
baina ya MSD na wateja wao ni mazuri ambapo ameeleza muda wote wanapowapigia
simu kwa ajili ya kupata mahitaji hayo wamekuwa wakipatikana wakati wote.
ziara hiyo ya Mjumbe wa Bodi ya
Wadhamini ya MSD Dkt. Mwifunyi aliyoifanya na kufikia tamati
Septemba 4, 2024 ilikuwa na lengo la kuzungumza na wateja wanaohudumiwa na MSD ili kupata maoni
yao nini kifanyike ili kuendelea kuboresha huduma zinazotolewa na MSD na
kupokea changamoto zao ili ziweze kufanyiwa kazi.
Aidha, ziara imekuwa ni sehemu ya ya kuadhimisha miaka 30 ya ufanyaji kazi wa MSD tangu ilipoundwa.
Muonekano wa jengo la Utawala la Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto/
Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Bohari ya Dawa (MSD) ambaye pia ni Mlezi wa MSD Kanda ya Tanga, Dkt. Rukia Mwifunyi (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa ziara hiyo. Kutoka kulia ni Mfamasia wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, RashidaIsmail, Mhasibu wa MSD Kanda ya Tanga, Grant Mwapele, Meneja wa MSD Kanda ya Tanga, Sitti Abrahman, Afisa Huduma kwa Wateja MSD Kanda ya Tanga, Mary Isangu, Kaimu Afisa Huduma kwa Wateja MSD, Dkt. Pamella Sawa na Afisa Huduma kwa Wateja MSD, Gendi Machumani.
Kikao na Watumishi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Mtae kikiendelea. Kutoka kulia ni Mganga Mkuu wa kituo hicho, Azizi Nanjasye, Muuguzi na Matroni wa kituo hicho, Josephine Nkya, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Shafii Makamba, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Bohari ya Dawa (MSD) ambaye pia ni Mlezi wa MSD Kanda ya Tanga, Dkt. Rukia Mwifunyi na Meneja wa MSD Kanda ya Tanga, Sitti Abrahman.
Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Bohari ya Dawa (MSD) ambaye pia ni Mlezi wa MSD Kanda ya Tanga, Dkt. Rukia Mwifunyi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Mtae na MSD baada ya ziara hiyo.
0 Comments