Bohari ya Dawa (MSD) imepongezwa kwa kuimarisha mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya mkoani Kagera, ambao umepunguza malalamiko ya upungufu wa bidhaa za afya mkoani humo.
Pongezi hizo zimetolewa hapo jana tarehe 6/1/2025 na Katibu Tawala wa Mkoa
huo Stephen Ndaki, wakati akizungumza na ujumbe maalum kutoka MSD uliomtembelea
ofisini kwake, ukiongozwa na Mwenyekiti
wa Bodi ya Wadhamini ya MSD Bi. Rosemary Silaa, ikiwa ni ziara maalum ya
kuadhimisha miaka 30 ya MSD.
Ndaki amebainisha kuwa maboresho ya huduma za MSD yamesaidia kuondoa kero
na malalamiko ya mara kwa mara yaliyokuwepo miongoni mwa jamii na wateja juu ya
uhaba wa Dawa vituoni, hivyo kupelekea kuimarika kwa hali utoaji wa huduma za
afya Mkoani humo.
Ameongeza kwamba, mbali na kuimarika kwa utoaji huduma, hivi sasa uelewa wa
majukumu ya MSD na jinsi inavyofanya kazi zake, umeongezeka miongoni mwa
viongozi hivyo kuondoa kasumba ya kutupiana lawama juu ya ununuzi ya bidhaa za
afya, baina ya MSD na Wateja wake, kwani viongozi wote ndani ya Mkoa huo
wamejengewa uelewa.
"Hapo mwanzo kulikuwa na kelele sana kutoka vituoni kwamba tumelipa
lakini MSD hajaleta, hatahivyo kwa siku za hivi karibuni malalamiko hayo
yemeondoka, na uelewa juu ya mnyororo wa bidhaa za afya umeongezeka mpaka kwa
viongozi, hivyo tuwapongeze kwa maboresho" Alisema Ndaki.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD, Bi. Rosemary Silaa,
ameeleza namna MSD ilivyopitia katika vipindi tofauti, na jinsi ilivyojizatiti
kuboresha huduma zake, ili kupunguza, ama kuondoa kabisa changamoto chache
zilizoukabili mnyororo wa bidhaa za afya.
Ameongeza kwamba MSD imeendelea kuboresha mikataba yake na wazalishaji na
washitiri, kuajiri kada mbalimbali Ili kukidhi mahitaji ya huduma za MSD kwa
wateja, kuboresha na kuimarisha mifumo ya kiutendaji, kuboresha huduma na
mawasiliano na wateja wake, Ili kuhakikisha inatatua changamoto chache
zilizobakia katika upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.
"Katika kipindi cha Miaka 30 ya utendaji wa MSD, hali ya utoaji huduma
na upatikanaji wa bidhaa za afya nchini imeendelea kuimarika kwa kiasi kikubwa,
huku out of stock zikiendelea kupungua, hivyo tunajivunia kutimiza miaka 30, na
tunaahidi kuendelea kutafuta suluhu ya changamoto zilizobaki kwenye mnyororo
huu wa bidhaa za afya nchini". Alisema Silaa.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Dkt.Samuel Laizer ameipongeza
MSD kwa kutimiza miaka 30, huku akisema takwimu zinaonyesha mabadiliko makubwa
kwenye upatikanaji wa bidhaa za afya na huduma za MSD, ukilinganisha na miaka
kadhaa iliyopita.
Ujumbe wa MSD ukiongozwa na Silaa, uko ziarani kutembelea wateja katika
mikoa ya Kagera na Geita inayohudumiwa na Kanda ya MSD Kagera, kwa lengo la
kupokea mrejesho wa huduma za MSD, ikiwa ni maadhimisho ya Miaka 30, toka ianze
kazi zake.
0 Comments