SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Stars of Poverty Rescue Foundation (SPRF) lenye makao makuu yake Mkoa wa Singida linajivunia mafanikio ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake huku likijipambanua kwa kuendelea kuwa na mipango kabambe kuanzia mwaka huu wa 2025 hadi ifikapo 2030.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi kiaratu akizungumza Disemba 31, 2024 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 10 tangu shirika hilo lianzishwe aliwapongeza watendaji wa SPRFkwa kutimiza miaka hiyo chini ya maono ya kuwa kitovu cha ubora katika kutokomeza umaskini kwa Afya na ustawi.
“Mimi sikuifahamu vizuri SPRF, lakini nimeelezwa, nimejifunza, nimeelewa na ninafahamu kwamba, SPRF imejielekeza katika kutokomeza umaskini kwa njia mbalimbali kama kutoa elimu za stadi za maisha, ujuzi na biashara kwa makundi ya kijamii, kutoa huduma za afya, ikiwemo huduma za afya ya uzazi na magonjwa ya wanawake, uhamasishaji wa matumizi ya maji safi na salama na utunzaji wa mazingira,” alisema Kiaratu.
Kiaratu alitaja kazi nyingine zinazofanywa na shirika hilo kuwa ni kuanzisha vituo vya afya na programu za elimu ya afya katika kusaidia watu na vikundi vilivyo katika mazingira hatarishi, kutekeleza kanuni za utawala bora kwa kupinga ukatili wa kijinsia kwa vitendo, kuweka misingi ya ukuzaji wa ujuzi na ubunifu kwa wafanyakazi wake, washirika na wanufaika inaowahudumia na kufanya mafunzo, ufuatiliaji, tathmini ya program zake na utafiti kwa takwimu zao za mafanikio.
Kiaratu alisema kupitia mawasilisho mbalimbali amejifunza jinsi SPRF inavyoweza kuchangia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2025.
“ Wote tunatambua kwamba madhumuni ya Dira ya Taifa ya maendeleo ya 2025 ni kufikia maisha ya hali ya juu kwa watu wake kupitia utawala bora utawala wa sheria na kuendeleza uchumi imara na shindani na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anaitekeleza azima hiyo kwa vitendo,” alisema Kiaratu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Kiaratu alisema pamoja na SPRF kutekeleza MKUKUTA katika kuisaidia Serikali kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2025, pia inatekeleza malengo matatu makuu ya maendeleo Endelevu ya Dunia kwa vitendo.
Aliyataja malengo hayo kuwa ni lengo la kwanza la Dunia la Maendeleo Endelevu (SDGs) linalosema NO POVERTY (yaani kusiwepo umaskini) akitolea mfano SPRF inavyotafuta fedha kujenga mradi wa soko eneo la Kideka katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, kusadia wanawake 100 kiuchumi katika kupunguza umaskini wa kaya. Pia Mkurugenzi wake anakusudia kujenga ofisi za asasi ya SPRF Mkoa wa Singida.
Alitaja lengo la tatu la Dunia la Maendeleo Endelevu linahusu AFYA na Ustawi wa jamii [yaani Good Health & well Being] ambapo SPRF inatoa huduma za afya kwa wananchi wa Singida. Kwa mwaka 2025 inakusudia kupanua wigo wa huduma kwa kuanzisha kliniki ya uzazi na chanjo (PRIDE RCH) hapa mjini Singida, ambapo pia wameombwa na Manispaa kusaidia kazi hiyo.
Alitaja lengo la tano la Dunia la Maendeleo Endelevu ni kuleta usawa wa Kijinsia [Gender equality] kwa kupinga ukatili dhidi wanawake na watoto zikiwemo aina zingine zote za ukatili; ambapo tumeona, SPRF inatekeleza Mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA) katika hali na sura zote kwa vitendo ikishirikiana na washirika wengine.
“ Kuna mashirika mengi yanayopinga ukatili na ninaamini kwamba nguvu ya pamoja ni muhimu zaidi mkishirikiana katika kutekeleza kazi hii muhimu kwa jamii,” alisema.
Kiaratu alisifia mpangilio wa kazi na ustadi wa mawasiliano kwenye ngazi za Mkoa, Halmashauri na Mamlaka ya Serikali za Mitaa na vijiji vikihusika katika kumwezesha mwananchi kupinga ukatili na kuleta maendeleo kupitia mradi wa AWARE uliotekelezwa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
“ Naipongeza SPRF kwa kuendelea kuwepo Singida na kutekeleza miradi ya kijamii kwa miaka 10 iliyopita. Siyo kazi rahisi kufanya kazi za kujamii bila kuwa na msaada wa kifedha.
Nawapongeza tena SPRF kwa kutembelea wagonjwa hospitali ya Manispaa na kutoa misaada kwa wahitaji na hasa akina mama waliojifungua wakiwemo; Kama vile haitoshi mlitembelea pia wafungwa na mahabusu katika Gereaza la Singida mjini na kutoa misaada ya kiutu katika kufanya maadhimisho ya kutimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwa shirika lenu la SPRF,” alisema Kiaratu.
Kiaratu katika hafla hiyo alizindua kitabu cha Usimamizi wa Biashara na Ujasiriamali kilichoandikwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Dr.Suleiman Charles Muttani na kueleza kuwa anaamini kitabu hicho kitakuwa chachu ya mafunzo kwa mradi wa Wanawake 100 ambao umeasisiwa na SPRF kwa nia njema ya kuwatoa wanawake juani na kuwaweka kivulini kwa kujenga soko eneo la Kideka kwa msaada wa wananchi na wadau wengine.
Katika hatua nyingine Kiaratu aliendesha harambee ya uchangishaji fedha kwa miradi ya Kideka wenye thamani ya Sh.8,733,750/=) na mradi wa Wanawake 100 wenye thamani ya Sh. 6,560,200.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya SPRF, Bi. Redempter Rweyemamu alisema
lengo kuu la taasisi hiyo ni
kusaidia Serikali katika kutekeleza MKUKUTA na DIRA ya Taifa ya Maendeleoya
2025 yakiwemo maendeleo endelevu ya Dunia SDGs ifikapo 2030 mikakati
ambayo haijaeleweka sana ngazi za jamii.
Rweyemamu
alitaja malengo makuu ya Asasi ya SPRF ni Kutengeneza mazingira wezeshi
katika kuchukua hatua za punguza umaskini wa kipato hasakwa kuimarisha
uchumi wa kaya, kuweka mifumo yenye kusaidia watu, makundi athirika na
jamii katika kuondokana na umaskini kwa kuanzisha programu za elimu na afya ili
kusaidia mtu mmoja mmoja na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi na
magumu.
Alitaja lengo
lingine kwa upande wa afya kuwa, SPRF inatoa huduma za Afya kwa magonjwa ya
wanawake, afya ya uzazi, mama na mtoto; sambamba na hayo SPRF inahamasisha
usawa wa kijinsia, haki za Wanawake na watoto.
SPRF pia inahamasisha ushirika na taasisi za kitaifa na kimataifa kwenye
juhudi za pamoja katika kuchukua hatuaendelevu za kuondoa umaskini nchini
Tanzania na kwingineko.
Akielezea dhana
ya shirika hilo; alisema ni kuwezesha, kukuza na kuhifadhi utu, haki za
binadamuna utawala bora ili kuondoa umaskini na kuleta maendeleo ya kaya na kwamba
kama nchi hatutaweza kuzungumza uchumi wa nchi bila kuimarisha uchumi wa kaya
ama kuacha mila na desturi zilizopitwa na wakati zikitamalaki.
Mwenyekiti huyo
wa bodi ya wakurugenzi akizungumzia mradi wa AWARE alisema halijawahi
kuwa jambo rahisi kwa watu wenye mitazamo na mapokeo tofauti kuacha mila zao na
kuwafanya watu hao wenyewe wapinge mila zao wenyewe ambazo kwa kiasi Fulani
zinazorotesha maendeleo.
“Tulishuhudia
SPRF ikiwashirikisha watu mahala pamoja na kuwafanya kuzungumza lugha yao na
hatimaye wenyewe kuwa kipaza sauti dhidi ya mila potofu ya Ukeketaji ndoa na
mimba za umri mdogo, ukatiliwa kijinsia kwa wanawake na watoto. Kazi ambayo ni
kati ya sababu ya kukutana leo tukiadhimisha miaka kumi,” alisema Rweyemamu.
Rweyemamu
akizungumzia miaka 10 ya shirika hilo alisema imejengwa katika kujitoa kwa nia
thabiti kuitumikia Jamii, kwa moyo na kwa nguvu zao zote na kuwa anatambua hamu
kubwa ya wadau katika kusaidia kutokomeza umaskini wa kipato na kuwa na jamii
inayotambua kazi kama kipimo cha utu.
Halikadharika
alisema anatambua kwamba Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 inaisha na tutaanza
Dira ya Taifa ya 2050 na baada ya kuwa tutaendelea na malengo ya dunia ifikapo (SDGs)
2030.
Alisema anaiona
SPRF kama mfano halisi wa asasi za kiraia; ikilenga kuendeleza juhudi halisi
katika kwenda na Dira mpya ya maendeleo ya nchi ya 2050 na agenda ya Afrika
2063 ambapo asasi zote zinapashwa kwenda kwenye uelekeo huo kwa ajili ya
kujenga asasi imara na watu makini.
Naye Mkurugenzi
wa SPRF Dr. Suleiman Muttani akizungumzia kazi za shirika hilo alisema ni
kutoa elimu ya stadi za maisha, ukuzaji ujuzi na ubunifu katika kupunguza
umaskini na linatoa huduma za elimu ya afya kwa jamii.
Alitaja kazi
nyingine ni kuhamasisha usawa wa kijinsia na kupinga ukatili wa aina zote,
kujenga uwezo wa kitaasisi kwa kushirikiana na wadau wake kokote duniani na
kuiwezesha jamii kutokomeza umaskini kwa na ustawi kwa wote.
Dr. Muttani
aliongeza kuwa SPRF kama mojawapo ya Asasi za Kiraia (AZAKI) ni taasisi kamili
yenye jukumu la kufanya kitu fulani katika kuimarisha ama kuboresha maisha ya
watu mahali iliko. Kwamba kuwa kazi kuu ya azaki yoyote duniani ni
kulinda ubinadamu na ustawi wa watu Mahali lilipo kwa kujielekeza kwenye kusudio
Maalum ya kazi zake.
Aidha, Dr.
Muttani alisema matarajio ya shirika hilo kwa mwaka 2025-2030 ni kuendelea
kuchukua hatua za kupunguza umaskini wa kaya, kuendeleza program za
elimu na afya katika kusaidia makundi athirika kwenye Jamii, kuendeleza
ushirikiano na wanajamii, taasisi za kitaifa na kimataifa katika kutafuta
fedha za kujenga miundombinu za ujasiria mali Singida,kuendelea na kujenga
uwezo wa kitaasisi katika kukua na kuwa azaki endelevu.
Alitaja kazi
zinazotarajiwa kufanywa na shirika hilo kuwa ni kufundisha ujasiriamali
kwa wanawake 100 wanaojitambua ifikapo Disemba 2027, kujenga soko
dogo kwa ajili wa wanawake wanaofanya biashara eneo la Kideka ili kuwapunguzia
kuungua na jua katika hatua za kupunguza umaskini wa kaya kwa uchangishaji wa
fedha kutoka jumuia za ndani kwa ajili ya kupata fedha za ujenzi wa mradi huo wenye
thamani ya Sh. 8,733,750 watatumia fomu maalum kwa ajili ya kuzipata hadi
ifikapo ifikapo Disemba 2027 ama kabla.
Alitaja kazi
nyingine kuwa watapanua wigo wa huduma za afya kwa kuanzisha kliniki kwa
wajawazito na chanjo katika ofisi za sasa za PRIDE polyclinic ili
kuwahudumia wajawazito na watoto kwa ufanisi zaidi kuanzia mwezi Machi, 2025.
Kazi nyingine
wanayotarajia kuifanya ni kuanzisha ujenzi wa ofisi ya shirika hilo mkoani
Singida kabla ya Disemba 2030, kutafuta fedha kwa ajili ya mradi wa AWARE hatua
ya II kutoka kwa wadau wengine ili kutekeleza dhana ya utawala bora na kupinga
ukatili wa aina zote, kuhamasisha uwepo wa usalama wa chakula kwa kuzingatia utunzaji
wa mazingira na kupunguza athari zitokanavyo na Mabadiliko ya tabia nchi.
Alitaja baadhi
ya changamoto ni ukosefu wa fedha za kuendeshea miradi ya kijamii, kwa kuishiwa
mbinu ama uwezo wa utafutaji fedha kama utegemezi kutoka mataifa ya kigeni, ukosefu
wa watumishi walio tayari kutekeleza kazi za jamii kwa malengo tuliojikwekea,
mawasiliano dhafifu na jamii hasa jamii kutokujua kazi zinazofanywa na asasi za
kiraia kama SPRF.
Dr. Muttani alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa SPRF itaendelea kujitanabaisha na Jamii wanayoihudumia kama nyenzo ya kufahamika na iwe tayari kuchangia miradi ya kijamii.
0 Comments