SERIKALI inatarajia kujenga vyuo 65 katika
mikoa mbalimbali ikiwa na lengo la kuongeza nafasi kwa wanafunzi pamoja na
kuongeza udahili wa wanafunzi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Ustadi ( VETA ) CPA Anthony Kasore ameyasema hayo katika Ufunguzi wa Maadhimisho ya miaka 30 ya VETA pamoja na miaka 50 ya utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kupitia taasisi mbalimbali za serikali nchini yaliyofanyika Mkoa wa Singida Februari 21, 2025.
Kasore alisema kuwa ongezeko hilo la vyuo 65 litaleta manufaa kwani watanzania watakaosoma katika vyuo hivyo watapata ajira.
Alisema kwa sasa kuna vyuo 80 ambapo vinadahili wanafunzi 83,974 kwa mwaka tofauti na ilipoanzishwa ilikuwa na vyuo 14 ambavyo vilikuwa vinadahili wanafunzi 1940.
"Vyuo 65 vinaendelea kujengwa kwenye wilaya mbalimbali nchini ambavyo vinatarajia kuongeza udahili kwa zaidi ya wanafunzi 80,000,"alisema Kasore.
Akizungumzia mafanikio
ya sekta ya mafunzo chini ya VETA CPA Kasore alisema zimeongezeka
kutoka 10 mwaka 1995 hadi 13 mwaka 2025 ikihusisha fani 89 zinazokidhi
mahitaji ya soko la ajira.
Akizungumzia kuhusu ushirikiano na viwanda katika utoaji wa mafunzo alisema wamepanga kupanua wigo zaidi wa mafunzo kwa mfumo wa uanagenzi kwa kushirikiana na sehemu za kazi.
“ Tunafanya hivyo kwa kutambua kuwa sehemu za kazi ambako ndiko ni kwenye makampuni na viwanda ndiko kwenye teknolojia nyingi za za kisasa na ndiko ambako mazoezi ya uhalisia yanafanyika,” alisema Kasore.
Alisema VETA ilianzishwa mwaka 1995 ikiwa na lengo la kuwapatia mafunzo mbalimbali wananchi wa Tanzania ili waweze kujiajiri na kuanzishwa kwake kumeleta tija kubwa kwa watanzania.
Katika maadhimisho hayo mkurugenzi huyo na timu yake walitembelea eneo inapojengwa ofisi na Halmashauri ya Manispaa ya Singida na kuona jinsi wanafunzi wa VETA Mkoa wa Singida walivyopata fursa ya kushiriki ujenzi wa ofisi hiyo.







0 Comments