Na Happiness Shayo- Wanging’ombe
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb)
amefungua rasmi semina ya kuwajengea uwezo wadau wa uhifadhi kuhusu mikakati ya
kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu ikiwa ni pamoja
na uanzishaji na usimamizi wa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (Wildlife
Management Areas -WMAs) iliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya
Wanging’ombe Mkoani Njombe.
Akizungumza katika semina hiyo leo Aprili 14,2025 katika
ukumbi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe amesema
semina hiyo ni mojawapo ya mikakati ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya kuunga
mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika kuendeleza utalii kupitia uhifadhi.
“Serikali inaendelea kutekeleza dhana ya ushirikishaji wa jamii
katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake nchini kwa kuhamasisha
uanzishaji wa maeneo ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMAs) na uongoaji wa
Shoroba za Wanyamapori ambapo maeneo haya ya WMAs yameendelea kuchangia katika
kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo
kwenye vijiji wanachama” amesema Mhe. Chana.
Amefafanua kuwa maeneo ya WMAs yamechangia katika uchumi hasa
kupitia uwekezaji katika sekta ya uwindaji wa kitalii na utalii wa picha ambayo
imeendelea kukua na kuwa chachu ya uchumi kwa wakazi wa vijiji wanachama
wanaounda Jumuiya.
“Katika kipindi cha Mwaka 2023/2024 Serikali imetoa mgao wa
takribani bilion 13.2 kwa wanufaika ikiwemo WMAs zinazofanya shughuli za utalii
ambazo tunaamini zimetumika kwa mujibu wa Kanuni za WMAs kutekeleza miradi ya
maendeleo ya vijiji” amesisitiza Mhe. Chana.
Aidha, Mhe. Chana amesema uvamizi wa maeneo ya shoroba za
wanyamapori umechangia ongezeko la migongano baina ya binadamu na wanyamapori
wakali na waharibifu hususani tembo katika maeneo ya wananchi na kusababisha
taharuki kwa wananchi na uharibifu wa mali.
“Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Wizara imekuwa ikichukua
hatua mbalimbali za utatuzi ikwemo kuendesha doria za udhibiti wa wanyamapori
wakali na waharibifu kwa ushirikiano wa taasisi zetu za TAWA, TANAPA na Wilaya
ya Wanging’ombe; kutumia teknolojia katika udhibiti wa wanyamapori ikwemo ndege
nyuki, mikanda maalum ya mawasiliano (GPS Satellite Collars), na mabomu baridi;
kutoa elimu kwa wananchi juu ya mbinu za kukabiliana na wanyamapori wakali na
waharibifu, Amesema Mhe.Chana
Ameongeza kuwa " Tumeweza kutoa mafunzo kwa Wakufunzi 170 juu
ya mbinu za kukabiliana na wanyamapori wakiwemo Wakufunzi 5 kutoka Wilaya
Wanging’ombe; kutoa semina ya kujenga uelewa kwa Maafisa Wanyamapori 122 kutoka
Halmashauri za Wilaya mbalimbali nchini ikiwemo Wanging’ombe, Makete,
Makambako, Ludewa, Njombe DC na Njombe TC” amesisitiza Mhe. Chana.
Vilevile, amesema Serikali inaendelea kuimarisha vikosi vya doria
za udhibiti kwa kuwapatia mafunzo maalum vijana ili kuwaandaa kuwa Askari
Wanyamapori wa Vijiji (VGS) ambapo katika awamu ya kwanza jumla ya vijana 100
kutoka Halmashauri mbalimbali nchini wakiwemo vijana 30 kutoka Wanging’ombe,
Makete, Makambako, Ludewa, Njombe DC na Njombe TC wataanza mafunzo hayo tarehe
17 Aprili 2025 hadi tarehe 16 Mei 2025 katika Chuo cha Wizara cha Likuyu
Sekamaganga kilichopo Mkoa wa Ruvuma.
Katika hatua nyingine, Mhe.Chana amesema ili kukabiliana na
changamoto ya mamba, Wizara imejenga vizimba kumi na nane (18) vya kuzuia mamba
na viboko katika maeneo mbalimbali nchini yenye changamoto ikiwemo Wilaya ya
Ludewa ambapo vizimba viwili (2) vimejengwa ili kuimarisha usalama wa wananchi
dhidi ya mamba na viboko pindi wanapotumia maji ya mto.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya
Maliasili na Utalii, CP Benedict Wakulyamba amesema kuwa Wilaya ya Wanging’ombe
ina Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Umemaruwa ambayo ni ushoroba muhimu wa
wanymapori wanapotoka Hifadhi ya Taifa Ruaha kwenda Pori la Akiba
Mpanga-Kipengele hivyo semina hiyo ni muhimu kwa wananchi kuendeleza uhifadhi
wa maeneo hayo.
“Katika mwaka wa fedha 2024/2025 Wizara imepanga kuendelea kujenga uwezo kwa wadau mbalimbali nchini kuhusu usimamizi wa WMA, Shoroba na mikakati ya kudhibiti migongano baina ya binadamu wa wanyamapori. Aidha, leo tupo hapa kwa ajili ya kutekeleza mpango huo ili wadau wa wilaya ya Wanging’ombe wawe na sauti moja ya uhifadhi.”amesema CP Wakulyamba.
Semina hiyo imehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Mhe. Zakaria Mwansasu, Katibu Tawala Wilaya ya Wanging’ombe, Bi. Veronoca Sanga, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Katibu wa CCM Wilaya ya Wanging’ombe; Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Anthonia Raphael, Wawakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Makamishna Wasaidizi wa Kanda kutoka TAWA, TANAPA na TFS, Wataalam kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii,wadau mbalimbali wa uhifadhi kutoka kata za wilaya ya Wangingombe, Viongozi wa Jumuiya za Wanyamapori Umemarua na Wenyeviti na Watendaji wa vijiji.
No comments:
Post a Comment