Na Dotto Mwaibale,Tanga
WAKATI Wanawake wa Mkoa wa Tanga wakiendelea kupanga mikakati ya kurejesha maadili katika jamii, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Selebosi Mustafa amewaagiza watendaji wa kata kusimamia maadili katika maeneo yao ambako jamii inaishi.
Mustafa ametoa maagizo hayo wakati akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri hiyo kilichoketi Januari 2, 2026 jijini humo.
“ Naomba nizungumzie suala zima la amani, sasa hivi kwenye kata zetu kunachangamoto lakini kwa makusudi kabisa watendaji mmekaa nazo kimya hasa matukio ya uhalifu,” alisema Mustafa.
Alisema kuna vijana katika jiji hilo maarufu kama 'vishandu' walikuwa wakitishia uhuru na amani ya wananchi ambao wanapora watu mali zao na simu na ninyi watendaji mnajua,” alisema.
Alisema anatambua kwamba wahalifu hao hawatoki nje ya Tanga bali wanatoka ndani ya Tanga katika mitaa ambayo wanaiongoza.
“Sasa tuna kwenda kufanya kazi ngumu isiyo na maelezo ya kuwadhibiti wahalifu hao na sijui watendaji waliopo kwenye mitaa hiyo wanayoiongoza wanafanya nini,” alihoji Mustafa.
Mustafu alisema Jeshi la Polisi limewapa Mrakibu wa jeshi hilo kila kata na kata nyingine mpaka askari wa Uhamiaji yupo na kueleza kuwa Tanga neno amani ni asili yake na mahali pake hivyo aliwataka watendaji wakalisimamie jambo hilo kuanzia kwenye mitaa hadi kata ili jiji hilo liwe na utulivu.
Mbali ya tabia hiyo ya uporaji kumekuwa na ngoma sisizo na maadili kama vigodoro, vijamvi asilia ambazo zinakesha hadi asubuhi huku watendaji wa maeneo husika wakiziona bila kuchukua hatua yoyote jambo ambalo linachangia mmomonyoko wa maadili.
“Ninyi ndiyo mnaotoa vibali ambavyo vinaelekeza ukomo wa muda wa kumaliza shughuli zao lakini utakuta zinakesha hadi asubuhi nawaagiza kuanzia sasa muende kusimamia jambo hilo na kulitolea taarifa,” alisema Mustafa.
Meya huyo alieleza kuwa utoaji wa vibali hivyo bila kuzingatia maadili na ustawi wa jamii umekuwa chanzo cha kuongezeka kwa vitendo visivyokubalika, akisisitiza kuwa watendaji wa serikali za mitaa wanapaswa kubeba dhamana ya kulinda maadili ya jamii wanayoihudumia.
Aidha, Mustafa alisema kuwa vitendo hivyo visivyo na maadili vimekithiri zaidi eneo la Sabasaba ambako baadhi ya watu wameanzisha gesti bubu zinazotoza hadi sh. 2000 huku eneo hilo wakiwepo maafisa wa serikali waliopewa dhamana wakiviangalia bila ya kuchukua hatua yoyote.
Akizungumzia suala la ukusanyaji wa mapato alisema wamepiga hatua kidogo lakini watapiga hatua zaidi baada ya madeni wanayozidai baadhi ya taasisi na viwanda kulipwa na wakipiga mahesabu watavuka lengo la makusanyo.
Aliongeza kuwa Mkoa wa Tanga ulikuwa ukiongoza kwa ufaulu lakini umeshuka hadi kushika nafasi ya 10 kitaifa ambapo amewataka watendaji wa sekta ya elimu kuanzisha mikakati ambayo itarejesha ufaulu katika mkoa huo.
Aidha, Mustafa alisisitiza suala la usimamiaji wa mIradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao kukamilika kwa wakati kulingana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa na Serikali badala ya kumuachia kazi hiyo mkurugenzi.
0 Comments