Header Ads Widget

Responsive Advertisement

WANAWAKE TANGA WAUNGANA KUREJESHA MAADILI

 Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally akizungumza katika Kongamano la wanawake wa Kiislamu la kuukaribisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambalo limefanyika Januari 31, 2026 Jijini Tanga. Kushoto ni Sheikh wa Mkoa wa Tanga, Alhaji Juma Luwuchu na Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Ayubu  Semabili.
Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally akisisitiza jambo kwenye kongamano hilo.Mkuu wa Wilaya ya Muheza Ayubu Semabili akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batlida Burian 
Mshereheshaji (MC) wa kongamano hilo Saum Iddi kutoka Dar es Salaam akimkabidhi Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally zawadi kutoka kwa wanawake wa kongamano hilo. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhe. Ayubu Semabili.
Sheikh wa Mkoa wa Tanga, Alhaji Juma Luwuchu akizungumza.
Mwenyekiti wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali Tanzania (NGO’s),  Mwantumu Mahiza, akisisitiza jambo kuhusu kumomonyoka kwa maadili mkoani Tanga.
Mratibu wa kongamano hilo Shamsa Diwani, akizungumza.
Wanawake wa Kiislamu wakiwa kwenye kongamano hilo
Kongamano likiendelea.
Wanawake wa Kiislamu wakiomba dua wakati wa kufungua kongamano hilo.
Mwanafunzi wa Sekondari ya Pongwe Zainabu, Jumbe akisoma Quran kwenye kongamano hilo.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Pongwe, Zena Hassan akisoma utenzi.
Kongamano likiendelea.
Kongamano likiendelea.Sheikh  Shaib Khuzeima akitoa mada kwenye kongamano hilo.
Mshereheshaji (MC) wa kongamano hilo Saum Iddi kutoka Dar es Salaam akiwajibika ipasavyo.Amiri Khofu kutoka Taasisi ya Jamarat Haji and Umra Travelles, akitoa mada kuhusu maadili huku akielezea kisa cha mtu aliyekuwa amekubuhu kwa kutenda dhambi ambaye alizikwa na watu wanne  aliokuwa amewakodi kwa kuwapa fedha siku chache kabla ya kifo chake na kumuambia mama yake asije akamuambia mtu atakapofariki.Kisa hicho kiliwatoa machozi wanawake waliokuwepo kwenye kongamano hilo. Ukitaka kukijua kisa hicho chenye mafunzo piga namba 0715318615 kitakujenga kiimani hasa kimaadili.Bi. Khadija Mgambo kutoka Taasisi ya Tawheed Development Network Hajj and Umra ya Dar es Salaam akizungumzia umuhimu wa kwenda kuhiji Maka na kueleza kuwa mtu yeyote hata masikini anaweza kwenda iwapo tu mtu atajipanga kwenda na Alah atawafanyia wepesi na kuwabariki katika kazi zao na kuwaongezea kipato.
----------------------------

Na Dotto Mwaibale, Tanga

Wanawake wa Mkoa wa Tanga wanatarajia kukutana kujadili na kupanga mikakati madhubuti ya kurejesha maadili katika jamii, kufuatia mkoa huo kushika nafasi ya tatu kitaifa kwa kukithiri kwa mmomonyoko wa maadili.

Hayo yameelezwa katika Kongamano la Wanawake wa Kiislamu la kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, lililofanyika Januari 31, 2026 jijini Tanga.

Mgeni wa heshima katika kongamano hilo Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally, alihudhuria  akiwa ameambatana na viongozi waandamizi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) pamoja na masheikh mbalimbali.

Kongamano hilo liliandaliwa na Wanawake wa Kiislamu wa kikundi cha Subra na Nusra cha Mkoa wa Tanga.

Akizungumza awali, Mwenyekiti wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) Tanzania, Mwantumu Mahiza, alisema Mkoa wa Tanga umekumbwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili hali inayohitaji hatua za haraka kunusuru jamii.

“Wananchi wa Mkoa wa Tanga tunapaswa kuchukua hatua za makusudi kurejesha maadili tuliyokuwa nayo awali, kwani kwa sasa mkoa wetu umeshika nafasi ya tatu kitaifa kwa mmomonyoko wa maadili,” alisema Mahiza.

Mahiza alieleza kuwa awali Tanga ilikuwa ni mkoa uliotambulika kwa ustaarabu na maadili mema, hasa ikizingatiwa kuwa ni miongoni mwa chimbuko la Uislamu nchini, lakini kwa sasa hali imebadilika.

Alisema tafiti za awali zilizofanywa kwa mfumo wa ‘sampling’ na baadhi ya mashirika zinaonesha Tanga kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa mmomonyoko wa maadili.

“Nimesema ukweli ili kila mmoja achukue hatua kwa nafasi yake. Wanawake wa Kiislamu tuna wajibu mkubwa wa kutoa malezi bora kama ilivyokuwa zamani,” alisema Mahiza.

Kwa mujibu wa Mahiza, sababu zinazochangia hali hiyo ni pamoja na asilimia 60 ya watoto kuishi katika familia zenye ndoa zilizovunjika au zisizo salama, huku asilimia 20 wakikua katika malezi holela ya kuhamahama kutoka mlezi mmoja hadi mwingine.

Aliongeza kuwa changamoto ya uchumi duni imechangia kwa kiasi kikubwa malezi hafifu, huku asilimia 10 ya mmomonyoko wa maadili ikitokana na tabia za watoto wenyewe.

Mahiza pia alieleza kuwa Mkoa wa Tanga unakabiliwa na changamoto kubwa ya matumizi ya dawa za kulevya, akibainisha kuwa sensa ya mwaka 2022 ilionesha watoto wa kike kuanza mahusiano katika umri mdogo wa hadi miaka tisa.

Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir, aliwataka wanawake wa Kiislamu kudumisha mshikamano na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuvuruga umoja wao.

“Msikubali kuingiza harufu yoyote yenye lengo la kuharibu mshikamano wenu,” alisema Mufti Zubeir, huku akiwahimiza wanawake kujikita katika elimu na shughuli za kiuchumi ili kuharakisha maendeleo.

Mufti Zubeir alisema kupitia mshikamano wao, wanawake wanaweza kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo uanzishaji wa hospitali maalum ya akina mama wajawazito.

Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Ayubu Semabili, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Batlida Burian, aliwahimiza wanawake kutunza amani na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Aidha, alisema Mkuu wa Mkoa ametoa msaada wa Shilingi milioni tatu kwa ajili ya kusaidia wanawake wasio na uwezo kupata mahitaji ya chakula wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Naye Mratibu wa Kongamano hilo, Shamsa Diwani, alisema lengo kuu ni kuwafikia wanawake katika maeneo yote ya Mkoa wa Tanga ili kujadiliana kwa pamoja namna bora ya kurejesha maadili mema katika jamii.

Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale
 simu namba 0754362990

Post a Comment

0 Comments