Mratibu wa Vifaa Tiba, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Eng. Elfrida Deogratias akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mafunzo.
Watoa huduma ya afya katika vituo vya kutolea huduma (Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati) wilayani Ikungi, wamehimizwa kuzingatia matumizi salama na sahihi ya vifaa tiba na vitendanishi ili kupunguza matukio na madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa hizo.
Ushauri huo umetolewa na Bw. David Matle, Kaimu Meneja, Ufuatiliaji Usalama wa Vifaa Tiba na Vitendanishi kutoka TMDA Makao Makuu, Dodoma wakati wa zoezi la kuhamasisha watoa huduma hao kuhusu utoaji taarifa za madhara na matukio ya vifaa tiba na vitendanishi. Zoezi hili liliendeshwa na TMDA Makao Makuu ikishirikiana na Ofisi ya Kanda ya Kati kwenye vituo tisa (9) vilivyopo Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida kuanzia Aprili 8 hadi 10, 2026 .
Akifafanua kuhusu matumizi salama na sahihi ya vifaa tiba na vitendanishi, Bw. Matle, ameeleza kuwa matumizi hayo yanahusisha kutumia vifaa kwa matumizi yaliyokusudiwa na watengenezaji na kufuata maelekezo ya utunzaji, matumizi na matengenezo ya vifaa tiba ili kuhakikisha vifaa hivyo vinaendelea kukidhi vigezo vya ubora, usalama na ufanisi wakati wote wa matumizi.
Aidha, aliwaeleza watoa huduma pale ambapo vifaa tiba na vitendanishi vinatumika kwa usahihi na bado vikasababisha madhara kwa wagonjwa na wao wenyewe, wasisite kutoa taarifa TMDA haraka iwezekanavyo ili hatua za kiudhibiti zichukuliwe na kuzuia madhara hayo yasiendelee kutokea kwenye maeneo mengine ya huduma ambako vifaa hivyo vimesambazwa.
Naye Afisa Vifaa Tiba kutoka TMDA Makao Makuu, Dkt. Nassoro Matuzya, pia amesema matumizi sahihi ya vifaa tiba na vitendanishi sio tu yanaongeza ubora wa huduma, bali pia yanaongeza imani ya jamii kwa watendaji wa Sekta ya Afya kuhusu huduma itolewayo kwenye vituo.














0 Comments