Aliyekuwa muuguzi na mtunza dawa katika Zahanati ya Bunyambo wilayani Kibondo, Leonard Alfonsi Mosha (31), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kibondo akikabiliwa na shtaka la ubadhirifu na ufujaji wa dawa za binadamu zenye thamani ya Sh. 2,020,345.36.
Mosha amefikishwa mahakamani Septemba 3, 2026 katika shauri la uhujumu uchumi namba ECO.19924/2026, linalosikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Maila M. Makonya (PRM).
Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Balamu Kisumo, amewasilisha shtaka hilo kwa niaba ya Jamhuri.
Kwa mujibu wa mashtaka, mshtakiwa anakabiliwa na kosa la ubadhirifu na ufujaji kinyume na Kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, marejeo ya mwaka 2023.
Mahakama imeelezwa kuwa katika kipindi cha Novemba 2023, wakati Mosha akiwa muuguzi na mtunza dawa katika Zahanati ya Bunyambo, aliomba dawa kutoka katika zahanati mbalimbali akieleza kuwa dawa hizo zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya Zahanati ya Bunyambo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mashtaka, dawa hizo alizitumia kwa maslahi yake binafsi, hatua ambayo inadaiwa ilisababisha ubadhirifu wa dawa zenye thamani ya Sh. 2,020,345.36.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa alikana kufanya kosa hilo na mahakama ilimpa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Septemba 21, 2026, ambapo litasikilizwa kwa ajili ya uwasilishaji wa hoja za awali (PH).
TAKUKURU Mkoa wa Kigoma kupitia ofisi yake ya Wilaya ya Kibondo imeendelea kusisitiza umuhimu wa matumizi sahihi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma, ikiwemo dawa zinazotolewa kwa ajili ya huduma kwa wananchi.

0 Comments