Waziri Kairuki ameyasema hayo wakati akishiriki Mkutano wa Saba wa Jukwaa la Sera za Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (WTPF-26), unaofanyika Nassau, Bahamas, ambapo amesema hatua hizo zinalenga kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali 2024–2034.
Amesema Tanzania imekamilisha ujenzi wa minara 758 ya teknolojia ya 4G, hatua iliyowezesha zaidi ya vijiji 1,400 na takribani wananchi milioni 8.5 waliokuwa hawapati huduma za mawasiliano ya uhakika kuunganishwa na huduma hizo.
Aidha, kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Serikali imeanzisha Vilabu vya Kidijitali 800 kwa ajili ya kujenga ujuzi wa TEHAMA, kuwezesha huduma za Wi-Fi katika maeneo 100 ya umma na kujenga maabara za kompyuta katika shule 250 za umma, zikiwemo huduma zinazozingatia mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu.
Akieleza vipaumbele vya Tanzania katika kuziba pengo la kidijitali, Waziri Kairuki amesema nchi inalenga kupanua huduma za mawasiliano kwa gharama nafuu, kuongeza ujuzi wa kidijitali na matumizi ya Akili Unde (AI), pamoja na kuendeleza miundombinu ya kidijitali iliyo salama, jumuishi na inayolinda taarifa binafsi za watumiaji.
Waziri Kairuki amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) na wadau wengine wa maendeleo kuimarisha ujuzi wa kidijitali na matumizi ya Akili Unde barani Afrika. Amesisitiza kuwa mafanikio ya mageuzi ya kidijitali hayapaswi kupimwa kwa idadi ya minara pekee, bali kwa namna teknolojia inavyoboresha maisha, kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika uchumi wa kidijitali.


0 Comments