KAMPUNI
ya mbegu ya TANSEED International yenye makao makuu mjini Morogoro
imeandaa maonesho ya shamba darasa ya teknolojia mpya ya mbegu za
mahindi ya TAN 222 kukomesha kiduha “trigaway maize”kwa ajili ya
kudhibiti magugu hatari ya kiduha kwenye zao la mahindi.
Maonesho hayo yatafanyika kesho
(Jumamosi) katika maadhimisho ya siku ya wakulima (Farmer Field Day)
katika kijiji cha Mkuza wilayani Mheza ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Mkuu
wa Mkoa wa Tanga, Chiku Galawa.
Ambapo yatahudhuriwa na watafiti
wa mazao ya kilimo, wataalamu wa ugani, makampuni ya mbegu, wakulima,
taasisi za serikali na zisizo za kiserikali mkoani humo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa
kampuni hiyo, Isaka Mashuri leo jijini Dar es salaam katika ukumbi wa
mikutano wa Idara ya Habari -MAELEZO alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari juu ya maadhimisho hayo yatakayofanyika mkoani Tanga.
Alisema lengo la maonesho hayo ni
kuhamasisha wakulima, watafiti, washauri wa ugani, wasiasa, taasisi za
serikali na zisizo za kiserikali pamoja na wadau wengine ni kuhusu
tishio linatokana na magugu ya kiduha.
“Magugu ya kiduha yamekuwa ni
tatizo kubwa kwa wakulima wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa
kipindi cha miongo saba. Kiduha ni magugu tegemezi yanayojishikiza
kwenye mizizi ya mazao ya nafaka na kunyonya maji , madini na
virutubisho vingine.” alisema Mashuri.
Mashuri aliongeza kuwa magugu
hayo huharibu ya mahindi kwa kutoa sumu na kuweza kuangamiza mimea ya
mazao hata kabla magugu hayajajitokeza juu ya ardhi.
“Magugu ya kiduha huzaa mbegu
nyingi kati ya 5,000 hadi 200,000 kwa mmea mmoja, hivyo kufanya tatizo
kuwa kubwa zaidi kwani mbegu za kuduha huweza kubaki zikiwa hai
aridhini kwa muda mrefu zaidi ya miaka 20 na zaidi na kusababisha
upungufu wa chakula kila mwaka, ” alisema Mashuri.
Alisema kwamba inakadiriwa kuwa
takribani hekari milioni 1.5 za ardhi Afrika Mashariki zimeathiriwa na
magugu ya kiduha ambapo aliitaja mikoa iliyoathirika Tanzania na
magugu hayo ni pamoja na Morogoro, Pwani , Tanga, Dodoma,Singida,
Tabora, Shinyanga , Mwanza, Mara, Ruvuma, Iringa, Mbeya, Rukwa, Lindi
na Mtwara na kubainisha kuwa ni zaidi ya ekari 1,500,000 zimeathirika.
Aidha Mashauri alieleza kuwa
magugu hayo husababisha upotevu wa mavuno takribani tani milioni 1.7 za
nafaka zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 356 ambazo ni sawa
na Sh.bilioni 584.6 za Kitanzania kwa mwaka.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la BASF
Nchini Kenya linalojishughulisha na shughuli za madawa ya kilimo, Sammy
Wairuingi alisema kuwa Tanzania tushangilie kwa furaha ya kuja kwa
fursa hii ya teknolojia mpya kwani itasaidia kuzalisha chakula cha
kutosha kulisha familia ,kufukuza njaa na umasikini.
Kampuni ya TANSEED inashirikiana
na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mahindi na Ngano ‘ International
Maize and Wheat Improvement Centre’ (CIMMYT), Taasisi ya kimataifa ya
‘African Agriculture Technology Foundation’ (AATF) inayojishughulisha na
kuunganisha sekta za umma na binafsi katika usambazaji wa teknolojia za
kilimo, na kampuni ya madawa ya kilimo na majumbani BASF.
0 Comments