Na Mwandishi Wetu
TAMASHA
la Pasaka mwaka huu linatarajiwa kufikisha miaka 14 tangu kuanzishwa
kwake na kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam.
Tangu
kuanzishwa kwa tamasha hilo Watanzania wameweza kujumuika pamoja siku
ya sikukuu hiyo ya kufa na kufufuka kwa Kristo Yesu kwa kutumbuizwa na
waimbaji mbalimbali wa nyimbo za Injili kutoka ndani na nje ya nchi ya
Tanzania.
Umaarufu
wa matamasha hayo umetokana na waandaaji wake kuweza kuyaandaa kwa
ubunifu mkubwa na umakini ambapo tamasha hilo limekuwa kivutio kwa watu
mbalimbali huku mikoa mingi nchini ikipigania tamasha hilo kufanyika
mikoa hiyo.
Pamoja
na Kampuni ya Msama Promotions kuandaa tamasha la Pasaka kila mwaka,
kampuni hiyo pia ni waandaaji wa tamasha la Krismasi ambalo lilianza
kufanyika mwaka jana ikiwa ni mara yake ya kwanza.
Hata
hivyo Mwenyekiti wa matamasha hayo, Alex Msama anabainisha wazi kuwa
matamasha hayo yatakuwa ya kudumu na yenye lengo moja la kuhamasisha
amani, umoja na mshikamano nchini.
Hata
hivyo anaeleza kuwa kauli mbiu ya tamasha la Pasaka mwaka huu ni
‘Uzalendo kwanza, haki huinua taifa’. Kauli mbiu hii ni kwa ajili ya
kuhamasisha na kuchochea juhudi za maendeleo nchini, kwa kizazi
kilichopo na kijacho.
Katika
kutimiza miaka 14 ya Tamasha la Pasaka, kampuni ya Msama Promotions
imeeleza kujiandaa vya kutosha katika kuhakikisha tamasha hilo linafana
na kuzidi kuwa bora kutokana na uzoefu wa kuandaa matamasha hayo nchini
kuongezeka siku hadi suku.
Pamoja
na kujiandaa vya kutosha katika tamasha la mwaka huu, kampuni imeweza
kubuni utaratibu wa kufanya kile mashabiki wanahitaji kwa kutoa nafasi
kwa mashabiki kujichagulia waimbaji wanaoamini kuwa watawaburudisha
zaidi.
“Mwaka
huu tumeamua kuwaacha mashabiki wajichagulie waimbaji, hivyo tumeweka
utaratibu wa kupiga kura ambapo kwa kutumia simu za mkononi, unaenda
kwenye sehemu ya ujumbe mfupi wa maandishi, unaandika jina la msanii,
mgeni rasmi na mkoa unachokitaka kwa nyakati tofauti, kisha unatuma
ujumbe huo kwenda namba 15327, kisha tutaangalia waliopigiwa kura nyingi
nao wataweza kupata nafasi ya kuwemo katika tamasha letu la mwaka huu.”
Pamoja
na juhudi hizo za uandaaji wa tamasha hilo nchini, kampuni hiyo imeweza
kurudisha shukrani zake kwa Watanzania kila lifanyikapo tamasha hilo
nchini kwa kuhakikisha inakuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii
isiyojiweza ili kuweza kujimudu kimaisha.
Mkakati
mkubwa wa kampuni ni kujenga kituo cha kisasa kwa ajili ya watu wenye
uhitaji maalum kitakachojengwa eneo la Pugu kitakachokuwa na jina
la Jakaya Mrisho Kikwete rafiki wa wasiojiweza ambacho kitasaidia
kuwaunganisha watu wenye uhitaji maalum ili waweze kupata uangalizi wa
karibu ikiwa ni pamoja na kuonyeshwa upendo.
Katika
maandalizi ya Tamasha la pasaka linalotarajiwa kuanza Aprili 20 jijini
Dar es Salaam litaweza kujumuisha wasanii mbalimbali wa nyimbo za injili
kutoka katika nchi mbalimbali za Afrika huku waimbaji kutoka nchini
Tanzania ambao watakutana na changamoto kubwa na kujifunza kutoka kwa
wenzao kutoka nje ya nchi.
Kupitia
mapato yanayopatikana kupitia Tamasha la Pasaka husaidia wenye uhitaji
maalum kama wajane, walemavu, yatima na wengine wenye uhitaji maalum
katika maeneo mbalimbali kama ada za shule na kwingineko.
0 Comments