Rais
Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akipokea tuzo kutoka kwa Waziri wa mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membekupokea Tuzo ya
Uongozi Bora Afrika aliyotuzwa nchini Marekani ambako aliwakilishwa na
Mhe Membe.
Picha na Ikulu
………………………………………………………………………………………….
Na Aron Msigwa- MAELEZO, Dar es salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete leo Ikulu
jijini Dar es salaam amepokea Tuzo ya Utumishi Bora wa Umma Barani
Afrika kufuatia mchango mkubwa alioutoa kwa maendeleo ya wananchi wa
Tanzania na Bara la Afrika.
Akiwa
mwenye furaha mara baada ya kupokea tuzo hiyo ambayo awali ilipokelewa
kwa niaba yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Mhe. Bernard Membe jijini Washngton Marekani, Rais Kikwete amesema kuwa
ameipokea tuzo hiyo kwa moyo wa shukrani na heshima kubwa kufuatia imani
kubwa iliyoonyeshwa kwake na kwa watanzania.
“Nimeipokea
tuzo hii kwa moyo wa ukunjufu, ni tuzo ya watanzania wote kwa sababu
mambo yote niliyoyafanya sikuwa peke yangu nimeyafanya kwa kushirikiana
na watanzania wote” Amesema Rais Kikwete.
Rais
Kikwete amesema kuwa amepokea tuzo hiyo kufuatia wasomaji na wadau wa
Jarida la African Leadership Magazine ambalo huchapishwa mjini London,
Uingereza na mjini Washington kuonyesha imani juu yake kwa kumchagua kwa
njia ya kura ya maoni kama kiongozi aliyetoa mchango mkubwa zaidi kwa
maendeleo ya wananchi wake katika Bara la Afrika kwa mwaka 2013.
“Nawashukuru
sana African Leadership Magazine, kwangu ni heshima kubwa nawaomba
watanzania tuendelee kushirikiana wenzetu duniani wanaona, wanatambua na
kuthamini mchango wetu” Amesisitiza Rais Kikwete.
Awali
kabla ya kumkabidhi Rais Jakaya Kikwete Tuzo hiyo na cheti cha shukrani
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Benard Membe
amesema kuwa tuzo hiyo ni heshima kwa taifa la Tanzania kufuatia juhudi
kubwa alizoonyesha Rais Jakaya Kikwete katika kuboresha maisha ya
watanzanzania.
Amesema kuwa
wasomaji na wadau wa jarida maarufu la kimataifa la African Leadership
Magazine wamemuona Rais Kikwete kuwa Kiongozi Bora wa Afrika aliyetoa
mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya kiuchumi ya wananchi wake kwa
mwaka 2013 kwa kumpigia kura nyingi za maoni.
Aidha
ameeleza kuwa Rais Kikwete alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo katika
sherehe kubwa iliyotangazwa na kuonyeshwa moja kwa moja na mitandao
mbali mbali ya kijamii duniani pia kuhudhuriwa na watu mbali mbali
mashuhuri wakiwemo mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Marekani na Naibu
Spika wa Bunge la Tanzania Mheshimiwa Job Ndugay ambaye alikuwa
Washington kikazi.
Wengine
ni Mwakilishi katika Bunge la Wawakilishi wa Jimbo la Georgia nchini
Marekani na mwenyekiti wa wabunge weusi katika Bunge hilo, Bi. Dee
Dawkins-Haigler na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mheshimiwa
Liberata Mulamula.
Rais
Kikwete amepata tuzo hiyo akimfuatia Rais wa Sierra Leone ,
Mheshimiwa Ernest Bai Koroma, ambaye alishinda Tuzo hiyo mwaka 2012.