Random Posts

MHE. NAGU ASISITIZA SUALA LA MUUNGANO

 Na Benedict Liwenga, MAELEZO-Dodoma.
 
MUUNGANO wa Tanzania ni muungano wa damu na wa watu, ambapo Ibara ya kwanza Sura ya kwanza inaeleza kuwa msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano pamoja na katiba iliyopo na inayopendekezwa ni haki ya makubaliaono ya mwaka 1964.
 
Hayo yamesemwa leo na Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Mary Nagu wakati akichangia mada katika mjadala ndani ya bunge hilo kuhusu mambo mchakato mzima wa kusaka Katiba Mpya.
 
Mhe. Nagu amesema kuwa Hati ya Makubaliano hayo imejengeka katika misingi ya utu, udugu na kuaminiana ambapo Waasisi wa muungano huo hawakupeleka maslahi yao wenyewe binafsi wala kuzingatia suala la mali, bali walizingatia umuhimu na mahitaji  ya muungano kutokana na mambo hayo makuu matatu.
 
Ameeleza kuwa mambo wanayoyajadili bungeni hapo kwa sasa ndiyo yatatokana na muungano ambao una mfumo bora na muundo bora.
 
Mhe. Nagu amebainisha kuwa wale viongozi wenye kutaka muungano wenye gharama kubwa watawafanya wengine washindwe hapo baadaye.
 
“Naomba sana tuendelee na kuona kuwa muungano huu ni muhimu nataka niwaambie kwamba Zanzibar ni lango kuu la Jamhuri ya muungano wa Tanzania na lango hili linatuhakikishia usalama wetu na ulinzi wetu kwahivyo na Wazanzibar nao wanufaike na rasilimali za Bara, kwahiyo muungano huu ni muhimu na utanufaisha pande zote mbili mimi sina wasi wasi”, alisema Mhe. Nagu.
 
Aidha, Mhe. Nagu amegusia suala la usawa wa jinsia kupitia hamsini kwa hamsini katika uwakilishi, ajira na maeneo mengine.
 
Mhe. Nagu ameleza kuwa usawa wa jinsia utajenga jamii nzuri ya Tanzania ikiwemo kuleta heshima pamoja na haki katika jamii hiyo kwani kwa mila na desturi za Waafrika na Watanzania, wanaume hawakupaswa kuwa wamiliki wa kila kitu.
 
“Akina baba ni Custodians lakini  wakajigeuza wamiliki, tunachotaka waendelee kuwa Custodians na sisi watuone ni wenzao, kwahivyo suala la jinsia halina mjadala, kupitia uwakilishi teundelee na hamsini kwa hamsini na Katiba iseme wazi, mengine yatajitokeza kwenye Sheria ya uchaguzi”. Alisisitiza Mhe. Nagu.
 
Kuhusiana na suala la ajira na uongozi Mhe. Nagu ameeleza kuwa wanawake zaidi ya asilimia 52% wangepaswa kuwa katika kila eneo lakini hawapo na suala hilo linaleta tofauti isipokuwa mashambani ambapo chakula chote kinachotoka kwa kiasi kikubwa wanaolima ni wanawake.