WAZIRI MKUU Mizengo
Pinda amesema Serikali haitataifisha shule, zahanati, hospitali wala
Vyuo Vikuu vinavyoendeshwa na taasisi za kidini na amewahimiza wajenge
zaidi na zaidi ili kuisaidia jamii kubwa ya Watanzania.
Ametoa wito huo wakati
akizungumza na walimu, wazazi na wahitimu wa kidato cha nne wa shule ya
sekondari Magnificat iliyoko Sanya Juu, wilayani Siha mkoani
Kilimanjaro.
Waziri Mkuu ambaye
aliwasili Sanya Juu jana asubuhi (Jumamosi, Septemba 20, 2014) akitokea
Dodoma, alisema huko nyuma Serikali ilitaifisha shule na vyuo lakini kwa
kiasi fulani ilishindwa kuviendesha ikaamua kuvirudisha kwa wamiliki
wake ambao ni taasisi za kidini.
“Ni kweli huko nyuma
tulikuwa navyo, lakini tumevirudisha kwenu tunataka na ninyi ni
washirika katika kuleta maendeleo kwa wananchi walio wengi,” alisema
Waziri Mkuu.
“Nilishawahi kusema
huko nyuma na leo nasisitiza tena kwamba hatutaifisha shule, zahanati,
hospitali wala Chuo Kikuu chochote cha taasisi ya kidini. Ninawasihi
mjenge zaidi na zaidi,” aliongeza.
Waziri Mkuu ambaye
alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa shule hiyo iliyoanzishwa Januari
15, 2011, aliwakabidhi vyeti wanafunzi 42 wa kidato cha nne wanaotarajia
kufanya mtihani wa kidato cha nne Novemba, mwaka huu ikiwa ni mara ya
kwanza kwa shule ya sekondari ya Magnificat kufanya mtihani huo.
Waziri Mkuu
aliwapongeza wanafunzi hao kwa kushika nafasi ya kwanzawilayani Siha
kwenye mitihani ya utamirifu (yaani mock) katika kidato cha nne.
“Vilevile, shule hii imekuwa ya 12 kati ya shule 316 za Mkoa wa
Kilimanjaro na ya 16 kati ya shule 564 kwa Kanda ya Kaskazini Mashariki
zilizofanya mtihani huo. Mimi napata imani kuwa watafanya vizuri kwenye
mtihani wao wa kidato cha nne Novemba 2014,” aliongeza.
Mapema,Mkuu wa Shirika
la Masista la Kazi ya Roho Mtakatifu na Meneja wa Shule hiyo, Sista
Inviolata Kessy alisema shule hiuo ilianzishwa kwa lengo la kutoa elimu
bora na kuwashawishi watoto wa kike wa Kimasai waone umuhimu wa elimu na
hivyo kuwaepusha na ndoa za utotoni. Vile vile, kuwapa msingi mzuri wa
elimu kama sehemu ya maandalizi yao ya kupata elimu ya juu. Alisema
shule hiyo ambayo ni ya mchanganyiko na ya mchepuo wa sayansi na
biashara, imefanikiwa kujenga maabara tatu za kemia, fizikia na
baiolojia pamoja na chumba cha kompyuta.
Akisomarisalakwa niaba
ya wahitimu, Anastazia Kimaro alisema shule hiyo inakabiliwa na
changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa jengo la utawala pamoja na basi la
shule la kuwapeleka wananfunzi kwenye ziara za mafunzo.Aliomba pia wawe
wanapelekewa magazeti ya kila siku na kila wiki ili wanafunzi wa shule
waweze kupata taarifa mbalimbali za mambo yanayojiri nchini na duniani.
0 Comments