Mwalimu wa muda wa darasa la awali, Shule ya Msingi Nakayaya, Teckla Milanzi akionesha baadhi ya nakala za vitabu walivyonavyo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Majengo, Madina Mkali akizungumza na mwandishi wa habari hizi (hayupo pichani) ofisini kwake.
Mwalimu Christina Komba (kulia) wa darasa la awali Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko akiwa darasani.
Wanafunzi
wa darasa la awali Shule ya Msingi Nakayaya wakiwa darasani. Hata hivyo
shule hii haina chumba cha darasa la awali chumba hiki kimejengwa kwa
matumizi mengine na kwa sasa kinatumika kwa muda kwa kuwa kipo katika
ujenzi.
ELIMU YA AWALI YA ENDESHWA BILA VITABU TUNDURU.
Tunduru
SHULE nyingi za msingi zenye
madarasa ya awali Wilayani Tunduru zimekuwa zikiendeshwa kwa changamoto
mbalimbali ikiwemo ya kutokuwa na vitabu vya baadhi ya masomo kabisa
huku zikiwa na upungufu mkubwa wa vitabu kwa masomo mengine.Hali hiyo
imebainika hivi karibuni katika uchunguzi uliofanywa kwa baadhi ya Shule
za Msingi za Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma huku walimu wa madarasa
hayo wakielezea jitihada binafsi wanazozifanya kukabiliana na changamoto
hiyo.
Mwalimu Christina Komba wa darasa la awali Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko akizungumzia hali hiyo alisema darasa lake halina vitabu vya masomo kama ya sanaa, Haiba na Michezo
na wala miongozo ya namna ya ufundishaji hivyo kila mwalimu
anayefundisha darasa hilo hubuni nini afundishe katika masomo
hayo.“Madarasa ya elimu ya awali hayana vitabu, hayana miongozo…huwa
tunaazima au ukipata hela yako wewe binafsi unaenda kununua kitabu
kimoja au viwili ili uweze kuwasaidia watoto. Na baadhi ya masomo hayana
vitabu kabisa hata ukienda madukani katika Wilaya yetu vitabu kama
Haiba na Michezo, pamoja na Sanaa hazipo kabisa madukani,” alisema Bi.
Komba.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi
Nanjoka, Batadhari Mkwela akizungumzia shule yake alisema licha ya
usajili wa wanafunzi wa awali kuongezeka kila mwaka upatikanaji wa
bajeti ya kuendesha elimu hiyo ni changamoto kubwa huku uchangiaji kwa
wazazi ikiwa wa kusuasua.“…Darasa la awali linahitaji vitendea kazi
lakini havipo, hatuna vifaa kama vitabu vya kutosha, nyenzo za
kufundishia, hakuna bajeti hata ya vifaa hivi toka Serikalini, hatuna
hata madawati maalum kwa ajili ya wanafunzi wa darasa hili,” alisema
Mkwela.Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Majengo, Madina Mkali
alisema uendeshaji wa darasa la awali shuleni hapo ni wa kusuasua
kutokana na kutokuwa na bajeti inayoletwa kusaidia elimu hiyo, isipokuwa
kwa baadhi ya mwaka kuletwa madawati kumi kwa ajili ya wanafunzi wa
awali.
“…Uendeshaji elimu ya awali hapa
ni wa wastani kwa kweli kutokana na changamoto zinazotukabili, kwanza
vifaa vya kuwafundishia watoto hawa ni tatizo na wazazi kwa eneo hili
wamekuwa hawana mwamko wa elimu hii kabisa. Kwanza hawachangii michango
ya chakula kama inavyotakiwa ili mtoto apate chochote awapo shuleni,”
anasema mwalimu Mkali.
Kwa upande wake mwalimu wa darasa
la awali, Shule ya Msingi Nakayaya, Teckla Milanzi akitolea mfano
shuleni hapo alisema vitabu vya Kiswahili, Kiingereza, Sayansi na
Hisabati kuna nakala moja moja tu kwa kila somo, ambazo huzitumia yeye
mwenyewe.Aidha mwalimu Milanzi aliongeza kuwa darasa hilo licha ya kuwa
na changamoto kedekede hata kwenye mgao wa fedha zinazoletwa shuleni
kila mara halimo jambo
ambalo husababisha hali kuendelea kuwa mbaya zaidi.Hata hivyo mwalimu
wa darasa la awali Shule ya Msingi Majengo, Hadija Makamla alisema
anavyo baadhi tu ya vitabu vinavyoitajika katika darasa hilo, nakala
ambazo pia ni chache ukilinganisha na ukubwa wa darasa lake. “…Ninazo
nakala chache kwa ajili ya mwalimu tu ila wanafunzi hawana hata
kimoja…lakini kuna masomo mengine sina vitabu kabisa kama vile Sanaa na
Haiba ya Michezo sina kabisa hata mimi,” anasema mwalimu Makamla.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa ushirikiano na HakiElimu
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa ushirikiano na HakiElimu
0 Comments