Kaimu
Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Godfrey Mngereza
akijumuika na Kikundi cha Sanaa cha watoto cha Blessed Hill kutoa
burudani kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza hilo lililofanyika mapema wiki
hii.
Msanii
mkongwe wa Sanaa za Maonesho Bakari Mpelemba maarufu kama Mzee Jangala
(Kulia) akifuatilia kwa makini burudani za ngoma za asili na maigizo
zilizokuwa zikitolewa na kikundi hicho cha Blessed Hill sambamba na
wadau wengine wa Sanaa.
Kikundi hicho kikiendelea kuonesha manjonjo ya ngoma mbalimbali za asili kwenye Jukwaa la Sanaa
Na Mwandishi Wetu
Wadau wa Sanaa wameeleza
kusikitishwa na kudumaa kwa utamaduni na mwamko mdogo miongoni mwa
watanzania katika kuthamini utamaduni huku wakitoa wito kwa Serikali
kufikiria kurejesha masomo ya Sanaa katika mitaala ya shule za msingi
kama ilivyokuwa zamani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa lililofanyika mapema
wiki hii kwenye viwanja vya Baraza hilo, wadau hao walisema kwamba ni
muda muafaka sasa wa kujenga misingi ya Utamaduni kutoka ngazi za chini
hasa mashuleni ili kuepuka kutokomea kwa utamaduni wa mtanzania.
“Tunahitaji kujiuliza kama
tunataka kupata utambuzi wa mtanzania au kukubali kupoteza utamaduni
wetu. Hakuna jinsi kama taifa tunaweza kupiga hatua kama hatuthamini
utamaduni na kuhakikisha watoto wetu na vizazi vijavyo vinarithi
utamaduni wetu” alisisitiza msanii maarufu wa Sanaa za Maonesho Bakari
Mpelemba maarufu kama Mzee Jangala.
Aliongeza kwamba, ni wajibu wa
kila mmoja aliyepo sasa kuhakikisha anauona utamaduni kama urithi mkuu
kwa watoto na vizazi vijavyo na kusisitiza kwamba kama jamii itashindwa
kutimiza hili basi si ajabu vizazi vijavyo kuja kupiga viboko makaburi
ya baba na mama zao.
Msanii mwingine mkongwe wa Sanaa
za Maonesho Nkwama Bhallanga alisema kwamba muda umefika sasa kuanza
kusukuma utambuzi wa mtaala wa Sanaa katika shule za msingi kwani ndiyo
njia pekee ya kujenga jamii inayojitambua lakini pia uwezo wa kumudu
masomo miongoni mwa watoto mashuleni.
“Sanaa huleta ukakamavu, huwajenga
watoto katika misingi ya kujielewa na kuzingatia masomo yao mashuleni.
Watoto wanaojikita kwenye sanaa na masomo mengine ni wepesi kufanya
vizuri darasani pia” alisisitiza Ballanga.
Awali wakitoa burudani kwenye
Jukwaa hilo, watoto wa shule ya awali na msingi ya Blessed Hill
inayopatikana eneo la Kitunda, wilaya ya Ilala katika mkoa wa Dar es
Salaam, waliigiza maigizo mbalimbali yaliyobeba maudhui ya kutoa wito
kwa wadau wa Utamaduni kuanza kuthamini utamaduni na kuurithisha kwa
watoto.
0 Comments