Mke
wa Rais Mama Janeth Magufuli akikabidhi sehemu ya vyakula hivyo kwa Mwenyekiti
wa Kituo cha Charambe Islamic Center Dkt. Haruni Kondo aliyepokea kwa niaba ya
vikundi vigine vinne. Mke wa Rais amekabidhi mchele kilo 500, sukari kilo 500
na tende kilo 28, tukio hilo limefanyika katika ofisi ya Mke wa Rais Ikulu
jijini Dar es Salaam.
Khalifa
wa Zawiyatul lqadiria, Abas Hamdan watatu kutoka kulia akiongoza dua ya
kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na viongozi wengine
wakuu wa serikali mara baada ya tukio la kukabidhi vyakula hivyo. Wengine
katika picha ni Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Mke wa Waziri mkuu Mama Marry
Majaliwa pamoja na viongozi mbalimbali vya vikundi vya kulea watoto yatima na
watu waishio kwenye mazingira magumu.
Mke
wa Rais Mama Janeth Magufuli akiwa na
mke wa Waziri Mkuu Mama Marry Majaliwa katika picha ya pamoja na
viongozi mbalimbali wa vikundi vya kulea watoto yatima na watu waishio kwenye
mazingira magumu. Tukio hilo limefanyika katika Ofisi za Mke wa Rais Ikulu
jijini Dar es Salaam.
Mke
wa Rais Mama Janeth Magufuli akisalimiana na Mama Mlezi wa Kituo cha Charambe
Islamic Center Asile Zahali mara baada ya kukamilika zoezi la utoaji wa vyakula
mbalimbali kwa vituo vinne vya kulea watoto na watu waishio kwenye mazingira
magumu.
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akiwa na mke wa Waziri Mkuu
Mama Marry Majaliwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa vituo hivyo kabla ya
kuwakabidhi vyakula hivyo katika Ofisi yake Ikulu jijini Dar es Salaam.
PICHA NA IKULU
------------------------------------------------------------------------------------------------
Mke wa Rais Mama Janeth
Magufuli amekabidhi chakula kwa ajili ya futari wakati huu wa mfungo wa mwezi
Mtukufu wa Ramadhani kwa vituo vinne vya kulea watoto yatima na wale waishio
katika mazingira magumu Jijini Dar es salaam.
Vyakula hivyo
vimekabidhiwa leo tarehe 18 Juni, 2016 katika ofisi ya Mke wa Rais Ikulu Jijini
Dar es salaam vimejumuisha Mchele kilogramu 500, Sukari kilogram 500 na Tende
kilogramu 28.
Akizungumza mara baada
ya kukabidhi vyakula hivyo, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli aliyeongozana na
Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa amewatakia heri Waislamu wote katika mfungo
wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuwasihi waendelee kuliombea Taifa amani na
utulivu.
(“Tunawatakia mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa
Ramadhani, katika kipindi hiki tunawaomba mzidi kuiombea nchi yetu amani,
viongozi wetu wa nchi na watanzania wote kwa ujumla, nchi ikiwa na amani ndio
mambo mengi mazuri yanaweza kufanyika”)
Kwa niaba ya vituo
vilivyopatiwa vyakula hivyo, Mwenyekiti wa Kituo cha Charambe Islamic Center
Dkt. Haruni Kondo amemshukuru Mke wa Rais kwa kutoa vyakula hivyo na ameeleza
kuwa kitendo hicho kinaonesha mshikamano na ushirikiano walionao watanzania
wote bila kujali tofauti ya dini, kabila wala maeneo wanayotoka.
(“Kwa hiyo ndugu zangu mna imani ya kikristo
lakini mnatambua waislamu ni ndugu zenu, wote tunajenga nyumba moja, mshikamano
ndio tunu tuliyoachiwa na Baba yetu wa Taifa, leo mmeguswa kuona wenzenu
tunafanya ibada na nyinyi mmeingia kwenye ibada, sasa ibada ya kutoa ni ibada
kubwa sana, sio nchi nyingi katika Afrika zinafanya kitendo hiki, watu
hawaelewi, ni nchi chache sana ambazo imani moja inaunga mkono imani nyingine,
lakini sisi waislamu tunalitambua hili hata toka kipindi ambacho mtume wetu SWA
anapigana kusimika dini hii kwa waumini alipata nusura kwa wakristo”)
Vituo vilivyokabidhiwa
vyakula hivyo ni Charambe Islamic Center, Tasofe Lqadiria, Nur Twarigatu
Lqadiria na Zawiyatul Lqadiria.





