Na Mwamvua Mwinyi,Rufiji
...........................................................
MBUNGE wa jimbo la Rufiji,Mohammed
Mchengelwa,amemuomba waziri mkuu Kassim Majaliwa ,kuangalia uwezekano wa kuivunja
taasisi inayojishughulisha na umwagiliaji na kuendeleza bonde la mto Rufiji(RUBADA)na
kuipokonya majengo na ardhi waliyonayo ili ibakie kwa ajili ya tafiti za
kilimo.
Amesema RUBADA imehodhi
eneo la bonde hilo lenye ukubwa wa heka 500,000 pasipo kuliendeleza hivyo
kuendelea kuwepo haina manufaa kwa wanaRufiji kwa kwasasa.
Aidha Mchengelwa,ameiomba
serikali kushughulikia tatizo la kukatika kwa umeme wilayani hapo ambapo kwa
siku hupata nishati hiyo kwa masaa manne pekee kwa takriban mwaka sasa.
Mbali ya hayo alisema hospital
ya Utete inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa vifaa tiba hali inayosababisha
akinamama wanaokwenda kujifungua kununua vifaa madukani kwa gharama ya zaidi ya
sh. 40,000.
Mbunge huyo aliomba
kutatuliwa kwa changamoto hizo ,wakati wa ziara ya waziri mkuu aliyoifanya sept
26,wilayani Rufiji katika mwendelezo wa ziara yake ya mkoani Pwani.
Mchengelwa alisema bonde la
mto Rufiji lina rutuba ya kuweza kulima kilimo cha aina yoyote ikiwemo pamba
hivyo endapo watawezeshwa hata vijana na jamii wataweza kutumia bonde hilo na
kuinua sekta ya kilimo.
“Bunge lililopita tulipitisha
sheria za tafiti za kilimo na kwa kuwa wa Marekani waliwahi kufanya tafiti
katika bonde la mto huo, miaka ya nyuma na kugundua ni miongoni mwa mabonde
yenye ardhi yenye rutuba kuliko eneo lolote katika afrika,ni vyema likatumiwa
na wananchi kwa maslahi yao”alisema Mchengelwa.
Akizungumzia sekta ya
nishati na madini alisema,inafanya viongozi wilayani hapo kugombana na wananchi
kutokana na kukosa umeme wa uhakika kwani kwasasa wanapata umeme kwa masaa
manne kwa siku takriban mwaka mzima uliopita.
Mchengelwa aliomba
kurekebishwa mitambo iliyopo na kusema anafahamu kuna ufisadi mkubwa
uliotendeka ambapo mitambo ilipekwa mitatu huku inayofanya kazi ni miwili pekee
hali inayosababisha kushindwa kufanya kazi kwa siku nzima.
Kuhusu suala la migogoro ya
wakulima na wafugaji aielezea kuwa linakua
siku hadi siku kwasababu ya baaadhi ya watumishi wa halmashauri,wenyeviti wa
vijiji na watendaji kuchukua rushwa na kuingia idadi ya mifugo ambayo
hairuhusiwi.
Mchengelwa alisema tatizo
la migogoro hiyo ni sugu na kubwa kuliko ni kuchangiwa na viongozi na watendaji
wenyewe kujihusisha kuingiza mifugo hiyo na kupelekea kukua kwa changamoto hiyo.
“Kuna mifugo 200,000 na
uwezo wa ardhi ya Rufiji ni kuwa na mifugo 50,000 pekee,nidhamu ikiboreshwa
kutapatikana idadi ya mifugo inayolingana na wilaya”alisisitiza .
Nae diwani wa Utete,Hawa
Mtopa,alieleza kuwa serikali iwasaidie kupeleka vifaa na kuboresha huduma
katika wodi ya uzazi- hospitali ya Utete.
Alisema akinamama
wanagharamia huduma za uzazi zaidi ya 40,000 kwa kila kitu na ni lazima wanunue
dukani hivyo akinamama wenye maisha ya kawaida kushindwa kumudu gharama hizo.
Hawa alisema hospitali hiyo
imejengwa miaka ya 60 lakini huduma zake ni haba hivyo kusababisha akinamama na
wazee kupata tabu.
Kwa upande wake mkuu wa
wilaya hiyo,Juma Njwayo alisema wilaya imejiwekea mkakati wa kuwaondoa kwenye
uongozi viongozi wa vijiji na watendaji wanaohusika kuingiza mifugo kwenye
maeneo yao.
Akitolea ufafanuzi juu ya
maombi na kero alizotolea taarifa mbunge Mchengelwa,waziri mkuu Kassim
Majaliwa,alisema serikali haiwezi kuvumilia miradi isiyo na tija kama wa
RUBADA.
Alielezea kuwa mapema
kuanzia sasa kutafanyiwa uchunguzi juu ya mradi huo na ambae atabainika kufanya
ubadhilifu atawajibishwa.
Akizungumzia juu ya
migogoro ya wakulima na wafugaji alisema kiongozi ama mtumishi atakayejihusisha
na uingizwaji wa mifugo kiholela achukuliwe hatua na kuondolewa katika uongozi.
Kuhusu umeme Majaliwa ,aliwataka
ananchi wawe watulivu na serikali itamaliza suala hilo kwa kuongeza jenereta
jingine ili kuwepo na umeme wa kutosha.
Alisema tatizo la kukatika kwa
umeme mara kwa mara limetokana na majenereta yanayotumika ni mawili hivyo umeme
unaokuwepo ni mdogo hasa baada ya REA kuongeza vijiji na kusababisha ongezeko la mahitaji ya nishati
hiyo.
Majaliwa alisema serikali imefanya utaratibu kuwa jenereta
lisilofanya kazi lirudishwe kwa mkandarasi aliyoyapeleka ili abadilishe na
kupelekwa jingine.
Waziri mkuu yupo kwenye
ziara yake mkoani Pwani,ambapo alianza septemba 23 wilayani Mafia,septemba 28 anatarajiwa
kuwa wilaya mpya ya Kibiti na atamalizia wilayani Mkuranga.
0 Comments