Random Posts

CCM ZANZIBAR KIMEWATAKA WANACHAMA WAKE KUPUUZA PROPAGANDA ZA VYAMA VYA UPINZANI

caiqts3w8aaprak
Na Is-haka Omar, Zanzibar.
...........................
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka Wanachama wa Chama hicho na wananchi kwa ujumla kupuuza na kudharau propaganda zinazotolewa na baadhi ya Vyama vya Upinzani  kwa lengo la kuwapotezea muda wananchi.

Hayo yalisemwa kwa nyakati tafauti na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai ali Vuai huko Mkoa wa Kusini Pemba, alipokutana na Kuzungumza na Kamati ya Siasa ya Mkoa huo pamoja na Wanachama wa CCM Tawi la Vitongoji.

Naibu Katibu Mkuu alisema Wapinzani wanajua fika kuwa hakuna na wala hakutakua na Uchaguzi Mkuu mwengine  Tanzania bara  na Zanzibar hadi mwaka 2020, na wanachokifanya kwa sasa ni kuendeleza siasa zisizokuwa na maslahi kwa familia maskini za Wazanzibar .

Alieleza kwamba wanasiasa wanatakiwa kuwa wazalendo na kusoma alama za nyakati kwa kufanya siasa zinazowahamasisha wananchi wafanye kazi kwa bidii za kujiletea maendeleo badala ya kuwapotosha.

“Wana CCM na wananchi kwa ujumla tumemaliza Uchaguzi wa marudio na kwa sasa tufanye kazi za kujiongezea kipato na  kujiletea maendeleo huku tukisubiri kufanya siasa katika uchaguzi ujao na sio wakati huu.

Pia tunajua kuwa wapinzani hasa CUF kwa upande wa Zanzibar tumewathibiti kila upande na hawana pakutokea ndio maana wanaangaika kila kona ya dunia kuomba msaada ili kurudi katika ushindani wa kisiasa jambo ambalo haliwezekani kwa sasa .”, alisema Vuai.

Nd. Vuai aliwaomba  Wanachama wa Chama hicho  kutumia Uchaguzi wa ndani unaotarajiwa kufanyika 2017, kwa kupata Viongozi imara wa CCM wenye uwezo  wa kuendeleza Ushindi wa Chama katika Uchaguzi ujao.

Naibu Katibu Mkuu huyo aliwapongeza Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi  Pemba kwa kua karibu na Wananchi katika  utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi kwa kiasi kikubwa ndani ya kipindi kidogo cha Uongozi wao.

Aidha  Vuai aliridhishwa  ukomavu wa kisiasa uliopo kwa wafuasi wa chama hicho Pemba kwa kuendelea  kuwa na Ujasiri wa kuimarisha CCM licha ya kukabiliwa na Changamoto mbali mbali zikiwemo kuharibiwa Mali zao na kufanyiwa fujo za mara kwa mara.

Aliahidi kwa kusema kuwa CCM itaendelea kuwa karibu na wafuasi wake hasa waliopo Pemba ili kujenga mahusiano mema na ukaribu wa uimarisha Chama hicho kwa lengo la kujenga ngome ya ushindi kisiwani humo.

Alitoa  wito kwa Vyomb vya Dola kuendelea kuwa macho na Wanasiasa wenye nia za kufanya vitendo vya uovu kwa kupanga na kutekeleza njama za kuwagawa wananchi kwa kutumia njia za Dini kupitia nyumba za ibada jambo ambalo likiachwa linaloweza kuhatarisha amani ya nchi wakati wowote.

Nd. Vuai alitoa ufafanuzi huo baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa Wanachama wa Chama hicho aliokutana nao katika ziara zake zinazoendea Unguja na Pemba za kukutana na Viongozi na wanachama wa CCM.

Pamoja na hayo aliiomba Serikali kutowafumbia macho watu wanaovunja Katiba na Sheria za nchi kwa makusudi kwa kutumia mbinu chafu na hadaa kwa jamii.