Msimamizi
wa Miradi wa Shirika la Misaada na Maendeleo ya Jamii (CODERT), Edward Saramba
alipokuwa akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu njia
wanazozitumia kuwainua wazazi na vijana wa Mkoa wa Geita ili waache kuwapeleka
watoto walio na umri chini ya miaka 18 kufanya kazi katika maeneo ya
migodi.
Mmoja wa wananchi
waliosaidiwa kupata mradi wa kuku kupitia Mradi wa Uondoaji wa Ajira Hatarishi
na Vitendo vya Ukatili kwa Watoto unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la
Ufaransa (AFD), unaratibiwa na Shirika la Plan International na kutekelezwa katika
Wilaya 3 za Mkoa wa Geita, Shabani Masanja akiongea na waandishi wa habari
(hawapo pichani) kuhusu mradi huo ulivyomsaidia.
....................................................................................................
Shirika
la Misaada na Maendeleo ya Jamii (CODERT) limejipanga kuwasaidia jumla ya
wananchi 7000 wanaoishi katika mazingira magumu Mkoani Geita ili waweze kujikwamua kutoka
katika lindi la umasikini linalowakabili.
Shirika
hilo ni moja ya mashirika yanayoshirikiana na Shirika la Plan International
katika kutekeleza Mradi wa Uondoaji Ajira Hatarishi na Vitendo vya Ukatili kwa
Watoto unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na kuratibiwa na
shirika la plan International kwa kuwapatia wananchi hao vifaa pamoja na elimu
ya ujasiriamali.
Hayo
yamesemwa leo Mkoani Geita na Msimamizi wa Miradi wa shirika hilo, Edward Saramba
alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu njia wanazozitumia kuwainua
wazazi na vijana wa mkoa huo ili waache kuwapeleka watoto walio na umri chini
ya miaka 18 kufanya kazi katika maeneo ya migodi.
Saramba
amesema kuwa mradi huo unaoratibiwa na shirika la Plan International umewasaidia
wananchi wa mkoani Geita kuinua maisha yao kwa kuwasaidia kuunda vikundi vya
kuweka na kukopa pamoja na kuwapatia vifaa mbalimbali vinavyowawezesha
kujipatia vipato ambavyo vinawasaidia kuendesha maisha yao ya kila siku.
“Awamu
ya kwanza ya mradi huu iliisha Novemba 2015 na tulifanikiwa kuwafikia wananchi wenye
mazingira magumu zaidi ya 4000 waishio katika Wilaya za Nyan’ghwale na Geita,
kwa awamu hii tumeongeza wilaya ya Chato hivyo tumejipanga kuwafikia wananchi
7000 tukiamini kuwa kuwasaidia wananchi hao kutapunguza ajira hatarishi kwa
watoto”, alisema Saramba.
Amevitaja
baadhi ya vifaa walivyovitoa kwa wananchi wanaoishi kwenye mazingira magumu
kuwa ni mashine za kujazia upepo magari na pikipiki (compressor), vyerehani,
mabomba ya maji, mizinga ya nyuki, viti na meza kwa mama lishe, kuwapatia wafugaji
kuku pamoja na mbegu za mahindi na mpunga kwa wakulima, zaidi ya hayo waliweza
kufadhili mafunzo ya kutengeneza baiskeli, pikipiki na cherehani.
Kwa
upande wake mmoja wa wananchi waliosaidiwa kupitia Mradi huo, Shabani Masanja
ameyashukuru mashirika hayo kwa sababu kabla ya mradi huo kumfikia alikua na
maisha magumu lakini baada ya kuanza ufugaji wa kuku aliopewa kutoka katika shirika
hilo ameona tofauti kubwa ya maisha.
“Nashukuru
sana mashirika yaliyoniwezesha kwa sababu yameninufaisha, kwa sasa ninaweza
nikauza kuku na mayai vinavyoniwezesha kusomesha watoto wangu, kununua chakula,
nimeweka umeme kwenye nyumba yangu ambao unanisaidia kufanya ufugaji wa kisasa
kwa sababu mwanzoni nilikua nikikuza vifaranga kwa kuwawekea moto lakini sasa
hivi natumia umeme kuwakuza”, alisema Masanja.


0 Comments