Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (kulia) akisalimiana na Afisa Rasilimaliwatu
kutoka Shirika la Umeme Nchini (TANESCO)-
Tanga, Samia Suleman (kushoto) mara baada ya kuwasili kwenye ofisi zake mkoani
Mtwara. Profesa Ntalikwa yupo katika ziara ya siku tatu katika
mkoa wa Mtwara yenye lengo la kukagua shughuli za sekta za nishati na madini.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa akisaini kitabu
cha wageni mara baada ya kuwasili katika
kituo cha kuzalisha umeme cha Mtwara.
Kituo
cha kuzalisha umeme mkoani Mtwara kama
kinavyoonekana pichani.
Meneja
wa kituo cha kuzalisha umeme cha Mtwara, Mhandisi Mkulungwa Chinumba (kulia)
akitoa maelezo juu ya uendeshaji wa kituo hicho kwa Katibu Mkuu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (kushoto)
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (katikati mbele) pamoja na wataalam kutoka Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Shirika la
Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) akiendelea na ziara katika kituo cha kuzalisha umeme cha
Mtwara.
Meneja
wa kituo cha kuzalisha umeme cha Mtwara, Mhandisi Mkulungwa Chinumba (kushoto)
akielezea mitambo ya kuzalisha umeme
inavyofanya kazi katika kituo hicho.
Msimamizi
wa mradi wa ujenzi wa kituo cha kupooza
umeme cha Mtwara, Mhandisi Amon Gamba (kushoto) akielezea maendeleo
ya ujenzi wa kituo hicho kwa Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa ( wa pili kushoto)
Kamishna
Msaidizi wa Madini- Kanda ya Kusini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (kushoto)
akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya
sekta ya madini katika kanda hivyo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Profesa Justin Ntalikwa (kulia) mara Profesa Ntalikwa alipofanya ziara
katika kituo hicho.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (kushoto)
akisalimiana na Meneja Uendeshaji wa Mnazi Bay,
David Chaudronnier (kulia) mara baada ya kuwasili katika kituo hicho.
Msimamizi
wa shughuli za uzalishaji kutoka Mnazi Bay, Kilemo Nyomwa akielezea mikakati ya
uzalishaji wa gesi ya kutosha katika kituo hicho ili kuendana na kasi ya ukuaji wa viwanda katika mkoa wa Mtwara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
Profesa Justin Ntalikwa (mwenye suti nyeusi) pamoja na wageni wengine, akiendelea na ziara katika kituo cha Mnazi Bay
mkoani Mtwara.
...........................................................................................................
Na Greyson Mwase, Mtwara.
Serikali
kwa kushirikiana na kampuni ya Helm
kutoka Ujerumani inatarajia kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea katika
eneo la Msanga Mkuu mkoani Mtwara.
Hayo
yalielezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin
Ntalikwa katika nyakati tofauti katika
ziara ya siku tatu mkoani Mtwara ya
kutembelea maeneo ambayo gesi inazalishwa na kujiridhisha iwapo itatosha katika
uendeshaji wa kiwanda kikubwa cha mbolea kinachotarajiwa kujengwa.
Profesa
Ntalikwa alisema kuwa kutokana na ugunduzi wa gesi nyingi mkoani Mtwara wawekezaji wengi wameanza kuonesha nia ya
kuwekeza katika mkoa huo hususan katika
uanzishwaji wa viwanda vya mbolea na saruji.
Alisema
kiwanda cha mbolea kinachotarajiwa kujengwa, kitahitaji gesi kiasi cha futi za
ujazo trilioni 0.8 kwa kipindi cha miaka 20 na kusisitiza kuwa serikali imejipanga katika kuhakikisha kuwa gesi ya kutosha inazalishwa ili kuendana
na mahitaji ya kiwanda hicho pamoja na matumizi mengine ya majumbani.
Akielezea
uwezo wa kampuni zilizopo Mtwara katika uzalishaji wa gesi ya kutosha, Profesa
Ntwalikwa alifafanua kuwa, kampuni ya Ndovu Resources Limited iliyopo katika
eneo la Ntorya ipo katika programu ya
kuchimba visima ambapo imeshachimba kisima kimoja ambacho kimeweza kutoa kiasi
cha futi za ujazo trilioni 0.15
Aliongeza
kuwa kampuni hiyo ina mpango wa kuchimba kisima cha pili ambacho kitakuwa na
uwezo wa kuzalisha gesi kiasi cha futi za ujazo trilioni 0.9 na kisima cha tatu
kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha gesi kiasi cha futi za ujazo trilioni 1.5
na kuongeza kuwa kisima cha pili kinatarajiwa kukamilika mapema Machi, 2017 na
cha tatu mwezi Juni, 2017.
Aliongeza
kuwa kampuni nyingine ya Maurel & Prom yenye visima vitano imesema kuwa ipo
tayari wakati wowote kuchimba visima vya ziada vya kuzalisha gesi ili kuongeza
wingi wa gesi itakayohitajika katika viwanda mbalimbali ambapo kwa sasa
wanazalisha gesi nyingi hali inayopelekea nyingine kukosa soko.
Akielezea
maandalizi ya ujenzi wa kiwanda hicho,
Profesa Ntalikwa alisema kuwa Serikali
imetenga eneo la Msanga Mkuu lililopo Mtwara lenye ukubwa wa hekta 400
kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho.
Aliongeza
kuwa eneo hili limeshalipiwa fidia pamoja na halmashauri ya Mtwara kuboresha
miundombinu ya barabara kwa kuweka lami
kutoka Mtwara Mjini hadi eneo la kiwanda tayari kwa kukabidhiwa kwa mwekezaji
kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda.











0 Comments