Na Joseph Sabinus, Nottingham University
.......................................................
.......................................................
JUZI
niliandika makala kuonesha kuwa kelele zinazoendelea kuhusu Muswada wa Sheria
ya Huduma za Habari ukizitazama kwa undani utakubaliana nami kuwa ni matokeo ya
kada isiyojiamini.
Tasnia ya
habari hapo nchini haijiamini na hili linaweza kuelezwa ama na miaka mingi ya
kuhangaika kuwa na sheria yao huku zoezi hilo kila mara likikumbwa na sababu
mbalimbali na kuahirishwa au kwa namna wanavyojenga hoja zao.
Hata hivyo
ukiziacha kelele hizo na kuanza kuusoma muswada huu kwa kina na kwa kutafakari
makosa mengi yanayofanywa na vyombo vya habari popote duniani utakubaliana nami
kuwa muswada huu, kama walivyosema pia Tanganyika Law Society na Twaweza, una
mambo mengi mazuri na ni bora zaidi kuliko ile ya awali.
Nilidhani
wanahabari wangeshiriki vyema katika kuboresha yale maeneo yenye changamoto
badala ya kuwaachia watu wa tasnia nyingine. Ni bahati mbaya wadau hawa wamechagua
kuwa wanaharakati zaidi badala ya wanataaluma.
Binafsi
baada ya kuusoma muswada nimebaini masuala makubwa yafuatayo katika hili.
Naomba tushirikiane.
1. Sheria kutosajili
mitandao
Awali nilipomsoma Mbunge Zitto Kabwe
nilistushwa kusikia kuwa sheria hii inalenga kubana hadi mitandao ya kijamii.
Hata hivyo sheria haisomwi kama gazeti.
Wakati Zitto alikuwa akisoma tafsiri ya neno
“media” na kuona limejumuisha mpaka mitandao ya kijamii, ukweli ni kwamba
ukiusoma muswada ule eneo ambalo sheria itahusika nalo kwa maana ya uratibu ni
sekta iitwayo “print media”
Kwa hiyo ni kujidanganya kusema sheria hii
itasajili mitandao ya kijamii na vitu vinavyofanana na hivyo. Badala yake
ukisoma kifungu cha 8(1) unauona ukweli huu.
2.
Habari ni taaluma
Kwangu mimi, sijui
kwa wanahabari wenyewe, muswada huu unaleta kwa mara ya kwanza mfumo madhubuti
wa kuifanya sekta ya habari kuwa taaluma kamili na itakayoheshimika na
kutambuliwa zaidi.
Ukiutazama mfumo
unaopendekezwa wa Bodi ya Ithibati katika ibara ya 10 utaiona “spirit” hii.
Taaluma kuwa taaluma moja ya sifa ni hii. Lazima wanataaluma hiyo wawe na Bodi
inayowasajili kwa viwango vilivyowekwa. Hata hivyo sijapata sababu kwa nini
sifa hazijaanishwa kwa sasa.
3.
Bodi kumilikiwa na wanahabari
Wakati nikiendelea kuusoma muswada huu pia nilipatwa
na wasiwasi kuhusu kuundwa kwa Bodi hiyo ya Ithibati nikidhani ingejaa warasimu
tunaowafahamu siku zote.
Hata hivyo kama kuna jambo lingine la
kuusifu muswada huu ni pamoja na muundo wa Bodi yake. Bodi itakuwa na wajumbe 7
na kati ya hao wanne (4) watakuwa ni wanataaluma ya habari akiwemo mwenyekiti
wa Bodi.
Haya ni mapinduzi makubwa katika uundaji wa
Bodi za kitaaluma ambapo katika maeneo mengine ingezingatiwa tu uwakilishi
labda wa jinsi, umri au taasisi. Katika hili tuwapongeze waliosanifu muundo wa
Bodi hii.
4.
Bara Huru lenye meno
Hapa nianze kwa kusema muswada huu
umechelewa sana na hakuna hoja wala haja ya kusubiri tena. Wananchi wanahitaji
kuhudumiwa na sekta bora zaidi ya habari na kila mmoja wetu anajua umuhimu huu.
Ukisoma kifungu cha 23 na kuangalia majukumu
yale ya Baraza Huru la Habari utakubaliana nami kuwa tunahitaji Baraza hili
Huru kuliko wakati wowote. Hilo Baraza linalotajwa kuwepo ni NGO tu na Serikali
yoyote duniani haiwezi kuendeshwa na NGO.
Baraza linaloundwa humu nimeona litakuwa na
uhuru na haki ya kutunga kanuni za maadili za wanahabari na kuhakikisha wenyewe
wanazielewa katika kuwasimamia kwenye kazi zao. Hii ni muhimu sana.
Ukienda Mahakamani inachukua miaka. Ukienda
MCT ya sasa hata wakitoa uamuzi chombo cha habari kinakuwa na uhuru wa kuukataa
au kuukubali uamuzi huo. Baraza hili kwa kuwa limeanzishwa kisheria na lina
nguvu za kisheria litakuwa na uwezo wa kusimamia hata utekelezaji wa hukumu
zake.
5.
Wanahabari kutunga
kanuni zao
Katika hili niseme
tu kwamba kama kuna jambo wanahabari wamekuwa wakilikosa kwa muda sasa ni
kwanza kuwa na chombo kimoja kinachowaunganisha bila kuwabagua zaidi ya wao tu
kuwa wanahabari.
Katika Baraza
linaloanzishwa nimeona vifungu kuwa litakuwa na kazi nyingine muhimu na ya
kipekee (exclussive rights) ya kuandaa kanuni za maadili (media code of
ethics). Hii ni muhimu kwa sababu badala ya kutungiwa na watu wengine ni
wanahabari wenyewe watakaozitunga kwa sababu pia wanafahamu vyema kazi yao.
6.
Kamati ya malalamiko
Kumekuwa na fikra
miongoni mwa watu kuwa kuipata haki mahakamani ni gharama kubwa sana na
inayochukua muda mrefu. Katikati ya keleleza za baadhi ya watu kuwa sheria hii
haina jema, ni muhimu kuona umuhimu wa kifungu hiki.
Kwa kuanzishwa
Kamati ya Malalamiko chini ya Baraza Huru la Habari, sasa wananchi watapata pa
kulalamikia na tena penye meno. Lazima tukubali kuwa ama kwa ajenda fulani au
makosa ya kibinadamu, vyombo vya habari nchini vinawakosea sana watu binafsi au
taasisi.
Naamini ni vyema
kuwapa wahusika mahala pa kulalamika kwa sababu kwenda Mahakamani ni suala
ambalo kila mmoja, kwa sababu tulizokwishaeleza, asingependa kulichagua. Kamati
hii basi ikiundwa itoe uamuzi kwa haraka na iwe madhubuti.
7.
Bima ya Afya
Mwezi Novemba mwaka
jana nilirejea nchini kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka. Katika pita pita zangu
jijini Dar es Salaam nilikutana na matukio mawili ya wanahabari kuchangiwa na
wenzao.
Nilipofuatilia suala
hili nikaambiwa kuwa wanahabari hao hawakuwa na bima na walipopatwa na maradhi
ya muda mrefu ikawalazimu kuishi na kupata tiba kupitia michango ya kujitolea
ya wanataaluma wenzao.
Wapo pia waandishi ambao hadi sasa wako hai
lakini wanaishi kwa kutegemea misaada ya ndugu na jamaa kwa ajili ya kupata
huduma za afya. Nauona muswada huu unakuja kuwakomboa wanahabari. Ni muswada
unaokuja kuhakikisha kuwa si tu wanataaluma hii wanafanya kazi zao kwa ufasaha
lakini pia waweze kupata haki yao ya matibabu na kuwekewa hifadhi ya jamii.
Iliniuma na leo
tunapoona katika kifungu cha 58 cha muswada huu kuna ulazima kwa wamiliki wa
vyombo vya habari kuwakatia bima watu wao, inashangaza kuona wapo wanahabari
ambao wanadai muswada huu haufai na kutaka urejeshwe nyuma.
8.
Haki za watu
Ukisoma Tamko la
Haki za Binadamu la 1948 utaona msingi wa haki kuwa umebebwa katika dhana ya
haki ya mtu mmoja hukoma pale utekelezaji wa haki hiyo unapoingilia uhuru au
haki ya mtu mwingine.
Nimeviona vifungu
kadhaa vya muswada huu vikiwa na mlengo huu wa kuhakikisha wakati, kwa mfano,
haki ya wanahabari kukusanya na kusambaza habari ikiwa ni muhimu, pia ziko haki
za watu wengine zinazopaswa kulindwa na wanahabari.
Kifungu cha 32
katika hili kwa mfano kinaainisha au kukataza waandishi kuchapisha kashifa na
kuwashushia watu wengine hadhi zao bila sababu (wawe hai au wamekufa). Hii ni
muhimu sana.
9. Usalama wa Nchi
Nikikumbuka jinsi vyombo vya habari
vilivyochangia katika machafuko katika nchi mbalimbali duniani hasa Rwanda
(1994) na Kenya (2007) nashawishika kuchekelea ninapousoma muswada huu.
Ukiacha vifungu vinavyoainisha uchochezi,
nimeguswa zaidi na kifungu cha 55 cha Sheria kinapompa mamlaka Waziri
akijiridhisha kuwa kuna suala linalokwenda kukiuka usalama wa nchi basi achukue
hatua haraka.
Wanaharakati hupinga vifungu kama hivi kwa
hoja za juu juu tu za kutokuwaamini viongozi wanaoweza kupewa madaraka hayo,
lakini uhalisi kwamba mambo haya yameshatokea na kwamba zipo nchi zimeshawahi
kuingia katika umwagaji wa damu kwa vyombo vya habari kuachwa huru watakavyo,
mtu hawezi kubeza kuwekwa kwa vifungu kama hivi.
Lipo pia kosa la
uchochezi ambalo wengi, bila kulitafakari, wanapiga kelele zilizokosa tafakuri.
Unawezaje kuwaacha watu watumie vyombo vya habari kuchochea vurugu, kuhamaisha
uasi na machafuko katika nchi? Kwangu mimi makosa kama haya ni muhimu kwa
usalama wa nchi na ni juu ya kila mmoja kutekeleza sheria.
10.
Kufutwa sheria ya
Magazeti
Mimi nikiwa hapo nyumbani kwa miaka mingi
nimekisikia kilio cha wadau dhidi ya Sheria ya Magazeti, 1976. Sheria hii
tumekua nayo, tumeishi nayo na tulianza kuzeeka nayo lakini kila mwanataaluma
akijua haikuwa sheria nzuri.
Kwamba leo inafutwa ni faraja kwa tasnia na
nilidhani wenzetu wengine badala ya kulaani jambo hili wangeungana nasi
kulishangilia. Kwangu, kama kuna jambo jingine kubwa kwa wanatasnia
kulishangilia ni kufutwa kwa sheria hii ambayo wengine walifikia hatua ya
kuiita “ya kikatili.”
Wakati nikiamini wabunge watakuwa wamefanyiakazi
changamoto nyingine na kuuboresha muswada katika maeneo machache kama vile
kukamatwa mitambo kabla ya uamuzi wa mahakama na kuainishwa viwango vya taaluma,
niwaase wanahabri nchi kuwa katika ulimwengu wa utatuzi wa migogoro; mazungumzo
ni muhimu.
Ni bahati mbaya kwamba katika hili
walichagua kutozungumza na Kamati ya Bunge na wakasusia na hatimaye muswada huu
ukipita utawahusu hata kama wao hawakushiriki kuutunga.
*Mwandishi
wa makala haya amejitambulisha kuwa ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu (PhD)
kwenye Chuo Kikuu cha Nottingham, Uingereza.
0 Comments