Waziri wa Fedha
na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwasilisha hotuba kuhusu ni jinsi gani Tanzania
imejipanga kukabiliana na tatizo la utapiamlo na udumavu wa akili kwa watoto
walio na umri wa chini ya miaka mitano, alipomuwakilisha Makamu wa Rais Mhe.
Samia Suluhu Hassan, Jijini Washington DC, Marekani.
Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, wa kwanza kushoto akisikiliza kwa
makini hotuba ya Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim, katika mkutano uliowahusisha Mawaziri wa Fedha kutoka nchi kadhaa
duniani kama vile Cameroon, Ethiophia, Senegal na Indonesia ambapo rais huyo
aliwataka mawaziri hao wasimamie rasilimali fedha vizuri hasa katika suala la kukabiliana na
changamoto ya utapiamlo na udumavu wa akili kwa watoto waliochini ya umri wa
miaka mitano, mkutano uliofanyika Jijini Washington DC, Marekani.
Rais wa Benki
ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim akimpogeza Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip
Mpango, baada ya kuwasilisha hotuba kwa niaba ya Makamu wa Rais, Mhe. Samia
Suluhu Hassan katika mkutano huo kuhusu watoto kupata lishe bora wakati wa
kuzaliwa na kusisitiza wakinamama wanyonyeshe watoto ipasavyo ili kuondokana na
tatizo kubwa la utapiamlo ambalo mara nyingi huwakumba watoto wanapokuwa wadogo
na kusababisha kupoteza nguvu kazi ya Taifa, Jijini Washington DC.
Rais wa Benki
ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim akiwa na Mawaziri wa Fedha wa Afrika akiwemo na
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philiph Mpango(wa nne kutoka kulia),Jijini
Washington DC.
................................................................................................................................
Benny Mwaipaja,
MoFP
Washington DC
7.10.2016
MAKAMU wa Rais
Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo
kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha ili kutatua changamoto ya utapiamlo na udumavu
wa akili kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano kwenye nchi masikini na
zinazoendelea ili kujenga kizazi chenye afya kwa maendeleo endelevu ya mataifa
hayo.
Makamu wa Rais
ametoa wito huo Mjini Washington Marekani kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba
yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, wakati wa mkutano
ulioandaliwa na Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Kim, ulioshirikisha mawaziri wa
Fedha na wadau wengine kutoka nchi zaidi ya 180 wanaoshiriki mkutano wa Mwaka
wa Benki hiyo na Shirika la Fedha Duniani-IMF
Amesema kuwa licha
ya Tanzania kufanikiwa kupunguza utapiamlo na kiwango cha udumavu kwa watoto
walio na umri wa chini ya miaka 5 kutoka asilimia 42 hadi kufikia asilimia 34,
bado idadi kubwa ya watoto wanaokadiriwa kufikia milioni 2.7 wamedumaa akili
huku wengine laki sita wakikabiliwa na utapiamlo mkali.
Mhe. Samia Suluhu
Hassan amesema kuwa kwa kutambua changamoto hiyo, serikali imepanga kutumia
kiasi cha dola Milioni 115 sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 254 kukabiliana na
tatizo hilo katika kipindi cha miaka mitano kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo
wa Taifa wa miaka Mitano, kuanzia mwaka 2016/2021
Ameitaka jumuiya
ya Kimataifa kuunga mkono juhudi za mataifa masikini na zinazoendelea ili
kuwaokoa mamilioni ya watoto wanaokabiliwa na tatizo hilo hivyo kuathiri mustakabali
wa watoto kielimu na kimaisha.
Kwa upande wake
Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Kim, amesema kuwa asilimia 43 ya watoto
waliochini ya umri wa miaka mitano wanaokadiriwa kufikia milioni 250 katika
nchi zenye kipato cha chini na cha kati wamedumaa na kukabiliwa na utapiamlo
mkali unaoletelezwa na umasikini pamoja na ukosefu wa elimu kuhusu umuhimu wa
kuwapatia watoto lishe bora na unyonyeshaji wa maziwa ya mama,
Ameahidi kuwa Benki
hiyo itatenga fedha kupitia miradi mbalimbai inayotekelezwa kwa ufadhili wake
na kushirikisha sekta binafsi ili lengo la kunusuru watoto katika hali hiyo ya
utapiamlo na udumavu wa akili liweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Ameyataka Mataifa
kuwekeza fedha katika ujenzi wa miundombini ya sekta ya afya, elimu, maji, na
usalama wa chakula, kuwajali na kuwapenda watoto ili malengo ya kukomesha
tatizo hilo yafikiwe kama yalivyopangwa.




