
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
...........................
...........................
Kati
ya mafanikio makubwa ya Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa
Awamu ya Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kujenga umoja wa
taifa kati ya watu wa makabila na dini tofauti, na hivyo kudumisha
amani ya muda mrefu tofauti na hali ya nchi nyingi za jirani na hiyo
imeifanya Tanzana iitwe “Kisiwa cha Amani”.
Mwl.
Nyerere amepanua wigo wa siasa ya Tanzania na mataifa ya nje ambapo
ameimarisha uhusiano, ushirikiano na kuunga mkono vyama halisi vya
Ukombozi wa Afrika kama vile FRELIMO ya Msumbiji, ZANU-PF ya Zimbabwe,
ANC ya Afrika Kusini na MPLA ya Angola bila kusahau SWAPO ya Namibia
pamoja na mataifa yaliyopo mabara ya Ulaya, Amerika na Asia.
‘Tukiimarisha
kushirikiana kwetu, tukielewa kuwa vita vyao ni vita vyetu, tutaongeza
sana nguvu zetu za kuleta ukombozi wa Afrika nzima’ anasema Mwl.
Nyerere.
Katika
nukuu za Mwl. Nyerere, amewahi kusema “Uhuru wetu hauwezi kuwa kamili
kama jirani zetu hawajapata uhuru.” Hii inadhihirisha jinsi gani muasisi
huyu wa Tanzania alivyokuwa na dhamira ya dhati ya kushirikiana na
mataifa mengine ya kiafrika.
Katika
Azimio la Arusha Mwl. Nyerere amewahi kusema Tanzania iko tayari
kushirikiana kirafiki na nchi yoyote yenye nia njema bila kujali kama
nchi hiyo ni ya upande wa Mashariki, kwa maana ya nchi zenye mlengo wa
Kijamaa au Kikomunisti au Magharibi, zenye mwelekeo wa kibepari.
Aidha,
Mwl. Nyerere amesisitiza juu ya wajibu wa kuimarisha ushirikiano na
kuungana mkono nchi za kimapinduzi za Afrika, kwa vile aliamini kuwa
nchi zote zimo katika jahazi moja, yenye safari moja, akiwa na maana ya
mazingira na hali za kufanana za nchi hizo.
Katika
kipindi cha Utawala wake wa Awamu ya Kwanza na hata baadae Mwl. Nyerere
ameshiriki katika jitihada mbalimbali za kusaidia mataifa ya kiafrika
kujipatia Uhuru wake, pamoja na kutatua migogoro iliyokuwepo katika nchi
hizo. Amekuwa Mwenyekiti wa nchi zilizokuwa mstari wa mbele katika
ukombozi wa Afrika pia amekuwa msuluhishi wa migogoro ya Burundi.
Hali hiyo imesaidia Tanzania kuwa nchi yenye mahusino mema na nchi mbalimbali duniani bila kujali itikadi zao wala miongozo yao.
Kutokana
mchango na jitihada za Mwl. Nyerere, Tanzania imekua kivutio cha wageni
wengi kutoka nje, kuanzia wanasiasa wa kimataifa na wasomi kutoka
Marekani, Ulaya Magharibu na kwingineko.
Wasomi
hao wa Kimataifa kutoka maeneo mbalimbali walikuja kujionea na
kufanya utafiti juu ya sera ya Tanzania siri iliyomwezesha Mwl. Nyerere
kuiweka Tanzania katika ramani ya Dunia.
“Pembuzi
zao nyingi zilimwelezea Mwl. Nyerere kama “Roho ya Afrika na tumaini
la wasomi, wanasiasa wa Afrika na Dunia nzima”, kila neno lake lina
thamani kubwa, lenye kupimwa na kuchanganuliwa kwa makini na nchi za
Magharibi na za Mashariki.
Kitendo
hicho cha jamii ya kimataifa kumfananisha Mwl. Nyerere na wafalme wa
nchi za ustaarabu wa kwanza Duniani, kama Julius Ceasar, Suleimani na
Richard wa II, ni uthibitisho tosha kwamba kipaji chake kilivutia wengi.
Baadhi
ya viongozi waliofurahishwa na uwezo wa Mwl. Nyerere ni pamoja na Rais
wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter ambaye mwaka 1977 alimsifia na
kumwelezea Mwl. Nyerere kama “ Rais Mwandamizi, msomi, mwanafalsafa
aliyetukuka na mwandishi mahiri”.
Imewahi
kuelezwa kuwa Rais Carter alichukua daftari (notebook) na kuandika kila
kitu alichokuwa akisema Mwl. Nyerere na baadae gazeti moja nchini humo
liliandika “Inapotokea Rais wa Taifa kubwa kumnukuu Rais wa Kiafrika”
inaonesha ni jinsi gani busara ya Mwl. Nyerere ilivyoheshimika na
mataifa makubwa.
Mwl.
Nyerere ameimarisha mahusiano baina ya nchi kadhaa na Tanzania katika
harakati za ukombozi wa nchi hizo na uhusiano huo umezaa matunda ambayo
ni msaada katika kukuza uchumi wa nchi husika pamoja na kuchangia
maendeleo kwa kutoa fursa mbalimbali ikiwemo ajira, masuala ya
kidiplomasia ama utatuzi wa migogoro, sekta za viwanda, afya, kilimo,
elimu, teknolojia na biashara.
Mchango
wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika
ambazo bado zilikua zikikaliwa kimabavu na wakoloni katika nchi za
Zimbabwe, Msumbiji , Angola, Namibia na Zimbabwe zimeimarisha uhusiano
kati ya nchi hizo na Tanzania.
Kuwapatia
hifadhi salama vyama vya ukombozi vya mataifa, pamoja na rafiki wa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Dr. Kenneth David Kaunda (aliyekuwa
rais wa Zambia) ulisaidia jitihada za kuikomboa Afrika hususani Kusini
mwa Afrika.
Aidha,
kupitia uhusiano uliojengwa wakati huo kati ya Mwl. Nyerere na
Kenneth Kaunda ulifanikisha azma ya biashara ya nchi ya Zambia
iliyokuwa ikiuza shaba kwa kiwango kikubwa katika nchi za China,
Ujerumani na kwingineko kwa kujenga reli ya TAZARA kutokana na
ufadhili wa Serikali ya China kutoka Dar es Salaam hadi ukanda wa shaba
nchini Zambia.
Reli
hiyo ni mradi mkubwa wa kwanza kufanywa na China nje ya mipaka yao,
lakini pia ndiyo reli bora zaidi kujengwa Duniani baada ya Vita Kuu ya
Pili ya Dunia.
Mwl.
Nyerere hakuishia Afrika pekee, ameimarisha mahusiano baina ya Tanzania
na China ambayo kwa hakika yamekua yakileta faida kubwa kwa nchi zote
mbili.
Ni
kutokana na mahusiano hayo mema kati ya Tanzania na China, ndio kumezaa
matunda yaliyochangia juhudi zilizofanywa na Meya wa Mji wa Musoma
Bw. Kisusura Malima na aliyekuwa Balozi Mdogo wa China nchini Li
Xuhang alipokuwa mkoani Mara kuadhimisha miaka 50 ya Urafiki wa
Tanzania na China.
Juhudi
hizo ni katika kuwaenzi wanamapinduzi, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere na muasisi wa Taifa la China, Mao Zedong, kwa
kuunganisha mji wa Musoma kilipo kijiji cha Butiama alipozaliwa Mwalimu
na Jiji la Xiang Tan nyumbani kwa Mao mwasisi wa China.
Miji hiyo inaungana kuifanya Butiama na Mara kuwa kivutio cha utalii, uwekezaji kibiashara na kitaaluma kwa kushirikiana Xiang Tan jiji lenye maendeleo makubwa.
Mahusiano
mazuri ya Mwl. Nyerere yalishamiri pia katika taasisi mbalimbali
duniani, kwa mfano Robert Mac Namara, Rais wa zamani wa Benki ya dunia
aliita Tanzania “kipenzi” chake cha Afrika.
Naye,
Gavana Jerry Brown wa Marekani alipotembelea Tanzania, alikaa juu ya
magoti ya Mwl. Nyerere kwa kile alichosema “aweze kujifunza maajabu ya
bara la Afrika kutoka kwa bingwa wa masuala ya Afrika na Dunia”.
Ikumbukwe
kuwa Mwl. Nyerere amekuwa na ushawishi mkubwa na alitoa wazo la
kuunda mashirika mbalimbali yanayoziunganisha nchi za Afrika ikiwa ni
hatua mojawapo ya kuelekea kuunda Afrika moja, hivyo mashirika kama
vile SADC, ECOWAS, COMESA, EAC na kadhalika yaliundwa katika kufikia
azma ya kuunganisha nchi za Afrika, na hivyo mashirika hayo yamekua
yakiendelelea kufanya kazi hadi sasa.
Ni
dhahiri kuwa Tanzania imendelea kuaminika na kuwa kinara katika
masuala ya diplomasia na amani duniani kote na kuifanya kuwa na
mahusiano yaliyoimarika katika nchi mbalimbali . Na hiyo ikiwa ni
juhudi zilizofanywa na Mwl. Nyerere wakati wa utawala wake na hata
baada.
Hakika mchango wake wa kukuza uhusiano wa Kimataifa na Tanzania utakumbukwa vizazi hadi vizazi.
0 Comments