Warda akiendea na kazi katika ofisi za TDL jijini Dar es Salaam.
.............................................................................................................
“Elimu ni ufunguo wa maisha na kumpatia elimu mwanamke ni kuelimisha taifa
zima.Pamoja na ukweli wa msemo huu wanawake wengi hususani katika nchi
zinazoendelea ikiwemo Tanzania bado wamebaki nyuma kielimu ikiwemo kupatiwa
nafasi za uongozi zenye kutoa maamuzi”.Anasema Warda Kimaro,Meneja Chapa (Brand
Manager) wa vinywaji wa kampuni ya Tanzania Distillers Limited (TDL),kampuni
tanzu ya TBL Group.
Kuondokana
na changamoto ya kubaki nyuma anashauri wanawake kupambana kusoma kwa bidii na wanapopata fursa kuzitumia
vizuri ili kuondoa dhana kuwa wanawake hawana uwezo au wanahitaji upendeleo
maalumu katika kushika nafasi mbalimbali
za kazi ama uongozi.
Katika mahojiano hivi karibuni Warda Kimaro,
alisema kuwa anajivunia kuajiriwa na kampuni kubwa kama TDL ambapo amepatiwa
nafasi inayomuwezesha kutoa maamuzi na amekuwa akitoa mawazo mbalimbali na
yamekuwa yakiheshimiwa bila kujali jinsia yake na umri wake.
Akiwa
ni msomi mwenye taaluma ya Masoko kutoka Chuo Kikuu cha Southhampton
Solent kilichopo nchini Uingereza na mwanafunzi wa mwaka wa mwisho wa shahada ya uzamili katika
Utawala na Uendeshaji Biashara (MBA) kutoka
chuo cha ESAMI anasema kwa sasa ni miongoni mwa wanafunzi wanaopata mafunzo ya
kumjengea mwanamke nafasi ya kiutawala katika progamu inaojulikana kama
‘Mwanamke Wa Wakati Ujao’ au kitaalamu kama Female Future Progamme.
Alisema
mafunzo haya yanayotolewa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana
na taasisi ya Confederation of Norwegian Enterprises katika taasisi ya ESAMI ni ya aina yake kwa kuwa yanawezesha kupata
maarifa ya masuala mbalimbali hususani utawala
na jinsi ya kushiriki na kutoa mawazo kwenye vikao vya bodi.
Aliongeza kuwa Programu za aina hii ni nzuri
hususani kwa wanawake kwa kuwa mafunzo yanayotolewa yanaongeza uwezo wa kujiamini na
kuna haja ya kuwa na programu nyingi za aina hii ili ziwafikie wanawake wengi
popote walipo nchini.
“Ili wanawake wengi kutobaki nyuma silaha
pekee ya kuwakwamua ni elimu na ninaposema elimu simaanishi kupata shahada za juu bali ni kujifunza mambo
mbalimbali na kupata maarifa na kuungana na kushirikiana ambapo watapata fursa ya kubadilishana uzoefu
wa masuala mbalimbali,kupeana moyo na kupanga mikakati ya kutatua changamoto
zinazowakabili”.Alisema.
Aliishukuru kampuni ya TDL kwa kumpatia fursa
ya kupata mafunzo haya na anavutiwa
mkakati wa kampuni hiyo kupitia programu yake ya TBL Women’s Forum (TWF)
kwa kuwapatia nafasi za uongozi wanawake katika vitengo mbalimbali ambapo
wanaendelea kufanya vizuri na kudhihirisha kuwa ujuzi hauna jinsia.
“Najua
zipo changamoto nyingi zinatukabili kama wanawake lakini vichwani mwetu tuondoe
dhana kuwa tunapaswa kuwa nyuma ya wanaume kwa kila jambo,tukiondokana na dhana
hiyo tutaweza kusonga mbele na ipo mifano ya wanawake hapa nchini wanaendelea
kung’ara katika nafasi zao za kazi kuzidi hata wanaume na kufanya kwao vizuri
kunatokana na elimu walionayo na kujiamini”.Alisisitiza.
Akiongea juu ya Progamu hii,Bi.Lilian Machera
kutoka Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) ambaye anairatibu alisema hii ni
programu ambayo dhumuni lake ni
kuwajengea uwezo wanawake kushika nafasi za uongozi. “Utafiti tuliofanya umebainisha kuwa ni wanawake asilimia 35% ndio
wanashikilia nafasi za uongozi wakati wanaume wanashikilia asilimia 65%.
Alisema mtaala wa mafunzo haya umejikiza zaidi
katika masuala ya utawala,jinsi ya kutoa michango ya mawazo kwa ufasaha kwenye
vikao vya juu vya bodi za makampuni,kuongea mbele ya watu kwa ufasaha,kujiamini
katika kazi na kwenye kutoa maamuzi sahihi,jinsi ya kujenga hoja sahihi kwenye
vikao,uchambuzi wa ripoti mbalimbali kwa haraka na mengineyo mengi.
Mratibu mwenza wa Programu hii kutoka taasisi
ya Confederation of Norwegian Enterprises
(NHO), Ms Mavie Bordvik, amesema mpango wa mafunzo haya tayari
umenufaisha wanawake zaidi ya 200 katika nchi ulipoanzia zikiwemo nchi za
Nigeria,Kenya na Uganda.
Alitoa wito kwa wanawake wote wa Tanzania
kuamka na kuchangamkia fursa za kujiendeleza zinapojitokeza na kuachana na
mawazo ya kujiona wanyonge mbele ya wanaume.
