Na: Mwandishi wetu Dar es Salaam.
......................................................
Wadadisi
au wakusanyaji taarifa za kitakwimu rasmi katika tafiti mbalimbali
zinazoratibiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wametakiwa kuwa
wamehitimu Mafunzo ya Ukusanyaji Takwimu Rasmi angalau kwa ngazi ya
cheti.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu
wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa imesema matakwa hayo ni
kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Na. 9 ya mwaka 2015 inayoipa mamlaka
ofisi hiyo ya kuratibu na kusimamia ukusanyaji wa Takwimu rasmi nchini.
Taarifa
hiyo imefafanua kuwa utumiaji wa wadadisi ambao wamepitia mafunzo ya
ukusanyaji takwimu angalau kwa ngazi ya cheti kutasaidia kuboresha zaidi
upatikanaji wa takwimu rasmi nchini.
Aidha,
taarifa hiyo imeeleza kuwa Mafunzo ya Ukusanyaji Takwimu Rasmi
yanatolewa na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika "Eastern Africa
Statistical Training Centre (EASTC) kilichopo Changanyikeni jijini Dar
es Salaam.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu ina jukumu
la kukusanya, kuchambua na kusambaza Takwimu Rasmi Nchini kwa mujibu wa
Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.
