Mkuu
wa Kikosi cha kutuliza Ghasia mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa
Polisi (SSP) Ramadhani Giro akiwa anaonyesha burungutu la madawa ya
kulevya aina ya bhangi ambalo lilikuwa limehifadhiwa kwenye moja ya
magunia yaliyopatikana katika kijiji cha Kismiri Juu wilayani Arumeru.
(Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Mkuu
wa Operesheni mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) James
Manyama akiwa ameshikilia ndoo lenye mbegu za mmea wa bhangi mara baada
ya operesheni iliyofanywa na jeshi la Polisi kijiji cha Kismiri wilayani
Arumeru kumalizika.
Mmoja
wa askari wa Jeshi la Polisi akiwa anaendelea na zoezi uchomaji wa
bhangi katika kijiji cha Kismiri Juu, wilayani Arumeru wakati wa
operesheni iliyofanyika katika eneo hilo.
Askari
wa Jeshi la Polisi wakivusha moja ya gunia la bhangi lililofichwa
katika korongo wakati wa operesheni ya bhangi iliyofanyika kijiji cha
Kismiri wilayani Arumeru.
......................................................................................................................
Na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa lipo kwenye mkakati wa
kuwachukulia hatua viongozi wote wanaoishi au kufanyia kazi katika maeneo
ambayo yatabainika wananchi wa maeneo yao wanalima bhangi bila wao kuwachukulia
hatua zozote au kutoa taarifa kwa vyombo husika.
Hayo yameelezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu
kamishna (DCP) Charles Mkumbo alipokuwa anaongea na waandishi wa habari ofisini
kwake baada ya operesheni iliyofanyika katikati ya wiki iliyopita katika kijiji
cha Kismiri Juu, kata ya Uwiro tarafa ya King’ori wilayani Arumeru,
“Mara kadhaa tunapofanya operesheni hizo wananchi wa eneo
hilo huwa wanakimbia na kuacha nyumba zao huku viongozi wao kutoonekana kabisa
au kutoa taarifa zozote juu ya uhalifu huo, sasa tutawachukulia hatua kwani wao
ni sehemu ya uwajibikaji katika kuzuia vitendo vya uhalifu”. Alisema Kamanda
Mkumbo.
Katika operesheni hiyo, jeshi la Polisi lilifanikiwa kupata
jumla ya magunia 22 ya bhangi yaliyokuwa yamehifadhiwa katika nyumba za wakazi
hao na kwenye makorongo yanayozunguka kijiji hicho pamoja na kilogramu 80 za
mbegu za mmea huo ambazo zote ziliharibiwa kwa kuchomwa moto.
Kamanda Mkumbo aliendelea kueleza kwamba, katika operesheni
hiyo pia walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja aitwaye Raphael Laizer (33)
mkazi wa Kismiri Juu akiwa na magunia matatu ya bhangi huku taratibu za
kumfikisha mahakamani zikiwa zinaendelea.
Kamanda Mkumbo aliongeza kwa
kusema kwamba, imekuwa vigumu kuwakamata watuhumiwa kutokana na jiografia ya eneo hilo ambapo kila kunapokuwa
na operesheni askari wanapokwenda, wananchi hao wanawaona kirahisi au kusikia
miungurumo ya gari na kisha hukimbilia milimani na kuwaacha wazee na watoto.
“Japokuwa operesheni hizo ambazo tunazifanya mara kwa mara
zimekuwa za mafanikio lakini changamoto zilizopo ni pamoja na miundo mbinu ya
eneo hilo si rafiki kwa magari hasa uwepo wa milima mirefu na ubovu wa
barabara”. Alifafanua Kamanda Mkumbo.
Operesheni hiyo iliyofanyika kuanzia saa 12:00 asubuhi mpaka
saa 7:30 mchana ilijumuisha askari wa vikosi na vitengo mbalimbali huku
ikisimamiwa na Mkuu wa Operesheni mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)
James Manyama.




0 Comments