Mkuu
wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa
Polisi Happyness Temu akisisitiza jambo kwa wanafunzi wa shule ya Msingi
Sombetini wakati anatoa elimu juu ya Ukatili dhidi ya Watoto kushoto
kwake ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Evelyn Simalenga.
(Picha na Rashid
Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Wanafunzi
wa Shule ya Msingi Sombetini iliyopo jijini Arusha wakishangilia mara
baada ya kupata elimu ya Ukatili dhidi ya Watoto iliyotolewa na kitengo
cha Dawati la Jinsia na watoto la mkoani hapa.
Askari
Polisi kutoka kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Arusha
Happy Mshana akiwaelezea wanafunzi wa shule ya Msingi Sombetini iliyopo
jijini hapa aina za Ukatili dhidi ya Watoto huku wanafunzi hao
wakionekana kumsikiliza kwa umakini.
Mwanafunzi
wa darasa la sita Shule ya Msingi Sombetini Jackson Mutalemwa akiuliza
swali baada ya kupata elimu ya Ukatili dhidi ya watoto kutoka Ofisi ya
Dawati la Jinsia na watoto mkoani hapa
...............................................................................................................
Na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa kupitia kitengo chake cha Dawati
la Jinsia na Watoto limeanza kutembelea shule za Msingi kwa nia ya kutoa elimu
ya Ukatili dhidi ya watoto. Hayo yameelezwa na Mkuu wa kitengo hicho Mkaguzi wa
Polisi Happyness Temu wakati alipokuwa anatoa elimu kwa wanafunzi wa shule ya
Msingi Sombetini iliyopo halmashauri ya jiji la Arusha.
Alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakipokea malalamiko
mbalimbali ya wanawake, wanaume na watoto wakiwa ofisini lakini wamegundua
kwamba wanafunzi wengi wa shule za Msingi hawana uelewa juu ya vitendo vya Ukatili
unaotokea miongoni mwao.
Akitoa elimu hiyo kwa wanafunzi hao Mkuu huyo wa Dawati
alisema kwamba baadhi ya watoto wanafanyiwa vitendo vya ukatili kwa kubakwa na
kulawitiwa lakini ukaa kimya na wasijue nani wa kumwambia, hivyo kuwataka pindi
wanapoona dalili za watu kutaka kuwafanyia vitendo vya aina hii watoe taarifa
haraka kwa wazazi wao, majirani au walimu.
Alisema kumekuwa na mbinu tofauti tofauti zinazotumiwa na
walaghai kama vile kumnunulia Mwanafunzi pipi, kumpa msaada wa kumpeleka shule
na kumrudisha nyumbani “lift”, kumpa pesa hali ambayo aliwaambia wanafunzi
waikatae kwani sio watu wote wana nia nzuri na wao.
“Mara unapohisi kuna mtu ambaye anasogea karibu yako na
kukudanganya kwa kukupa msaada wa lift au kukunulia pipi unatakiwa kutoa
taarifa mapema kwa wazazi wako, walezi wako, majirani au walimu wako hali
ambayo itasaidia kukuepusha kuingia kwenye matatizo”. Alisisitiza Mkuu huyo wa
Dawati.
Alisema watoto wanaweza wakafanyiwa vitendo hivyo si kwa watu
wa nje na nyumba zao tu bali hata watu wao wa karibu kwa maana ya wazazi au
walezi wao wanaweza kuwafanyia vitendo hivyo, na kuwaeleza kwamba wana nafasi
ya kuwaeleza majirani na walimu wao ambapo taarifa hizo baadae zitawafikia
katika ofisi yao ya Dawati na wao kuchukua hatua mara moja.
Akizungumzia aina mbalimbali za ukatili askari wa kitengo
hicho, Happy Mshana alisema kwamba ukatili upo wa aina tofauti tofauti kama
vile ukatili wa kingono, ukatili wa kijinsia, ukatili wa Kisaikolojia, ukatili
wa kielimu na kadhalika.
Alisema mara nyingi wanafunzi wanaathirika na ukatili wa
kielimu ambapo hali hii inatokana na wazazi au walezi kuwazuia watoto wao
kwenda shule huku wakiwa wanastahili kusoma, hivyo kuwataka pindi wanapoona wao
au wenzao wanakumbwa na hali hii watoe taarifa kwa majirani na ikishindikana
wawaeleze walimu wao.
Kutokana na elimu iliyotolewa na Dawati hilo iliweza kuibua
hisia za wanafunzi mbalimbali ambao wengi waliuliza maswali ambayo yalijibiwa
na askari wa kitengo hicho walioongozwa vyema na Mkuu wa kitengo hicho Mkaguzi
wa Polisi Happyness Temu, huku wengi wao wakionekana kushangilia baada ya mmoja
wao kutaka adhabu ya kunyongwa itumike kwa watuhumiwa wanaokutwa na hatia kwa
makosa ya ubakaji na ulawiti badala ya
kifungo.
Mwanafunzi wa darasa la sita aitwaye Jackson Mutalemwa ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Haki
za Watoto (Children Right Club) alisema
kwamba kitendo cha Dawati kutoa elimu shuleni hapo kimekuja muda muafaka
kutokana na vitendo hivyo kuripotiwa kwenye Klabu yao mara kwa mara hasa
wanavyofanyiwa watoto wa mitaani hivyo kuwataka wasiishie kwenye shule tu bali
wawaelimishe pia watoto wa mitaani
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Evelyn Simalenga alisema
kwamba Dawati la Jinsia na watoto limewafanya wanafunzi wake wawe na uelewa
mpana zaidi hivyo utawafanya wawe makini na kushauri kwamba elimu hiyo iendelee
kutolewa kwa wazazi ili wawe karibu na watoto wao.




0 Comments