Mhariri Msanifu wa Gazeti la Mtanzania, Khamis Mkotya,
akiangalia kisima kilichochimbwa katika Kijiji cha Chandama wilayani Chemba, chini
ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), kikiwa kimepigwa kufuli.
Katikati ni mkazi wa kijiji hicho, Igwana Maulid na Yusuph Kijuu.
Na Mpiga picha
Wetu
......................................................................................
Na Mwandishi Wetu, Chemba
WANANCHI wa Kijiji cha Chandama, Wilaya ya Chemba
mkoani Dodoma, wameshindwa kufanya shughuli za maendeleo, kutokana na
kukabiliwa na tatizo la maji kwa miaka mingi.
Wananchi hao walisema, wanashangaa kuona wanapata shida ya maji,
wakati kuna visima viwili vilivyochimbwa kijijini hapo na vyenye maji mengi,
lakini hawafaidiki navyo kutokana na ukosefu wa miundombinu.
Taarifa hiyo ilitolewa juzi kwa nyakati tofauti na baadhi ya
wakazi wa kijiji hicho, walipokuwa wakizungumza na MTANZANIA.
Kutokana na shida hiyo, wananchi hao wamemwomba Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge, afike kijijini hapo ili aweze kutatua kero
hiyo iliyodumu kwa muda mrefu.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Iddy Ijui, alisema kijiji hicho
kinakabiliwa na shida kubwa ya maji, ambapo hivi sasa wanalazimika kununua pipa
moja la maji kwa Sh 5,000.
“Kitendo cha kukosa maji kinatufanya tushindwe kufanya shughuli za
maendeleo, kwani tunapoteza muda mwingi kutafuta maji.
“Hapa kijijini kuna visima viwili na vyote vina maji mengi, lakini
vimefunikwa na magunia na kingine kimepigwa kufuli tangu 2011, sasa hatuelewi
lengo lao lilikuwa ni kutuachia mashimo au kutoondolea kero ya maji,” alihoji.
Naye Igwana Maulidi, alisema katika kujitafutia huduma hiyo
wananchi wa kijiji hicho wamechimba visima virefu vya kienyeji vinavyotumia
kamba, kiasi cha kuhatarisha usalama wao.
“Visima viwili vimechimbwa lakini havitumiki, hatuwezi kupata maji
kwa sababu havijafungwa mashine. Kibaya zaidi hakuna kiongozi anayezungumzia
hatima ya hivi visima na jitihada za kumaliza hii kero, ndiyo maana tunaomba
waziri wa maji aje hapa kijijini,” alisema.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Mustafa Kidunka maarufu kwa jina
la Munguji, alisema wananchi wa kijiji hicho ni kama yatima, kwani hakuna
kiongozi anayehangaika kutatua kero zao.
“Watu wanashida ya maji hakuna anayejali, kilichimbwa kisima hapa
na wajapani, kimepigwa kufuli hadi leo hakijafunguliwa. Mwaka jana tena
halmashauri ilichimba kisima kingine na chenyewe kimefunikwa tu, kama ni hasara
ya viongozi tumeipata,” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Said Mwaliko
(Chadema), maarufu kwa jina la Machapati, alikiri kuwapo kwa kero hiyo na
kusema uongozi wa juu ndiyo kikwazo cha kumaliza kero hiyo.
“Shida ya maji ni kubwa, watu wanaugua matumbo, mimi nafuatilia
ngazi ya juu nimekuwa nikimpigia simu mbunge, ananiambia linashughulikiwa
lakini sioni chochote na mimi hapa kijijini nasumbuliwa sana kuhusu tatizo la
maji.
“Tukikaa kwenye vikao vya WDC (kamati ya maendeleo ya kata) diwani
anasema suala hili linashughulikiwa mara anasema hela zimetengwa lakini ni muda
mrefu sasa hatuoni chochote na wananchi wanaendelea kupata shida,” alisema
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Chandama, Titus Sindamwaka
(CCM), alipotafutwa kuzungumzia kero hiyo aliwataka wananchi hao kuwa na
subira, kwani kuanzia mwezi ujao tatizo hilo litakuwa limepatiwa ufumbuzi.
“Tumechimba visima viwili kimoja kipo Chandama na kingine kipo
Mapango, tunasubiri bajeti ya Novemba 4, mwaka huu Baraza la Madiwani
litakapokutana tuone tunakiasi gani tuanze kufunga miundombinu,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu kisima kimoja kupigwa kufuli kwa muda mrefu,
Sindamwaka alikiri kisima hicho kuchimbwa 2011 na kueleza kuwa hakiwezi
kufunguliwa, kwani hakijakabidhiwa rasmi katika Serikali ya Kijiji.
