Waziri
wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akipokea maelezo ya ramani ya
mradi wa uchimbaji visima vya Kimbiji na Mpera kutoka kwa Mhandisi Mkazi wa mradi,
Injinia Charles Kaaya.
Mashine
ikiendelea na kazi ya uchimbaji kisima Kimbiji.
Baadhi
ya mafundi wakiwa eneo la kazi Kimbiji.
Waziri
wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akiwa pamoja na Mtendaji Mkuu wa
Kampuni ya Serengeti, Mehrdad Talebi (kushoto), Mhandisi Mkazi wa mradi,
Charles Kaaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es
Salaam (DAWASA), Archad Mutalemwa na Mkurugenzi wa Maji Mijini, Mhandisi Dkt.
Justus Rwetabula
Waziri
wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akionja maji yaliyopatikana
katika kisima namba K17.
Mhandisi
Mkazi wa Mradi wa uchimbaji visima vya Kimbiji na Mpera, Charles Kaaya (kushoto)
akizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Miradi na Ufundi ya Bodi ya DAWASA,
Prof. Felix Mtalo (katikati) na Waziri Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge.
..........................................................................................................
WAZIRI
wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge, ameiagiza Kampuni ya Serengeti
Limited kukamilisha mradi wa uchimbaji visima 20 vya maji vya Kimbiji na Mpera
kwa muda waliokubaliana, vinginevyo itabidi ilipe gharama za ucheleweshaji kama
itashindwa.
Alisema
serikali haitavumilia kuona mradi huo wenye manufaa makubwa kwa Jiji la Dar es
Salaam unachelewa kukamilika, kwa sababu unahitajika kuhudumia wananchi kwa
kuwapatia huduma ya majisafi na salama.
Waziri
Lwenge alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki, baada ya kufanya ziara ya kukagua
utekelezaji wa mradi huo mkubwa uliopo Kigamboni, Dar es Salaam ulioanza
kutekelezwa tangu mwezi Machi, 2013.
Alisema
mradi huo utagaharimu zaidi ya Sh. bilioni 18, na serikali imeshalipa kwa
mkandarasi zaidi ya Sh. bilioni 13, na ulitegemewa kukamilika ifikapo Desemba mwaka
huu, lakini utachelewa kutokana na changamoto mbalimbali alizotaja mkandarasi
huyo.
“Pamoja
na changamoto alizozitaja mkandarasi, hatutakubali utekelezaji wa mradi huu
uendelee kuchelewa, mkandarasi inabidi aongeze kasi ili tumalize kero ya
wananchi wa Kigamboni, Mkuranga na Dar es Salaam yote, ambao kwa muda mrefu
wamekuwa wakisubiri mradi huu, hatutavumilia uchelewaji zaidi na itabidi walipie
gharama endapo watashindwa”, alisema Inj. Lwenge.
Alisema
mradi umetekelezwa kwa asilimia 56 hadi sasa, visima nane vikiwa vimekamilika,
huku vingine saba vikiwa katika hatua mbalimbali za uchimbaji na vitano vikiwa
havijaanzwa kazi ya uchimbaji.
Wakati
huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Serengeti Limited, Mehrdad Talebi
alikiri kuchelewa kukamilika kwa mradi huo kama mkataba unavyosema, kutokana na
changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa vifaa vya kazi na kuahidi ifikapo
Machi, 2017 watakuwa wamekamilisha kazi hiyo.
Aidha,
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA),
Archad Mutalemwa, alisema mradi huo hautakamilika kulingana na makubaliano ya
awali, lakini ana imani na kukamilika kwa kazi hiyo mara baada ya kutatua
changamoto za mkandarasi, ikiwemo kupatikana kwa vifaa vya kazi.
Uchunguzi
wa awali ulionyesha uwepo wa maji mengi na safi katika maeneo ya Kimbiji na
Mpera. Hivyo, ikaamuliwa visima kati ya 20-40 vichimbwa kwenye maeneo hayo na
vinategemwa kuchangia hadi asilimia 30 ya mahitaji ya maji ya Dar es Salaam,
mji unaotarajiwa kuwa na watu wapatao milioni 7.59 ifikapo mwaka 2032.
Ili
kukabiliana na tatizo la maji kati ya sasa na hadi mwaka 2032, visima 12 vitachimbwa
maeneo la Kimbiji na 8 maeneo ya Mpera. Visima hivi vitakuwa na kina cha hadi
mita 600 na vinategemewa kuzalisha lita za ujazo 260,000 kwa siku.





