Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akifafanua jambo kuhusu wananchi waliovamia
msitu wa hifadhi ya Kijiji. Kushoto ni Bi. Veronica Nyasa mkazi wa eneo hilo
ambae amesema yuko tayari kuondoka endapo atapatiwa sehemu mbadala.
Uongozi wa Wilaya ya
Kaliua wakimwonyesha Waziri Makamba magogo ya miti ya asili yanayotumiwa na
wanachi katika kukaushia tumbaku kwa kutumia majiko ya kienyeji
Pichani ni moja ya
majiko ya kienyeji yanayotumia kuni/miti mingi katika kukaushia tumbaku. Waziri
Makamba amewaagiza wakazi wa Kitongoji cha Mtakuja Magharibi kutumia majiko
banifu ili kunusuru ukataji miti kwa wingi husnan ile ya asili
..................................................................................................
Na Lulu Mussa Tabora
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira
hii leo ameendelea na ziara ya kikazi katika Mkoa wa Tabora akitokea Mkoani
Kigoma.
Akiwa Mkoani Tabora Waziri Makamba ametembelea Wilaya ya
Kaliua na kukutana na changamoto kubwa ya Uharibifu wa Mazingira na Uvamizi wa
Misitu unaofanywa na wananchi. Katika Kijiji cha Ufugala Wilaya ya Kaliua
Waziri Makamba amefanya Mkutano wa hadhara kijijini hapo na kubaini kuwa
Kitongoji hicho hakikufuata taratibu za kisheria katika kuanzishwa kwake na
kimeanzishwa ndani ya Hifadhi.
Akitoa maelezo ya Awali Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Bw. Abel
Yeji Busalama amemueleza Waziri kuwa Kitongoji hicho kiko ndani ya Hifadhi ya
Msitu wa Kijiji ambapo jumla ya Vijiji 11 viamua kutenga eneo hilo kwa ajili ya
Hifadhi.
Bw. Busalama amesema kuwa wakazi hao wamekwisha amriwa
kuondoka katika hifadhi hiyo na utekelezaji wake unaendelea.
Akijibu hoja zilizowasilishwa na wakazi wa eneo hilo Waziri
Makamba amesema kuwa wajibu wa Serikali ni kuhakikisha kuwa Sheria, tararibu na
kanuni zinafuatwa bila kukiukwa. Waziri
Makamba pia amesisitiza kuwa maamuzi ya matumizi bora ya ardhi yapo mikononi
mwao. "Ndugu zangu ni nyinyi wenyewe mliamua kutenga eneo hili maalumu kwa
hifadhi ya msitu wa kijiji na kufuata taratibu zote za kisheri katika
kuusajili, maamuzi yenu ya awali yatabaki palepale mpaka mtakapofuata taratibu
nyinginezo." Makamba alisisitiza.
Aidha, Waziri Makamba ameahidi kuwasilisha suala hilo kwa
Wizara ya Maliasili na Utalii na ile ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
ili kupata ufumbuzi wa kudumu. "Nitaongea na Mawaziri wenzangu na kuleta
timu ya wataalumu kupitia upya mipaka ya kijiji na kuifanyia kazi" Makamba
alisisitiza.
Kuhusu hifadhi ya Mazingira Waziri Makamba amewataka wakazi
wa Ufulaga kuacha tabia ya kukata miti ya asili
na kusisitiza kuwa uharibifu wa mazingira unabadilisha tabia za watu.
"Wana Ufulaga, binadamu wakiharibu mazingira kwa kiasi kikubwa wanaanza
wizi na udokozi na wanyama wataanza kuwinda watu kwa kukosa malisho"
alisema Waziri Makamba.
Waziri Makamba pia amefanya ziara katika Wilaya ya Urambo na
kubaini changamoto kubwa ya uvamizi wa misitu na ukataji wa miti ya asili kwa
ajili ya kuni za kukaushia tumbaku.
Waziri ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC) kutumia Sheria ya Mazingira namba 20 ya mwaka 2004 kifungu
namba 196 (1) (a na b) kupiga marufuku ya matumizi ya majiko banifu ya kienyeji
pia ukataji mkubwa wa miti ya asili kwa
ajili ya biashara ya tumbaku.
Katazo hilo litawahusu Wakulima na Vyama vya Msingi vyote
vinavyojishughulisha na biashara ya tumbaku.
Waziri Makamba anaendelea na ziara yake kwa kutembelea Wilaya
za Nzega na Igunga.



0 Comments