Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mofisa wa Magereza wakati
alipotembelea Gereza Kuu la Mkoa wa Dodoma la Isanga mjini Dodoma
Oktoba 5, 2016.
Askari Magereza wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kati
alipowasilimia baada ya kutembelea Gereza Kuu la Mkoa wa Dodoma Isanga
mjini Dodoma Oktoba 5, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Maofisa na Askari Magereza
wa Gereza Kuu la Mkoa wa Dodoma la Isanga baada ya kulitembelea Oktoba
5, 2016. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Taifa wa Parole Augusine Mrema,
kulia kwake ni Mkuu wa mkoa wa Dodoma na aliyekaa kushoto ni Mkuu wa
Magereza wa mkoa wa Dodoma, SACP Kirumbi.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoka kwenye Gereza Kuu la Mkoa wa Dodoma
la Isanga wakati alipolitembelea mjini Dodoma Oktoba 5, 2016.
(Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
.............................................................................................................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw. Jordan
Rugimbana kuchunguza ni kwa nini Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma Bw Antonino
Kilumbi amekwenda kutengeneza madawati kwa watu binafsi badala ya karakana ya Magereza kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Magereza mkoa wa Dodoma ilipewa sh. milioni 24 na Serikali ili kutengeneza
madawati 480 na kila moja lilitakiwa kugharimu sh. 50,000. Uongozi wa gereza
hilo ulitengeneza madawati hayo kwa watu binafsi ambapo dawa moja limegharimu
sh. 70,000.
Waziri Mkuu ametoa kauli
hiyo leo (Jumatano, Oktoba 5, 2016) wakati alipotembelea Gereza la Isanga
mkoani Dodoma akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo yanayotoa huduma za jamii
mjini hapa.
Amesema kama gereza hilo
halikuwa na uwezo wa kutengeneza madawati hayo kwa nini kazi hiyo
wasingeipeleka kwenye taasisi nyingine ya umma, hivyo amemtaka Mkuu wa Mkoa Bw.
Rugimbana kufuatilia ziada ya sh. 20,000 kwenye utengenezaji wa kila dawati
inatoka wapi na inakwenda kwa nani.
“Nimesikia kwamba mnawachangisha askari kiasi kilichoongezeka kwenye
utengenezaji wa madawati hayo. Ni marufuku askari kutoa fedha mifukoni mwao
kulipia shughuli za Serikali,” amesisitiza.
Serikali imeandaa utaratibu
wa kuwezesha taasisi zake zikiwemo za kijeshi kwa kuzipa kazi ya kutengeneza
bidhaa na miundombinu mbalimbali ikiwemo madawati ili kuyaongezea tija
aliongeza
Kwa upande wake Mkuu wa
Magereza Mkoa wa Dodoma Bw. Kilumbi amesema waliamua kupeleka kazi hiyo kwa
watu binafsi kwa sababu hawana vifaa.
Aidha, Waziri Mkuu amemtaka
mkuu huyo wa magereza mkoa kuimarisha kitengo cha ufundi seremala na
kuhakikisha anatumia vizuri nguvu kazi aliyonayo katika kuzalisha bidhaa
mbalimbali.
Kuhusu changamoto ya makazi
kwa askari Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua na imeweka mkakati wa wa
ujenzi na kwa upande wa askari Magereza wataanzia kwa mkoa wa Dodoma.
Wakati huo huo Waziri Mkuu ametembelea maduka ya kuuzia bidhaa mbalimbali
zikiwemo nguo katika maeneo ya soko la Sabasaba na Majengo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATANO, OKTOBA 05, 2016





0 Comments