Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeipiga
faini ya sh. 5,000,000 (milioni tano) klabu ya Simba, kuiagiza ilipe
gharama za uharibifu wa viti uliofanywa na washabiki wake katika mechi
ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya timu yake na Yanga iliyochezwa Oktoba
Mosi mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pia Kamati hiyo katika kikao chake kilichofanyika jana (Oktoba 4,
2016), imelaani kitendo hicho na kuionya klabu hiyo kuwa vitendo vya
aina hiyo vikiendelea itakabiliwa na adhabu kali zaidi ikiwemo kucheza
mechi bila washabiki. Adhabu dhidi ya Simba imetolewa kwa mujibu wa
Kanuni ya 42(3) na 24(7) za Ligi Kuu.
Vilevile kwa kuzingatia Kanuni ya 9(8) ya Ligi Kuu, Kamati imefuta
adhabu ya kadi nyekundu iliyotolewa na mwamuzi wa mechi hiyo kwa Jonas
Mkude wa timu ya Simba baada ya kuthibitika bila mashaka kuwa nahodha
huyo hakustahili kadi hiyo.
Mbali ya ripoti ya Kamishna na kupitia tena mkanda wa mechi hiyo
iliyoonyeshwa 'live', Kamati inaendelea na uchunguzi wa jambo lingine
kuhusu uchezeshaji wa mwamuzi wa mechi hiyo Martin Saanya, na wasaidizi
wake Samwel Mpenzu na Ferdinand Chacha kabla ya kutangaza uamuzi wake.
Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara amepigwa
faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kuingia uwanjani baada ya mechi
hiyo wakati yeye hakuwa miongoni mwa maofisa wa mechi waliotakiwa kuwepo
katika eneo hilo.
Adhabu dhidi ya Manara ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(10). Eneo husika
ni kwa ajili ya wachezaji, mabenchi ya ufundi, waamuzi, madaktari,
huduma ya kwanza, wapiga picha na maofisa wengine wa mechi.
Klabu ya Azam imepigwa faini ya sh. 3,000,000 (milioni tatu) kwa
kuvaa nembo ya mdhamini wa Ligi Kuu kwenye mkono mmoja tu badala ya
miwili ambapo ni kinyume na Kanuni ya 13(1), na adhabu hiyo imetolewa
kwa mujibu wa Kanuni ya 13(6).
JKT Ruvu imepewa onyo na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano)
baada ya Msimamizi wa Kituo, na Ofisa wa Bodi ya Ligi kushambuliwa na
mshabiki wa timu hiyo katika mechi dhidi ya Mbeya City iliyofanyika
Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. Mshabiki huyo amefungiwa
miezi 12, na iwapo vitendo hicho vitaendelea Uwanja huo utafungiwa kwa
mechi za Ligi Kuu.
Mwamuzi Ahmed Seif amefungiwa miezi sita kwa kushindwa kumudu mechi
kati ya African Lyon na Mbao FC ikiwemo kutoa adhabu ya penalti ambayo
haikuwa sahihi. Pia Mwamuzi huyo alipata alama za chini ambazo
hazimruhusu kuendelea kuchezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.
Pia Makamisha David Lugenge na Godbless Kimaro wamepewa onyo kwa
kuwasilisha taarifa zenye upungufu katika mechi walizosimamia za raundi
ya tano na saba.
Katika Ligi Daraja la Kwanza (FDL),
Mbeya Warriors imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kupitia
mlango usio sahihi ikiwemo kuvunja kufuli kwenye mechi kati yao na
Kimondo FC iliyofanyika Septemba 24 mwaka huu Uwanja Vwawa mkoani
Songwe. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Daraja la
Kwanza.

0 Comments