Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba akijibu hoja mbalimbali za
wabunge katika kikao cha pili cha Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, leo mjini Dodoma.
..........................................................................................
Serikali
imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3 katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018
kwa ajili ya kukarabati, kupanua na kumalizia ujenzi wa mabweni mapya pamoja na
majengo ya utawala katika baadhi ya magereza nchini.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba ameyathibitisha hayo leo mjini
Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mhe. Hawa Mwaifunga (Mbunge wa Viti Maalumu)
lililohoji kuhusu mpango wa Serikali katika kuhakikisha hali za magereza katika
Mkoa wa Tabora zinaboreshwa.
Mhe.
Mwigulu amesema kuwa katika kuhakikisha hali ya magereza nchini inaboreshwa ili
kuhakikisha haki za binadamu zinatekelezwa, Serikali inaendelea na mpango
endelevu wa kufanya upanuzi wa magereza ya zamani na kujenga magereza mapya
katika kila Wilaya ambapo utekelezaji huo unafanyika kulingana na upatikanaji
wa fedha.
“Katika
mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga bilioni 3 katika Bajeti kupitia Fungu la
Maendeleo kwa ajili ya kukarabati magereza ambapo shilingi milioni 185 kati ya
bajeti iliyotengwa ni kwa ajili ya kukarabati magereza ya Mkoa wa Tabora, hivyo
tunategemea magereza ya mkoa huo yatakuwa katika hali nzuri”, amesema Mwigulu.
Ameongeza
kuwa Serikali inatambua msongamano wa mahabusu uliopo katika magereza mengi
nchini na kuongeza kuwa Jukwaa la Haki Jinai limekuwa likifanya vikao vya
kuharakisha kesi ambazo upelelezi wake haujakamilika ili kupunguza msongamano
huo.
Aidha,
Waziri Mwigulu amesema kuwa Serikali inahakikisha Askari Wapelelezi wanapewa
mafunzo kulingana na kazi yao ili waweze kufanya ukamataji wa watuhumiwa kwa
kuzingatia uzito wa ushahidi wa muhusika na kuepusha malalamiko ya kubambikiwa
kesi na kujikuta Serikali inatumia gharama nyingi kuwatunza mahabusu hao.
Kuhusu
usalama wa askari, Waziri Mwigulu amesema kuwa Serikali itaendelea kuliwezesha
Jeshi la Polisi nchini kwa kuwapa vitendea kazi bora na kuwajengea uwezo wa
mafunzo askari hao ili waweze kukabiliana na matukio ya uhalifu dhidi ya
wanananchi na mali zao pamoja na uvamizi wa vituo vya polisi nchini.
“Hadi
kufikia Septemba 2016 Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata silaha 19 kati ya
23 zilizoporwa kutoka kwa askari waliovamiwa wakiwa wakitekeleza majukumu yao
hatua inayoonesha jeshi la Polisi linavyofanya kazi kwa umakini” alisema
Mwigulu.
Kwa
upande mwingine, Waziri Mwigulu ametoa rai kwa wananchi kutoa taarifa katika vituo
vya Polisi vilivyo karibu pindi wanapokuwa na shaka juu ya watu wasiowatambua au
kufanya kazi zisizoeleweka ili kuwahakikishia wananchi usalama wakati wa
kutekeleza majukumu yao ya kimaendeleo.

0 Comments