Random Posts

MUSWADA WA HABARI UMEZINGATIA WELEDI NA MAADILI

Na Mwandishi wetu
................................................................
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 umezingatia vigezo muhimu anavyopaswa kuwa navyo mwanahabari ikiwemo weledi na maadili katika kutekeleza majukumu yake.

Hayo yamesemwa leo na mwanataaluma mkongwe katika tasnia ya habari nchini Bw. Clement Mshana wakati akitoa tathmini yake kuhusu muswada huo. 
  
Bw. Mshana ameeleza kuwa kutokana na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia hakuna budi kuwa na sheria mpya kwenye tasnia ya habari ili kuendana na mabadiliko hayo bila ya kuathiri maadili na miiko ya tasnia hiyo.

Alisema kuwa makosa mengi ya kihabari yanayojitokeza hufanywa kwa makusudi ili kupotosha jamii kama vile kuandika habari za uongo, hali hii inatokana na watu wasio na sifa kuvamia fani kwa hiyo ni muhimu kuwe na vigezo maalum vya kumtambua mwanahabari.

“Vyombo vya habari vya leo sio vile vya miaka ya nyuma, kuna mabadiliko mengi na wanahabari pia wamekuwa wengi wakiwemo baadhi ambao hawana sifa hivyo ni lazima kuwe na mabadiliko ya sheria na muswada huu umezingatia vigezo vyote vya msingi ili kuleta hadhi na heshima ya taaluma hiyo” alisema Mshana.

Pia Mshana aliongeza kuwa muswada huo una vipengele vya muhimu katika kuboresha maslahi ya wanahabari kama vile fursa za mafunzo, bima na hifadhi ya jamii mambo ambayo yana faida kwao ukizingatia kwamba kazi yao ni nyeti na ina misukosuko mingi.

“Vipengele vya bima na hifadhi ya jamii ni muhimu sana kwani vinalinda maslahi ya wafanyakazi katika tasnia ya habari kwa sababu mara nyingine kazi hii ina hatari lakini wamiliki wengi wa vyombo vya habari wanapenda kufanyiwa kazi bila ya kujali maslahi ya wafanyakazi wao ndio maana wanapinga sheria hii kwa vile itawabana” alifafanua Mshana.   
 
Aidha, Mshana amewataka baadhi ya wadau wa sekta ya habari kuacha kupotosha kwa kuwa muswada huo ni mzuri na wadau walishirikishwa hivyo walipaswa kutoa maoni ya kuboresha badala ya kupinga huku wakitetea maslahi ya watu wachache.   

Post a Comment

0 Comments